AZAM imekata tiketi ya kucheza nusu fainali ya Kombe la Shirikisho la CRDB ambapo itakutana na Yanga, baada ya kupata ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mashujaa, mechi ya robo fainali iliyopigwa leo Mei 17, 2026 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma.
Bao pekee la kiungo mshambuliaji Idd Seleman ‘Nado’ alilofunga dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza kwa faulo, limetosha kuivusha Azam kucheza nusu fainali.
Mpira huo uliopigwa na Nado, ulimuacha kipa wa Mashujaa, Erick Johola akiwa hana la kufanya akishtukia nyavu zikitikiswa.
Azam ilionekana kuwa na utulivu wa pasi kipindi cha pili, tofauti na kipindi cha kwanza ambapo timu zilikuwa zinashambuliana kwa zamu.
Mechi za nusu fainali ambazo zitachezwa Juni 20 na 21 mwaka huu, Azam itapambana na Yanga, ikikumbushia dabi nyingine ya Dar es Salaam kwa timu hizo msimu huu ambapo hadi sasa Yanga ndiyo mshindi kwani ilishinda kwa penalti 5-4 katika fainali ya Kombe la Mapinduzi 2026, kisha zikatoka 0-0 kwenye ligi.
Baada ya nusu fainali hiyo, timu hizo zitakutana tena kwenye ligi, Juni 24 mwaka huu.
Kitendo cha timu hizo kukutana katika nusu fainali, inatajwa itakuwa dabi ya ushindani wa hali ya juu na mvuto mkubwa kwa mashabiki.
Staa wa zamani wa Yanga na Taifa Stars, Peter Tino, amesema: “Ukiachana na Dabi inayozikutanisha Yanga na Simba, nyingine kali ni Yanga ikicheza dhidi ya Azam mechi zake ni ngumu na za ushindani wa juu.”
Staa mwingine aliyechangia hilo ni kipa wa zamani wa Yanga, Simba na Mtibwa Sugar, Said Mohamed ‘Nduda’ aliyesema: “Itakuwa mechi ya presha zaidi kuliko zingine, ingawa matokeo ya dakika 90 yanaweza yakashangaza.”
