UMESIKIA kilichomtokea beki na nahodha wa Yanga, Bakari Mwamnyeto? Basi kama hujasikia soma hapa.
Baada ya dakika 90 za ugenini dhidi ya Dodoma Jiji zilizokatisha ubabe wa timu hiyo ikipogea kipigo cha mabao 3-2 ukiwa ni mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Mei 13 mwaka huu, jamaa alikutana na mazito.
Mwamnyeto ambaye alijifunga bao moja kwenye mchezo huo kisha lile la tatu akikwepa kupiga kichwa akitaka kumuachia kipa Hussein Masalanga na mpira kujaa wavuni, mabao hayo yamefanya mashabiki wa Yanga kumjia juu.
Beki huyo amekuwa akipokea maneno makali kutoka kwa mashabiki wa Yanga, wengine wakimtuhumu vikali hatua ambayo ilimlazimu kuwaomba makocha wake wasimjumuishe kwenye mchezo wa wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB dhidi ya JKT Tanzania.
Baada ya mchezo huyo ambao Yanga ilishinda 2-0 na kufuzu nusu fainali, Mwanaspoti lilimtafuta kocha wa Yanga, Abdihamid Moallin ambaye alikiri kwamba walilazimika kumpumzisha Mwamnyeto baada ya saikolojia yake kuvurugika kutokana na yale yaliyotokea kwenye mchezo dhidi ya Dodoma Jiji.
Moallin aliwaangukia mashabiki wa Yanga kutowaondoa mchezoni wachezaji wa timu hiyo kutokana na umuhimu wa utululivu katika michezo saba iliyosalia, ambapo makosa yoyote yanaweza kusababisha shida ndani ya kikosi hicho.
“Nikweli tulilazimika kumpumzisha Mwamnyeto, alikuja akaomba akiona hayupo sawa, unajua tunafahamu kwamba matokeo ya kupoteza sio kitu rahisi kukubalika sio tu kwa mashabiki hata sisi na wao kama wachezaji,” amesema Moallin.
“Tunapopoteza mechi watu wa kwanza ambao wanaumia ni mashabiki na tunaposhinda watu wa kwanza tunaowafikiria ni mashabiki wetu, sisi kama makocha tunajua kila kosa la mchezaji ndio maana tunawapa nafasi ya kujisahihisha.
“Tunatakiwa kuendelea kuwa imara, nimefurahi leo (juzi) wachezaji wamecheza kwa umakini mkubwa (dhidi ya JKT), angalia tumekuwa na utulivu mkubwa eneo la ulinzi, katikati pia tulifanya mambo kwa umakini sana, kule mbele wakamaliza mechi mapema, hii maana yake ni kwamba hata wachezaji wanajua walikosea na matokeo kama yale hayastahili kwenye timu kubwa kama hii inayotaka ubingwa, mashabiki tunawapenda wawasamehe wachezaji.”
Kwenye mchezo dhidi ya JKT Tanzania, kikosi cha Yanga kilichoanza kilikuwa na badiliko moja pekee, ikimkosa Mwamnyeto na nafasi yake ikichukuliwa na Frank Assinki ambaye kwenye safu ya ulinzi ya timu hiyo, walionekana kutulia wakicheza kwa maelewao pamoja na kipa wao Djigui Diarra.
Kauli hiyo ya Moallin ikaongezewa nguvu na Ofisa Habari wa Yanga, Ally Kamwe ambaye aliwataka mashabiki kutoendelea kuwapa ugumu wachezaji wa timu hiyo, akisema bado wanafuatilia maendeleo ya Mwamnyeto ambaye ameonekana kuathirika zaidi na namna mashabiki walivyomtuhumu kwa matokeo ya mechi dhidi ya Dodoma Jiji.
“Niwaombe mashabiki wetu, hawa ndio wachezaji wao, wanaweza kufanya makosa basi wasipitilize kwa kuwa wakali kutokana na yale yanayotokea kwenye mechi zetu, bado ni wachezaji hawahawa tunawategemea kwenda kukamilisha malengo yetu,” amesema Kamwe.
