Kilio cha mawakala wanavyopigwaKilio cha mawakala wanavyopigwa

Mwanza/Dar. Wakati biashara ya uwakala wa huduma za kifedha ikiendelea kuvutia vijana wengi kutokana na mzunguko wake wa haraka wa fedha, mawakala wamejikuta wakikumbana na wimbi jipya la utapeli unaowaingiza katika hasara.

Licha ya kuonekana biashara yenye faida na uaminifu kwa wateja, baadhi ya mawakala wamepoteza mamilioni ya fedha kupitia mbinu za kitapeli zinazobuniwa kila siku.

Hali inayotishia usalama wa biashara zao na kuathiri imani katika huduma za kifedha za kidijitali.

Kwa mujibu wa mawakala, matumizi ya fedha kwa njia ya mitandao yanavyoongezeka nao wanajikuta katika mitego mipya ya kutapeliwa mara kwa mara.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni katika Soko la Buhongwa, jijini Mwanza, Wakala John Justine amesema hasara wanazopata si ndogo, kwa kuwa baadhi wamepoteza mamilioni ya fedha kwa tukio moja, hali inayowalazimu wengine kufunga biashara.

Mteja akipata huduma ya kifedha kwa wakala katika eneo la Tambukareli Kata ya Mkuyuni jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Amesema matapeli huanza kwa kujenga uaminifu kabla ya kuiba kwa kuwa,  mteja wa kawaida huku akisoma mazingira halisi ya eneo ilipo biashara.

“Matapeli kwa asilimia kubwa huanza kwa miamala midogo ili kufahamu mtoa huduma yupo makini kwa kiasi gani, kabla hajatapeli; akishagundua udhaifu ndipo anapoanza kutoa kiasi kikubwa kwa siku kadhaa kisha kuiba,”amesema Justine.

Amesema uzoefu humjengea uaminifu kwa mtoa huduma kwa kujifanya anatoa fedha hata akiwa mbali kisha anazipitia baadaye, mazoea hayo hufikia hatua ya kuomba fedha na kumhakikishia wakala atamtumia kwa sababu ana haraka.

“Kutokana na mazoea hayo ya siku kadhaa, wakala humuamini haraka na ndipo baadaye anajikuta ameingia kwenye mtego wa kutapeliwa bila kujua,”amesema.

Wakala mwingine, Leila Kisiel amesema mbinu nyingine ni uombaji wa simu za mawakala, hutumia dakika chache kufanya analolitaka kwa madai kuwa, simu yake ina changamoto.

Amesema hutumia fursa hiyo kuweka namba yake na kuandika jina la kampuni ya fedha kisha kutuma ujumbe mfupi wa maneno (SMS) uliohaririwa kwa kuonesha umetoka kwenye kampuni husika.

“Kuna dada alitapeliwa Sh1.8 milioni kwa njia ya SMS aliponiambia nilitaka kufahamu kama alimpatia simu mteja, baada ya kujibu ndiyo niliipigia ikatoka jina la kampuni,”amesema Kisiel.

Matapeli kutumia fursa

Wakala wa huduma za fedha Kariakoo, jijini Dar es Salaam, Sifa Mwakibete ametapeliwa Sh7 milioni kwa kutumiwa ujumbe hewa ulioboreshwa na kuonekana kama umetumwa rasmi kutoka kampuni ya simu.

Amesema matapeli hao walifika wakitaka kutoa fedha, ndipo alipowaambia wakishatoa wamuoneshe ujumbe ili kuhakiki kwa kuwa, simu yake ilikuwa imejaa, hivyo ujumbe unachelewa kuingia.

“Sikujua kama niliwapa nafasi ya kuniibia vizuri, walikuja wateja zaidi ya watatu wakihitaji kutoa Sh500,000 na kuendelea; na hii ilitokana na kutoona ujumbe kwa sababu ya kujaa kwa ujumbe,” amesema Sifa.

Amesema katika mazingira hayo, matapeli hao walikuwa wakipeana maelekezo kwa zamu huku wakichukua fedha kidogokidogo, mmoja alichukua Sh2 milioni na mwingine Sh1.5 milioni, kabla ya wengine kuendelea kufanya miamala tofauti hadi kiwango hicho kufikia zaidi ya Sh7 milioni.

Sheria inasemaje?

Mwongozo wa Uwakala wa Kibenki wa mwaka 2017 unaeleza kuwa, wakala anatakiwa kuthibitisha miamala yote kabla ya kutoa fedha, kutunza siri za taarifa za mteja, kuepuka matumizi yasiyo rasmi ya vifaa vya miamala pamoja na kuripoti viashiria vya udanganyifu au utapeli mara moja.

Pia, Kanuni za Fedha za Kielektroniki za mwaka 2015 inazitaka taasisi za fedha na mawakala kuhakikisha mifumo yao inalindwa dhidi ya udanganyifu, matumizi mabaya ya miamala na wizi wa kimtandao.

Pia, Kifungu cha 53 cha Sheria ya Mifumo ya Malipo ya Taifa ya mwaka 2015, Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kimepewa mamlaka ya kusimamia na kutoa miongozo kwa watoa huduma za malipo pamoja na mawakala wao ili kuhakikisha usalama wa mifumo ya fedha za kielektroniki.

Licha ya uwepo wa sheria na miongozo, watoa huduma wa fedha hawaifuati kwa sababu hakuna ukaguzi kutoka kwa wasimamizi wa malipo ya mtandaoni.

Hayo yanathibitishwa na wakala Stanslaus Moshi akisema wanapokwenda kuomba maombi ya kutoa huduma hizo hupewa miongozo na masharti ikiwamo vitabu vya kujazwa na wateja, ikihitaji na namba za vitambulisho.

“Kwa kiasi kikubwa makosa yanakuwa kwetu, tunapokwenda kusajili huduma tunapewa kila kitu ikiwamo miongozo na masharti na vitabu, lakini leo ukizunguka kwa mawakala hakuna anayetumia hivyo vitabu kujazisha wateja,” amesema Moshi.

Amesema sababu hizo zimetokana na uharaka wa wateja kwa kusema hawana muda wa kupoteza, ndiyo maana inakuwa ngumu kwa watu wanaofanya utapeli kukamatwa, kwa kuwa wao wenyewe wanakuwa wamekiuka sheria na miongozo yake.

Moshi amesema mawakala wangekuwa wanawajazisha watu fomu ingekuwa rahisi kukamata matapeli hususani wanaotumia miamala ya kwenye mitandao ya simu.

“Kwa sasa unauziwa laini haijalishi unafanyia wapi shughuli zako, wakati zamani walikuwa wanatembelea sehemu za biashara ili kupata uhakika wa eneo, lakini kwa sasa mtu anatembea na simu na namba za uwakala,” amesema.

Wakala Bahati Makubi amesema matapeli hutoa motisha ili kumshawishi wakala kufanya muamala bila kufuata taratibu zote muhimu.

“Matapeli wanajua hakuna ufuatiliaji wala kujaza fomu, ili kumlainisha wakala, anamdanganya kwa kumpa kiasi cha fedha ili kupata huduma kwa kuamini kuwa, anapata kiasi fulani nje ya kile anacholipwa,” amesema.

Mbali na hilo, amesema matapeli wanaendelea kuwaibia watu kwa sababu baadhi yao wametokea kwenye kampuni za simu au sekta zinazofanana na hiyo kwa kujua kuchezea mifumo husika.

Athari za utapeli

Mtaalamu wa Fedha na Uchumi, Sophia Mussa amesema ongezeko la matukio ya utapeli dhidi ya mawakala wa huduma za fedha linaathiri moja kwa moja ukuaji wa biashara ndogondogo na uimara wa sekta ya fedha za kidijitali nchini.

Amesema hali hiyo inapunguza imani ya wananchi katika matumizi ya huduma za fedha za kidijitali, jambo linaloweza kurudisha nyuma juhudi za Serikali za kukuza uchumi wa kisasa.

“Mawakala wengi huingia kwenye biashara hii kwa mikopo au akiba zao binafsi, hivyo wanapopoteza fedha kwa utapeli hujikuta wakiporomoka kiuchumi na wakati mwingine kufunga biashara,” amesema Mussa.

Amesema ni muhimu kwa taasisi za fedha na kampuni za simu kuongeza uwekezaji katika elimu ya matumizi salama ya mifumo ya kifedha kwa mawakala na wananchi kwa jumla.

“Teknolojia inabadilika kwa kasi na matapeli wanabuni mbinu mpya kila siku, hivyo bila elimu ya mara kwa mara na mifumo imara ya ulinzi, changamoto hii itaendelea kuongezeka,” amesema Mussa.

Ripoti za mamlaka

Kutokana na changamoto hiyo, Machi 2025 hadi Machi 2026, Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilibaini na kufungia jumla ya laini za simu 62,879, pamoja na kuzuia kufanya usajili wa laini mpya za simu kwa Vitambulisho vya Taifa (Nida) 60,177 vilivyohusika katika matukio ya ulaghai.

Hatua hizo ni muendelezo wa hatua zilizoanza kuchukuliwa na aliyekuwa Waziri ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye aliyeanzisha vita dhidi ya matapeli wa mtandaoni wanaotumia mbinu kadhaa.

Hayo pia, yalizungumzwa Aprili 30, 2026 bungeni na Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Angella Kairuki wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2026/27 na kuomba kuidhinishiwa Sh222 bilioni.

Wateja wa huduma za kifedha wakie delea kuhudumiwa eneo la Buhongwa sokoni  jijini Mwanza. Picha na Saada Amir

Novemba 22, 2024 aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Jerry Silaa alisema walikubaliana na BoT waendelee kuimarisha usimamizi wa mawakala wa huduma za fedha ikiwa ni pamoja na kuangalia uwezekano wa kuongeza masharti katika utoaji wa fedha kwa mawakala.

Hatua za Jeshi la Polisi

Kutokana na kuongezeka kwa matukio hayo, Jeshi la Polisi limeendelea kutoa elimu kwa wananchi na mawakala kuhusu mbinu za utapeli.

Akitoa elimu kwa mawakala wa huduma za fedha katika Manispaa ya Kigoma Ujiji Aprili 30, 2026, Mkaguzi wa Polisi, Ferister Kaywanga alisema ni muhimu kwa mawakala kuepuka kuwapa wateja simu wanazotumia kufanya miamala.

Alisema kufanya hivyo kunatoa mwanya kwa wahalifu kuingiza namba zao na kutuma ujumbe wa uongo unaoonesha fedha zimetumwa.

Kayangwa alitoa wito kwa mawakala kuhakiki fedha kabla ya kutoa huduma na kujiridhisha kikamilifu kwa kila muamala unaoingia na kutoka.

Pia, aliwakumbusha mawakala kuhusu umuhimu wa kushirikiana na vyombo vya usalama wanapobaini viashiria vya uhalifu kwa kutoa taarifa mapema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *