Dar es Salaam. Shule ya Msingi Darajani inakabiliwa na changamoto ya mazingira ya kujifunzia ambayo yameelezwa kuathiri moja kwa moja utulivu wa wanafunzi na ubora wa ufundishaji.
Shule hiyo iliyopo Kata ya Kimanga, Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam imezungukwa na barabara kuu ya kuelekea Tabata Kimanga pamoja na njia nyingine inayoingia mtaani, ambayo vyombo vya moto hupishana.
Kwa mujibu wa takwimu za Best zinazotolea na Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) za mwaka 2025 shule hiyo ilikuwa na wanafunzi ni 1254 na walimu ni 62.
Hata hivyo, changamoto kubwa eneo la shule limetumika kama njia ya mkato ya wapita njia, hali inayosababisha usumbufu wakiwamo wafanyabiashara na hata wasambazaji wa huduma mbalimbali wanaopita wakiwa na vispika.
Aidha, wazikaji wanaotumia njia kuelekea makaburini yaliyopo nyuma ya madarasa wamekuwa wakikatisha katikati ya uwanja wa shule, hali inayoongeza usumbufu na kuhatarisha usalama wa wanafunzi.
Baadhi ya madarasa ya shule ya msingi Darajani iliyopo kata ya Kimanga, jijini Dar es Salaam yakiwa pembezoni mwa mtaa unaoelekea kwenye makazi ya watu.
Hali hiyo inaonesha kwa uwazi namna shule hiyo ilivyo katika mazingira yasiyo rafiki kwa ujifunzaji, kinyume na matarajio ya eneo linalopaswa kuwa salama, tulivu na lenye kumwezesha mwanafunzi kujifunza bila kuingiliwa na shughuli za kijamii zinazozunguka shule hiyo.
Kelele, hofu na usumbufu wa kila siku
Mwanafunzi mmoja ambaye tunahifadhi jina lake anasema kukosekana kwa utulivu darasani kunasababishwa na kelele zinazotokana na wafanyabiashara wanaopita katikati ya eneo la shule, pamoja na shughuli zinazofanyika jirani na makaburi yaliyopo nyuma ya madarasa ya la nne, sita na saba.
Anasema hali hiyo huwafanya walimu kushindwa kuendelea na somo ipasavyo, mara nyingi hulazimika kusubiri shughuli za mazishi zimalizike.
Anasema wakati wa matukio ya mazishi, wanafunzi huvurugwa kisaikolojia kwa kushangaa au kusikiliza kinachoendelea nje ya madarasa yao, jambo linalokatiza umakini wa masomo.
“Wakati mwingine tunakuwa darasani, lakini tunaendelea kusikia sauti za watu kutoka makaburini nyuma ya shule. Mwalimu hulazimika kusimama kwanza mpaka mambo yatulie ndipo aendelee kufundisha,” anasema mwanafunzi huyo.
Wafanyabiashara wakikatisha katikati ya shule ya msingi Darajani iliyopo kata ya Kimanga, Wilayani Ilala, jijini Dar es Salaam wakati wanafunzi wakiwa wanaendelea na masomo
Anasema kelele za magari ya matangazo yanayopita barabarani yanachangia kukosekana kwa utulivu kwa sababu unapopigwa muziki wanafunzi huanza kuimba wakiwa darasani.
Mwanafunzi mwingine, anasema kipindi cha mitihani ya Taifa hufungwa utepe ili kuzuia watu wasipite katika eneo la shule na pindi inapomalizika huondolewa. Hata hivyo, bado makelele ya barabarani husikika kwani ni karibu na kuwa kero kwao.
“Kipindi cha mitihani wanaweka utepe ili watu wasipite kwa siku mbili ikimalizika tu utaratibu ni uleule hadi wale wa kusajili laini wanapita na spika zao bila kujua kama wanafunzi wapo darasani,” anasema.
Wapita njia na wafanyabiashara
Baadhi ya wapita njia na wafanyabiashara wanaokatiza katika eneo hilo, wanasema wamekuwa wakilitumia eneo hilo kama sehemu ya kawaida kwa kuwa ni njia rahisi na ya mkato inayowawezesha kufika upande mwingine.
Makaburi ambayo hayana uzio yaliyopo nyuma ya madarasa ya shule ya msingi Darajani iliyopo kata ya Kimanga, Wilayani Ilala jijini Dar es Salaam
Mmoja wa wapita njia, James Hosea anasema eneo hilo limekuwa sehemu ya kawaida, hivyo kulipita si jambo jipya kwao.
“Tunapita hapa kwa sababu ni njia fupi ya kufika upande wa pili tukisema tufuate barabara tunazunguka na hakuna nafasi ya kupita watembea kwa miguu,” anasema Hosea.
Mfanyabiashara, Angelina Mosha anakiri wanafanya makosa kupita eneo hilo la shule kwa kuwa, wanawakosesha utulivu watoto na kutaka kujua nje amepita nani.
“Ili kukomesha hili kuna haja Serikali kuweka uzio hiki ambacho tunafanya si sawa hata kama mtoto wangu hasomi hapa tunaondoa utulivu darasani hata kufanya jambo baya ni rahisi,”anasema Angelina.
Wasiwasi wa usalama
Mmoja wa wazazi, Kelvin Marwa anasema kutokana na changamoto hizo wazazi wamekuwa wakifanya vikao vya pamoja na mwaka 2022 walikubaliana kuchangia matofali kwa ajili ya ujenzi wa uzio wa shule pamoja na ukuta wa makaburi ulioanguka na kuwa kero kwa wanafunzi.
Anasema makubaliano ya kikao ni kila mwanafunzi anapojiunga na shule hulipia matofali Sh12,500 kwa ajili ya kusaidia ujenzi huo ili kuimarisha usalama wa watoto na mazingira ya kujifunzia.
“Tulikubaliana kwenye vikao vyetu kila mwanafunzi achangie matofali kwa ajili ya kujenga uzio na kurekebisha ukuta wa makaburi ulioporomoka. Hata kikao cha mwisho cha Februari mwaka huu kilisisitiza michango hiyo ikamilike ifikapo Juni,” anasema Marwa.
Pia, anasema wazazi wamekuwa wakishiriki kujaza vifusi kwenye makorongo yaliyokuwa yametawala eneo la shule na kusababisha watoto kuumia mara kwa mara licha ya kusombwa na maji.
Anatolea mfano tukio la Mei 12, 2026 mwanafunzi mmoja aliumia mkono kutokana na mazingira hatarishi ya shule hiyo.
Mzazi mwingine, Hamidu Seif anadai kuwepo kwa shughuli zisizofaa karibu na shule, ikiwamo matumizi ya dawa za kulevya, jambo linaloongeza hofu ya maadili ya watoto.
“Watoto wanakutana na harufu ya bangi kutokana na shughuli zinazofanyika jirani na mazingira ya shule hivyo tunahofia maadili yao,” anasema Seif.
Muongozo wa elimu
Kwa mujibu wa Muongozo wa Elimu wa mwaka 2020, kifungu cha 2.1.1.3 shule ya kutwa inapaswa kuwa na miundombinu muhimu ikiwamo madarasa, ofisi, maktaba, vyoo, jiko, bwalo, viwanja vya michezo, huduma ya maji na chumba cha huduma ya kwanza.
Hata hivyo, muongozo huo unasisitiza wazi uzio kuzunguka shule ni muhimu kwa usalama wa wanafunzi na watumishi.
Kifungu cha 11 cha muongozo huo kimeweka adhabu kwa kunukuu Sheria ya Elimu ya Mwaka 2002 Sura ya 353, Sehemu ya 8 kifungu na 60 (g) ikiwa ni pamoja na kulipa faini, kufungiwa kusajili wanafunzi kwa muda na kufutiwa usajili wa shule. Adhabu hizo zinaweza kutolewa ama moja au zote kwa pamoja.
Licha ya muongozo na sheria kuzungumzia hayo katika Shule ya Msingi Darajani imekuwa na upungufu ikiwamo viwanja vya michezo, maktaba, jiko, bwalo na chumba cha huduma ya kwanza pamoja na uzio.
Kwa mujibu wa Sheria ya Mtoto Na. 21 ya mwaka 2009 nchini ni haki ya mtoto kupata ulinzi, malezi bora na mazingira salama yatakayoweka mbele maslahi yake ya msingi.
Mazingira huamua ubora wa ufaulu
Mtafiti binafsi wa masuala ya elimu, Dk Muhanyi Nkoronko anasema mwanafunzi anapaswa kusoma katika mazingira salama, tulivu na rafiki yatakayomwezesha kuelewa vizuri masomo bila kuathiriwa na kelele au mwingiliano wa shughuli za kijamii.
Anasema baadhi ya shule zilizopo katikati ya makazi ya watu na maeneo yenye shughuli nyingi za kijamii zimekuwa zikikabiliwa na changamoto zinazopunguza ubora wa ujifunzaji na ufundishaji.
Dk Nkoronko anasema baadhi ya shule zimejengwa katika maeneo yasiyo sahihi kutokana na upangaji mbovu wa matumizi ya ardhi na kutokuzingatiwa kwa mahitaji muhimu ya mazingira ya elimu wakati wa kutenga maeneo ya shule.
“Makosa makubwa yaliyofanyika ni upangaji mbaya wa maeneo ya shule. Kuna shule nyingi zimezungukwa na makazi au shughuli nyingine za kijamii ambazo zinaathiri ujifunzaji,” anasema Dk Nkoronko.
Anasema kutokuwepo kwa uzio katika shule nyingi zilizopo mijini kunasababisha wanafunzi kuvurugwa wanapokuwa darasani, jambo linalopunguza umakini wao katika masomo.
Kisaikolojia imekaaje?
Mwanasaikolojia Ramadhani Massenga anasema uwepo wa makaburi karibu na mazingira ya watoto kujifunzia unaweza kuwaathiri kisaikolojia na kushusha uwezo wao wa kuzingatia masomo.
Anasema hata watu wazima wanapoona eneo lenye maziko au maiti hupata mawazo na kuvurugika kiakili, hivyo kwa watoto athari hiyo huwa kubwa zaidi kutokana na umri wao mdogo.
“Kama mtu mzima tunapoona sehemu kuna maziko kuna namna tunavurugika mawazo na kuanza kufikiria kuhusu maisha, sasa unaweza kufikiria kwa mtoto mdogo hali hiyo inakuwa kubwa zaidi,” anasema.
Massenga anasema watoto wanahitaji mazingira yenye utulivu wa akili na furaha ili waweze kuelewa wanachofundishwa darasani, kwa kuwa hisia zao zina mchango mkubwa katika maendeleo yao ya kielimu.
“Mtoto ili aweze kuelewa darasani inahitajika awe na mawazo chanya na awe katika hali nzuri ya kihisia, kwa sababu uwezo wake darasani unategemea hali ya hisia zake hivyo mazingira yenye hofu, huzuni au usumbufu kama watu kupita karibu na makaburi yanaweza kuwafanya watoto washindwe kutulia na kuelekeza akili kwenye masomo,” anasema Massenga.
Nini kifanyike
Dk Nkoronko anasema hatua ya haraka inayotakiwa kuchukuliwa ni Serikali, jamii na wadau wa elimu kushirikiana kuboresha mazingira ya shule kwa kujenga uzio utakaotenganisha eneo la shule na shughuli za kijamii zinazofanyika nje.
“Uzio utasaidia kutenganisha shughuli za kijamii na eneo la shule, hii itawafanya wanafunzi wajikite zaidi kwenye masomo bila kusumbuliwa na mazingira ya nje,” anasema Dk Nkoronko.
Pia, anasema kuna haja ya Serikali kuhuisha miongozo ya ujenzi wa shule pamoja na kuhakikisha halmashauri zote zinafuata utaratibu sahihi wa upangaji wa maeneo ya elimu kabla ya kuruhusu shule kujengwa.
“Kuna umuhimu wa kuwa na miongozo madhubuti ya school mapping ili shule zijengwe katika maeneo sahihi yenye mazingira salama na rafiki kwa ujifunzaji. Hii itasaidia kupunguza usumbufu, utoro na changamoto nyingine zinazoweza kuathiri maendeleo ya wanafunzi,” anasema.
Kauli ya Serikali
Akizungumza na Mwananchi Mei 14, 2026 Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Edward Mpogolo anasema Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam katika bajeti yake ya 2026/27 imetenga fedha za ujenzi wa ukuta katika shule zake ili kulinda usalama wa watoto na mali za shule.
Aprili 30, 2026 Mpogolo alisema shule nyingi zimekuwa wazi kwa muda mrefu jambo lililosababisha watu wasiokuwa na shughuli za kielimu kupita ndani ya maeneo ya shule na kuvuruga utaratibu wa masomo.
“Zamani tulikuwa na shule ambazo hazina uzio kabisa. Watu wanapita katikati ya shule muda wowote, wengine wanazungumza, wengine wanacheka, hali ambayo inaathiri umakini wa wanafunzi darasani,” alisema Mpogolo.
Alisema ujenzi wa uzio ni sehemu ya mkakati wa muda mrefu wa wilaya na kila mwaka fedha zinatengwa kwa ajili ya kujenga uzio katika baadhi ya shule huku lengo likiwa kufikia shule zote ndani ya miaka kadhaa ijayo.
Anasema utekelezaji wa mpango huo unahitaji kiasi kikubwa cha fedha kutokana na ukubwa wa mahitaji yaliyopo katika shule nyingi za Ilala.
Hata hivyo, Mpogolo alikiri kuwepo kwa changamoto katika baadhi ya maeneo ikiwamo migogoro ya mipaka kati ya shule na makazi ya wananchi, hasa maeneo yaliyoendelea kujengwa kiholela karibu na shule.
“Kuna shule zilijengwa zamani, lakini sasa zimezungukwa na makazi ya watu. Hivyo kabla ya kujenga uzio tunalazimika kwanza kuthibitisha mipaka ili kuepusha migogoro,” alisema.
Aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya wilaya itashirikiana na wataalamu wa ardhi na mipango miji kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kwa kuzingatia sheria na taratibu zote.
Hali ya matokeo
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita shule hiyo imekuwa na ufaulu wa wastani wa daraja B (Nzuri sana) kwa matokeo ya kumaliza elimu msingi.
Licha ya wastani wa ufaulu wa shule kubaki vilevile katika kipindi hicho mwaka 2025 ufaulu ulipunguza zaidi ikilinganishwa na miaka mwili iliyopita.
Baadhi ya madarasa ya shule ya msingi Darajani iliyopo kata ya Kimanga, jijini Dar es Salaam yakiwa pembezoni mwa mtaa unaoelekea kwenye makazi ya watu.
Takwimu za Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) zilionesha upungufu wa asilimia 11 wa wastani wa alama za ufaulu kwa mwaka 2025 hadi kufikia wastani wa alama 181.72 ikilingaishwa na 204.99 mwaka 2024. Mwaka 2023 wastani ulikuwa alama 185.21.
Vile vile licha ya idadi kubwa ya wanafunzi kufaulu kwa wastani wa madaraja A, B na C kwa miaka ya karibuni wapo wanaofaulu kwa wastani wa daraja D.
Mwaka 2023 wahitimu wote 145 walifaulu kwa wastani wa A, B na C. Hata hivyo, mwanafunzi mmoja alipata alama D kati ya 152 waliohitimu mwaka uliofuata na wanafunzi saba walipata daraja D mwaka 2025.
Ufaulu wa masomo pia umeshuka mwaka 2025. Takwimu za Necta zinaonesha kati ya masomo sita yanayofanyiwa mtihani Hisabati na Kingereza yamekuwa na ufaulu wa daraja C(wa chini zaidi) kwa kipindi chote kilicho fanyiwa uchambuzi, lakini mwaka 2025 liliongezeka somo la Maarifa na Stadi za Kazi, huku masomo mengine yakuendelea kuwa na ufaulu wa wastani wa daraja B.
