
Dar es Salaam. Wakati hatifungani ya EFTA ikiorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), asilimia 99.4 ya wawekezaji walioshiriki ni Watanzania, jambo linaloonyesha kuongezeka kwa imani ya wananchi katika masoko ya mitaji na mifumo rasmi ya uwekezaji nchini.
Hatifungani hiyo iliyolenga kukusanya Sh15 bilioni, imefanikiwa kuvutia zaidi ya Sh33 bilioni, hatua inayotajwa kuwa ishara ya kukua kwa ushiriki wa wananchi katika uwekezaji wa bidhaa za kifedha.
Akizungumza leo Mei 20, 2026 wakati wa hafla ya kuorodheshwa kwa hati hiyo DSE, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA), Nicodemus Mkama amesema mafanikio hayo yanaonyesha Watanzania sasa wanaona masoko ya mitaji kama sehemu salama ya kukuza fedha zao na kushiriki katika maendeleo ya uchumi.
Amesema kwa mara ya kwanza kampuni inayojihusisha na ukodishaji wa vifaa vya uzalishaji imeingia sokoni kuuza hatifungani na kupata mwitikio mkubwa kiasi hicho, huku karibu wawekezaji wote wakiwa Watanzania.
Amefafanua kuwa asilimia 95.4 ya waliowekeza ni wananchi mmoja mmoja, huku taasisi na kampuni zikichangia asilimia 4.5 pekee, hali inayoonyesha kuongezeka kwa mwamko wa wananchi kushiriki katika uwekezaji rasmi.
Hati fungani hiyo ya miaka mitano inatoa faida ya asilimia 14 kwa mwaka, huku kiwango cha chini cha uwekezaji kikiwa Sh500,000.
Mkurugenzi Mtendaji wa DSE, Peter Nalitolela amesema mafanikio hayo yanaonyesha Watanzania wanaanza kuwa chanzo kikuu cha mtaji wa maendeleo kupitia masoko ya ndani badala ya kutegemea fedha kutoka nje.
Amesema katika miaka mitano iliyopita, Tanzania imeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa masoko ya mitaji kupitia bidhaa mpya za uwekezaji na mifumo bunifu ya ukusanyaji mitaji.
Fedha zitakazopatikana kupitia hatifungani hiyo zinatarajiwa kutumika kuongeza mikopo ya vifaa vya uzalishaji kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati, ikiwemo matrekta, mashine za kilimo, vifaa vya uchimbaji madini, magari ya mizigo, mitambo ya viwandani na vifaa vya afya.
Pia inaendana na ajenda ya Taifa ya kukuza uchumi wa viwanda, kuongeza ujumuishaji wa kifedha na kuboresha kilimo cha kisasa kinachotumia teknolojia na mitambo.
Mkurugenzi wa EFTA, Nicomed Bohay amesema kampuni imeamua kutumia soko la ndani kupata mtaji wa muda mrefu badala ya kutegemea mikopo ya fedha za kigeni.
Amesema tayari kampuni imepokea na kuidhinisha maombi ya mikopo kwa zaidi ya matrekta 1,500 pamoja na vifaa vingine vya uzalishaji, huku maombi mapya yakiendelea kuwasilishwa kila siku.
