Dar es Salaam. Mbunge wa zamani wa Kisesa (CCM), Luhaga Mpina, ametangazwa kuwa Naibu Waziri Mkuu katika Baraza Kivuli la Mawaziri la Chama cha ACT Wazalendo, akiungana na makada wengine 24 wanaounda baraza hilo.
Hili ni baraza la tatu la mawaziri kivuli linaloundwa na chama hicho tangu lilipoanzisha utaratibu huo mwaka 2022, likiwa na jukumu la kufuatilia uwajibikaji wa Serikali katika maeneo mbalimbali nje ya Bunge.
Naibu Waziri Mkuu Kivuli na Waziri wa Nishati na Madini wa Chama cha ACT Wazalendo, Luhaga Mpina.
Kwa Mpina, huo ni wadhifa wa kwanza kuushika ndani ya chama hicho, tangu alipojiunga nacho kutoka Chama cha Mapinduzi (CCM), Agosti 5, 2025. Alipitishwa kugombea urais lakini baadaye akaenguliwa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).
Baraza hilo la mawaziri kivuli, limetangazwa leo, Jumatatu Mei 18, 2026 na Kiongozi wa chama hicho, Dorothy Semu katika mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika makao Makuu ya ACT Wazalendo, Magomeni, Dar es Salaam.
“Matokeo ya uchaguzi wa mwaka 2025 yameendelea kutoa uwakilishi mwembamba sana wa upinzani bungeni hali ambayo imekifanya chama kuendelea kutumia mifumo mbadala ya kuisimamia Serikali, kuikosoa na kuibana ili iwajibike kwa wananchi,” amesema.
Akitangaza baraza hilo, Semu amesema baraza la mwaka huu linajumuisha wabunge waliopo bungeni na wanasiasa wenye uzoefu ndani ya chama hicho ili kulipa nguvu na uwezo wa kuisimamia na kuishauri vema Serikali.
Katika muundo huo mpya, aliyekuwa kada wa muda mrefu wa chama hicho, Issihaka Mchinjita, ametuliwa kuwa Waziri Mkuu Kivuli. Mchinjita ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho bara.
Waziri Mkuu wa Baraza Kivuli wa ACT Wazalendo, Isihaka Mchinjita.
Mpina yeye akiteuliwa kuwa Naibu Waziri Mkuu Kivuli na Waziri wa Nishati na Madini. Mpina amewahi kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi wakati wa utawala wa awamu ya tano.
Aidha, Idrisa Kweweta ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi wa Baraza hilo.
Katika mgawanyo wa kisekta, Nagy Kaboyoka, ameteuliwa kuwa Msemaji wa Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge na Uratibu pamoja na kuwa Mnadhimu wa Baraza, huku Ado Shaibu akipewa Ofisi ya Rais, Mipango, Fedha na Hifadhi ya Jamii.
Ofisi ya Rais, Mipango, Fedha na Hifadhi ya Jamii, Ado Shaibu.
Ado ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Pavu Juma, ameteuliwa kusimamia Ofisi ya Rais, Utumishi na Utawala Bora, akisaidiwa na Samson Marwa, wakati Kulthum Mchuchuli, akisimamia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa, Serikali za Mitaa na Maendeleo Vijijini akisaidiwa na Shingo Bakari.
Wengine ni Said Mbarouk, aliyepangiwa Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano huku Rashid Ali, akiteuliwa Wizara ya Ulinzi, Mambo ya Ndani na Usalama wa Raia akisaidiwa na Hussein Kalyango.
Peter Madeleka, ameteuliwa kuwa msemaji wa Katiba na Sheria, Fatma Fereji, akikabidhiwa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki na Dk Elizabeth Sanga akipewa sekta ya Afya na Ustawi wa Jamii.
Aidha, Bazililo Mbwilo, ameteuliwa kusimamia Kilimo, Umwagiliaji na Maendeleo ya Ushirika akisaidiwa na Frank Ruhasha, huku Riziki Ngwali akipewa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia.
Wengine ni Mtututa Abdallah, aliyepangiwa wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Miundombinu, Janeth Rithe aliyepewa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu na Abdul Nondo amekuwa msemaji Wizara ya Ajira, Kazi na Maendeleo ya Vijana.
Pia, Yasinta Awiti, ameteuliwa msemaji wa Maji, Mazingira na Mabadiliko ya Tabia Nchi, Shangwe Ayo akikabidhiwa Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari huku Mwanaisha Mndeme, akipewa Viwanda na Biashara na Emmanuel Ntobii akiteuliwa kusimamia Maliasili, Utalii, Utamaduni na Michezo.
“Tofauti na mabaraza yaliyopita, safari hii tumeamua kuwashirikisha pia wabunge waliopo Bungeni sambamba na wanachama walioko nje ya Bunge ili kupanua wigo wa usimamizi wa Serikali na kuongeza ubora wa utendaji wa baraza,” amesema Semu.
Wapewa jukumu hili
Katika maelekezo yake kwa baraza hilo, Semu amewataka wateule hao kuelekeza nguvu kubwa katika kufuatilia uwajibikaji wa Serikali, matumizi ya fedha za umma na vitendo vya ubadhirifu ndani ya taasisi za umma.
Kiongozi wa Chama cha ACT Wazalendo, Doroth Semu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar ea Salaam leo Jumatatu Mei 18, 2026, wakati akitangaza baraza kivuli la mawaziri la chama hicho watakaofanya kazi kwa muda wa miaka mitano. Picha na Said Powa
Amesema kupitia uchambuzi wa chama hicho wa ripoti za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), zilizotolewa hivi karibuni, zimeibua changamoto za matumizi mabaya ya rasilimali za umma na fedha, akiwataka mawaziri kivuli kusimama imara kuhakikisha uwajibikaji serikalini.
“Ripoti ya CAG imesema zaidi ya Sh7 trilioni zimepotea au kutumika bila maelezo ya kuridhisha huku kukiwa hakuna hatua madhubuti za uwajibikaji zilizochukuliwa mpaka sasa, msilale katika kuisimamia na kubana Serikali ili kulifikia Taifa la wote kwa maslahi ya wote,” amesema.
Mbali na hoja ya matumizi ya fedha, amesema baraza hilo litakuwa mstari wa mbele kufuatilia masuala ya haki za wananchi, migogoro ya ardhi, matumizi mabaya ya madaraka na mwenendo wa utawala nchini.
Akizungumzia uteuzi huo, Madeleka amesema, ACT Wazalendo imechukua uongozi wa jambo hilo kwa sababu kazi ya bunge ambalo lilitakiwa kuisimamia na kuiwajibisha Serikali limekuwa la kupongeza Serikali, hivyo ACT imechukua jukumu la kuunda baraza hili kivuli kama mbadala wa wananchi kuisimamia Serikali.
“Kwa maana ya nafasi ya waziri ya katiba na sheria, hii ni hatua muhimu kwa kuwa matatizo mengi tunayoyaona nchi hii ni matokeo ya kupuuzwa kwa utawala wa sheria. Nchi inapoongozwa kama ‘gheto’ la washikaji kila mtu anajiamulia cha kufanya. Kwa kuwa na wizara hii tutahakikisha tunaisimamia Serikali kuhakikisha utawala wa Sheria na uwajibikaji unaheshimiwa na kufuatwa kwa mujibu wa Sheria,” amedai.
Kuhusu nguvu ya utendaji
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Dk Onesmo Kyauke, akizungumzia baraza hilo, amesema baraza kivuli la mawaziri linaundwa kwa msingi wa Kisheria, lina nafasi yake bungeni na linaundwa kwa kuzingatia idadi maalumu ya wabunge na mchango wake hutolewa bungeni na kuwekwa kwenye kumbukumbu za Bunge.
“Kutokana na msingi huo, baraza hili halitakuwa na nguvu ya kisheria katika kazi zake, ingawa ni hatua nzuri inaweza kusaidia kuwasemea wananchi japo si kwa nguvu kama ambayo lingeipata kama lingetokana na sheria ya kibunge,” amesema.
