New York, Marekani. Ijumaa wiki iliyopita, jarida la Forbes lilitoa orodha ya wanamichezo wanaoingiza kiasi kikubwa cha fedha kwa mwaka.
Katika orodha hiyo nyota wa soka, Cristiano Ronaldo alitajwa kuwa kinara akiweka kiasi cha Dola 275 mfukoni kwa mwaka na nafasi ya pili yupo mchezaji wa mpira wa kikapu, Stephen Curry ambaye kwa mwaka anaingiza kiasi cha Dola 157 milioni.
Curry mwenye umri wa miaka 38, kwa sasa anaichezea Golden State Warriors katika nafasi ya gadi na ana kimo cha Mita 1.88.
Nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry. Picha na Mtandao
Chanzo cha noti
Uwezo mkubwa wa kucheza mpira wa kikapu umechangia kwa kiasi kikubwa Curry awe anavuna mabilioni ya fedha kwa mwaka, zikiingia kupitia mishahara anayolipwa pamoja na mikataba binafsi ya wadhamini wanaotumia jina au picha zake kujitangaza.
Kwa mwaka mchezaji huyo anavuna zaidi ya Dola 56 milioni, kiasi cha fedha ambacho ni mjumuisho wa mishahara ambayo nyota huyo analipwa na Golden State Warriors.
Fedha nyingine zaidi ya Dola 100 milioni ni zile anazokusanya kupitia mikataba mbalimbali ya matangazo ambayo amesaini na kampuni tofauti tofauti.
Mfano wa kampuni ambazo Curry anatangaza bidhaa na huduma zao ni Rakuten na Under Armour.
Nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry. Picha na Mtandao
Rekodi, mafanikio tele
Curry amekuwa akitambulika kama mlengaji wa muda wote katika mpira wa kikapu na hito imechangiwa na uwezo wake mkubwa wa kufunga pointi kwa mitupo ya bali.
Uwezo wake wa kucheza mchezo huo umemuwezesha kushinda tuzo nyingi binafsi na pia kuisaidia timu yake kupata mafanikio.
Ameshinda mataji manne ya NBA ambayo ni ya mwaka 2015, 2017, 2018 na 2022 huku pia akiiongoza timu ya taifa ya Marekani kushinda mara moja medali ya dhahabu ya Olimpiki na mara mbili mashindano ya dunia ya kikapu.
Curry amefanikiwa mara mbili tofauti kushinda tuzo ya Mchezaji Bora wa NBA na ameteuliwa mara 12 kuingia katika kikosi bora cha Ligi ya Mpira wa Kikapu Marekani.
Nyota wa Golden State Warriors, Stephen Curry. Picha na Mtandao
Familia, maisha binafsi
Curry alizaliwa Machi 14, 1988 katika kitongoji cha Akron, kilichopo Ohio, Marekani na elimu ya juu aliipata katika Shule ya Charlotte Christian.
Kisha alijiunga na Chuo cha Davidson alichosoma kuanzia 2006 hadi 2009 na hapo ndipo kipaji chake kilipoonekana hadi leo hii ambapo amekuwa miongoni mwa wachezaji nyota wa mpira wa kikapu duniani.
Stephen Curry mwaka 2018 alifunga ndoa na Ayesha Curry na hadi sasa wamebahatika kupata watoto wanne ambao ni Riley, Ryan, Canon na Caius.
Baba wa mchezaji huyo wa kikapu anaitwa Dell na mama yake anaitwa Sonya Curry.
