Hali ya kiafya ya mwanamuziki Abdalla Hemba bado teteHali ya kiafya ya mwanamuziki Abdalla Hemba bado tete

Dar es Salaam. Msanii wa muziki wa dansi wa bendi ya Mlimani Park Orchestra ‘Sikinde Ngoma ya Ukaye’, Abdalla Hemba, ameendelea kupambana na hali ya kiafya baada ya kulazwa katika Hospitali ya Rufaa ya Temeke, Dar es Salaam, huku familia yake ikisema hali yake imekuwa tete zaidi kuliko ilivyokuwa awali.

Kwa mujibu wa kaka yake mkubwa, Ramadhani Hemba, msanii huyo amelazwa katika wodi namba tatu ya hospitali hiyo kwa siku sita sasa baada ya hali yake kuzorota ghafla, tofauti na siku za nyuma ambapo alikuwa akipelekwa hospitalini kuwekwa dripu na kurudishwa nyumbani.

Haongei, hatambui watu

Ramadhani amesema safari hii hali ya mdogo wake imewatia hofu kubwa kwa sababu haongei kabisa na ameshindwa hata kutambua watu wanaomzunguka.

“Kwa sasa hali yake ni mbaya sana, amelazwa Temeke wodi namba tatu. Ana siku ya sita sasa hospitalini, haongei kabisa, unamwangalia anaangalia tu lakini hakutambui. Hata ukimuita hawezi kuitikia wala kuelewa nani yupo pembeni yake,” amesema Ramadhani.

Amesema kabla ya kufikia hatua hiyo, walikuwa wakimpeleka hospitalini mara kwa mara kwa ajili ya kuwekewa dripu kutokana na mwili kudhoofika na kushindwa kula, lakini baada ya kufanya hivyo kwa mara ya sita ndipo madaktari wakaamua kumlaza moja kwa moja kutokana na hali kuwa mbaya zaidi.

“Tumekuwa tukimpeleka hospitali zaidi ya mara tano akiwekewa dripu anarudi nyumbani, lakini safari hii alizidiwa kabisa. Akaanza kupoteza uwezo wa kuzungumza na hata kutomtambua mtu yeyote ndipo madaktari wakaamua abaki hospitali chini ya uangalizi wa karibu,” amesema.

Awekewa mpira wa chakula

Kwa mujibu wa kaka huyo, Hemba kwa sasa amewekewa mpira maalumu wa kupitisha chakula baada ya kushindwa kula kawaida kutokana na kutapika kila anapojaribu kula.

“Amekuwa akitapika kila akila, ndiyo maana wakaamua kumuwekea mpira wa kupitisha chakula. Kiukweli hali yake inasikitisha sana maana hata nguvu mwilini hana kabisa,” amesema Ramadhani.

Ameongeza kuwa madaktari walimfanyia kipimo cha CT Scan kichwani ili kuangalia kama kuna tatizo lolote kwenye ubongo, lakini majibu hayakuonyesha tatizo hilo, huku vipimo vingine vikionesha kuwa msanii huyo anakabiliwa na maradhi mbalimbali yakiwemo TB, kisukari, matatizo ya figo pamoja na kushindwa kupumua.

“CT Scan ya kichwa imeonyesha hakuna tatizo kubwa upande huo, lakini vipimo vingine vimeonyesha ana matatizo mengi kwa pamoja. Kuna TB, kisukari, figo zina shida na pia mfumo wa upumuaji nao una matatizo. Madaktari wanaendelea kupambana kuhakikisha hali yake inatengamaa,” amesema.

Mwanzo wa ugonjwa wake

Taarifa za kuzorota kwa afya ya Hemba zinakuja ikiwa ni wiki chache tangu Mwananchi lifike nyumbani kwake Aprili 19, 2026 na kufanya mahojiano maalumu ambapo msanii huyo alifunguka kuhusu safari yake ya kuugua na namna alivyoanza kupambana na maradhi hayo.

Katika mahojiano hayo, Hemba alisema safari ya ugonjwa wake ilianza Machi 22, 2026 baada ya kugundulika kuwa na malaria na UTI, hali iliyomlazimu kulazwa Hospitali ya Malawi iliyopo Kiwalani kwa siku moja kabla ya kuruhusiwa kurejea nyumbani.

“Nilianza kuumwa ghafla, wakagundua ni malaria na UTI. Nikalazwa hospitali ya Malawi siku moja, nikarudi nyumbani lakini hali ikazidi kuwa mbaya zaidi mchana wake, ilibidi wanipeleke tena hospitali,” alisema Hemba.

Baadaye alihamishiwa Hospitali ya Temeke ambako alilazwa kwa siku tatu huku hali yake ikiendelea kuwa tete, kabla ya vipimo zaidi kubaini kuwa alikuwa pia akisumbuliwa na kisukari, BP, nimonia pamoja na TB.

Miguu kukosa nguvu

Katika mahojiano hayo ya awali, Hemba alisema athari za magonjwa hayo zilimfanya apoteze nguvu kabisa miguuni na kushindwa kutembea kwa muda.“Miguu yangu ilikuwa haina nguvu kabisa, sikuweza hata kutembea. Lakini nilikuwa nimeanza kupata nafuu kidogo na kuanza kutembea taratibu japo si kwa nguvu ile ya zamani,” alisema.

Pia alieleza kuwa changamoto kubwa aliyokuwa akiipitia ni kushindwa kula kwa sababu kila alipokula alikuwa akitapika, huku pia akisumbuliwa na kwikwi zilizokuwa zikimsumbua kwa muda mrefu.

Kwa sasa familia yake imeendelea kuwaomba Watanzania kumuombea huku wakiamini bado kuna matumaini ya hali yake kubadilika na kurejea katika afya njema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *