Dar es Salaam. Katika hali ya kukabiliana na changamoto ya uchafuzi wa hali ya hewa jijini Dar es Salaam, wanafunzi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) wamebuni mfumo wa kisasa wa kiteknolojia unaolenga kufuatilia hali ya hewa na kutoa taarifa za uwepo wa gesi hatari na vichafuzi katika mazingira.
Mfumo huo wa kidijitali unaojulikana kama ‘Air Quality Monitoring System’ unaweza kumpa mtu taarifa ya hali ya hewa, aina na kiwango cha gesi kilichopo katika mazingira yanayomzunguka na kumweleza nini anatakiwa kufanya kupitia simu janja.
Akizungumza leo Jumanne, Mei 19, 2026 na Mwananchi, mmoja wa wanafunzi waliobuni mfumo huo, Samia Hamadi, mwanafunzi wa mwaka wa tatu wa kozi ya Usimamizi wa Mifumo ya Taarifa, amesema kuwa mfumo huo utakuwa katika mfumo wa programu ya simu (App), ambapo mtumiaji ataweza kuona hali ya usalama wa hewa katika eneo alilopo.
Samia amesema hii inawezekana baada ya eneo husika kufungwa kifaa maalumu kwa ajili ya uchambuzi wa hewa kinachojulikana kama ‘Sensor Node’, kisha watu wa eneo hilo wanaweza kupata taarifa kupitia simu zao.
Samia Hamadi Mwanafunzi wa mwaka wa tatu Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU) aliyehusika kubuni mfumo wa kidigitali kubaini hewa hatarishi katika mazingira ‘Air Quality Monitoring Sysytem’.
“Mfumo wetu utamsaidia hata yule mtumiaji asiye na ujuzi wa mambo ya hewa. Ataweza kuona moja kwa moja ikiwa hali ya hewa ni nzuri, ya wastani, au mbaya,” ameeleza Samia wakati wa maonyesho ya ubunifu huo.
Amesema mbali na kutoa taarifa za sasa, mfumo huo una uwezo wa kipekee wa kutoa utabiri wa hali ya hewa kwa saa moja ijayo au hata siku mbili zijazo.
Pia, amesema mfumo unatoa mapendekezo kulingana na hali ya hewa iliyopo na makundi ya watu, ukizingatia zaidi watoto, wanawake wajawazito, na watu wenye mahitaji maalum au maradhi.
“Kwa mfano, ikiwa hali ya hewa ni mbaya, mfumo utatoa tahadhari watoto wasicheze nje au wasiwepo karibu na maeneo hayo,” amesema.
Ameeleza kuwa kwa wadau wa mazingira na watafiti, mfumo huu unaruhusu kupata na kupakua data za uchafuzi wa hewa katika mifumo mbalimbali kama CSV na PDF kwa ajili ya uchambuzi wa kina.
“Hadi sasa, majaribio ya mfumo huo yanafanyika chuoni lakini mpango wa baadaye ni kuweka vifaa vya kukusanyia taarifa za hewa katika maeneo yenye mrundikano mkubwa wa watu kama Mbezi, Ubungo, na Mwenge. Hii itawawezesha wakazi wa maeneo hayo kufuatilia usalama wa hewa wanayovuta kupitia simu zao,” amesema.
Pamoja na uzuri wa mfumo huu, Samia amebainisha changamoto zinazokwamisha kasi ya usambazaji wake, ikiwamo uhaba wa vifaa vya kutosha kuweka katika maeneo mengi zaidi na changamoto ya upatikanaji wa mtandao wa intaneti ili vifaa viweze kutuma data kwenye mfumo kwa wakati.
“Tukipata watu wa kutusaidia kupata vifaa vingi zaidi, tutaweza kuvifunga katika sehemu nyingi zaidi,” amehitimisha Samia.
Ubunifu huu unatajwa kuwa mkombozi kwa afya za wakazi wa Dar es Salaam, ukiwapa uwezo wa kuchukua tahadhari kabla ya kukumbwa na athari za uchafuzi wa hali ya hewa katika makazi yao.
Wakati wa ufunguzi wa maonesho hayo, Naibu Katibu Mtendaji wa Tume ya Taifa ya Mipango, Dk Blandina Kilama, alisema tafiti na bunifu zinazofanywa na wasomi nchini zinapaswa kutoa suluhisho halisi kwa changamoto za jamii badala ya kuishia kwenye makaratasi, akisisitiza umuhimu wa maarifa, teknolojia na ubunifu katika kujenga na kuchochea maendeleo ya uchumi.
Amesisitiza kuwa Tume ya Taifa ya Mipango iko tayari kupokea mawazo na tafiti zote zinazoweza kusaidia ujenzi wa miji himilivu na miundombinu salama dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.
