Dodoma/Dar. Wizara ya Ujenzi imeomba Bunge kuipitishia takribani ya Sh2.6 trilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na maendeleo kwa mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa na mkakati maalumu wa kuboresha miundombinu ya barabara kuu kwa hatifungani.
Katika bajeti hiyo yenye ongezeko kidogo ukilinganisha na ya mwaka 2025/26 iliyokuwa ni Sh2.28 trilioni, Waziri Ulega amesema Sh2.3 bilioni zimetengwa kwa ajili ya shughuli za maendeleo ambapo kati ya fedha hizo, Sh1.5 bilioni ni fedha za ndani wakati Sh922 bilioni ni fedha za nje.
Kwenye mipango yake ya maendeleo imetangaza kuanzisha mfumo wa hati fungani katika ujenzi wa barabara ili kupata fedha za kugharamia matengenezo makubwa na ukarabati kwa baadhi ya barabara.
Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega akiwasilisha bajeti ya mwaka 2026/27 leo Jumatano, Mei 20, 2026 bungeni jijini Dodoma.
Miongoni mwa barabara zitakazojengwa kwa mfumo huo ni zile kuu za kiuchumi ikiwemo ya Morogoro hadi Mwanza kupitia mikoa ya Dodoma, Singida na Shinyanga na nyingine kutoka Tinde hadi Rusumo, mpakani na Rwanda.
Hayo yameelezwa leo Jumatano Mei 20, 2026 na Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega wakati akiwasilisha hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya wizara yake kwa mwaka 2026/27.
Amesema mpango huo unakwenda sambamba na ujenzi wa barabara za Kibiti – Lindi – Mingoyo na ile ya Sirari hadi Mutukula kupitia Musoma, Mwanza, Geita na Bukoba.
Pia zitajengwa barabara kutoka Dar es Salaam kupitia mikoa ya Morogoro, Iringa, Makambako, Mbeya hadi Tunduma ikiongezwa kutoka njia mbili kwenda nne.
Hata hivyo, Waziri Ulega amesema mpango huo unatokana na uwekezaji mkubwa katika bandari, hususan Bandari ya Dar es Salaam ambao umesababisha ongezeko la mizigo inayosafirishwa ndani na nje ya nchi kupitia barabara.
“Ufanisi huu wa bandari unakumbana na changamoto kadhaa zikiwemo msongamano pamoja na uchakavu wa miundombinu ya barabara unaohitaji fedha nyingi kuziboresha,” amesema.
Mgawanyo kwa taasisi
Waziri Ulega ameeleza namna fedha hizo zitakavyotumika kwa kila taasisi ambapo Wizara ya Ujenzi imetengewa Sh102. 9 bilioni, Wakala wa Barabara (Tanroads) Sh926.9 bilioni, Tamisemi Sh31 bilioni, Tarura Sh279 bilioni na Bodi ya Mfuko wa Barabara Sh22.8 bilioni.
“Bodi ya mfuko wa barabara itaendelea kufanya tafiti za vyanzo vipya vya mapato ili kuongeza uwezo wa mfuko kugharamia matengenezo ya barabara, kufanya ukaguzi wa ubora wa miundombinu hiyo katika mikoa yote nchini ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inakidhi thamani ya fedha zilizotumika,” amesema Ulega.
Usafiri wa majini
Waziri Ulega amesema katika kuendeleza jitihada za kuimarisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji majini na kuchochea uchumi wa buluu, Serikali imedhamiria kukamilisha ununuzi wa vivuko vipya vitano Kanda ya Ziwa pamoja na uboreshaji wa usafiri katika ukanda wa Pwani.
Amesema kukamilika kwa kivuko kipya cha Nyamisati – Mafia kutahakikisha uwepo wa kivuko cha pili cha uhakika kwa safari za kila siku, huku kivuko kitakachohudumia Boza, Kuruti, Shungumbweni (Ngwevu) na Kisiju kikilenga kutoa huduma rahisi na salama kwa wananchi.
Kwa upande wa majengo, waziri amesema kupitia Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), wataendelea na usimamizi wa miliki ya Serikali ili kutoa makazi bora kwa ajili ya viongozi na watumishi wa umma.
Amesema wizara imejipanga kukamilisha mradi wa ujenzi wa nyumba za gharama nafuu 144 unaoendelea katika eneo la Temeke jijini Dar es Salaam na kuanza utekelezaji wa mradi wa nyumba 144 za gharama nafuu jijini Dodoma.
Waziri anasema ili kuuwezesha Wakala wa Majengo Tanzania kujitegemea na kupunguza utegemezi wake kwa ruzuku ya Serikali, wataendelea kukaribisha sekta binafsi kufanya ubia na Serikali kupitia TBA ili kuwekeza katika miradi ya ujenzi na uendeshaji wa nyumba na majengo.
Akiwasilisha maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Selemani Kakoso ameitaka Serikali kusimamia kikamilifu miradi inayotekelezwa ili iweze kukamilika kwa wakati na kwa kuzingatia ubora na thamani ya fedha.
Kakoso pia ameitaka wizara ya ujenzi kubuni vyanzo vya mapato na kuweka mikakati itakayoongeza ufanisi katika ukusanyaji wake ili kuzifanya taasisi zake kupunguza utegemezi wa ruzuku kutoka mfuko mkuu wa Serikali.
“Serikali ihakikishe inahamisha fedha zote kwenda kwenye akaunti ya Mfuko wa Barabara kama zilivyoidhinishwa na Bunge ili kutekeleza miradi ya matengenezo na ukarabati wa barabara na madaraja nchini na isitishe mara moja mpango wake wa kupunguza asilimia 5 ya fedha za mfuko wa barabara kwa ajili ya kuzihamishia katika shughuli zingine,” amesema Kakoso.
Amesema kuzihamisha fedha hizo kunaweza kuzorotesha maendeleo ya sekta ya barabara nchini na mpango huo ukitekelezwa utakuwa unavunja sheria kwani fedha hizo zinalindwa kwa mujibu wa sheria.
Kamati imeshauri pia Serikali kufanya tathmini ya kina kuhusu kuweka tozo maalumu ya maendeleo ya miundombinu ya barabara katika mapato ghafi ya madini, vibali vya ujenzi, muda wa maongezi kwenye sekta ya mawasiliano pamoja na kulipia daraja la Tanzanite kwa watumiaji wake.
Amesisitiza mpango wa ukamilishaji wa miradi viporo ya ujenzi wa barabara na madaraja nchini ili kuchochea uchumi na kupata tija iliyokusudiwa, ambayo inapaswa kwenda sambamba na malipo ya makandarasi na wahandisi.
Baadaye, Kakoso ambaye ni mbunge wa Mpanda Vijijini alipata fursa ya kuchangia bajeti hiyo akisema ili kumwezesha Waziri Ulega kutekeleza majukumu yake ni lazima wizara ipate fedha huku akiwashauri wabunge kubuni chanzo cha fedha bila kujali wananchi nje ya Bunge watasema nini.
Kakoso alisema bila kuangalia chanzo kingine, suala la miundombinu ya barabara litaendelea kuwapo kwa sababu ya uhitaji wa fedha, hivyo wabunge wasisite kufanya uamuzi huo mgumu wa kuanzisha chanzo kingine.
Naper na shilingi
Katika mchango wake, Mbunge wa Mtama (CCM), Nape Nnauye ametishia kushika shilingi akipinga kupitishwa bajeti hiyo kwa madai haijatenga fedha kwa ajili ya ujenzi wa Barabara ya Dar es Salaam-Kibiti-Lindi hadi Mtwara.
Nape amesema barabara hiyo ni kiungo cha mikoa kadhaa ya kusini na iliahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwamba itajengwa lakini anashangaa haijatengewa fedha kwenye bajeti hiyo.
Amesema wananchi wa jimbo lake wamemtuma asipoona fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo, aipinge.
Nape, amesema ameangalia randama na kuipitia mara nne, hakuona fedha zilizotengwa kwa ajili ya ujenzi wa barabara hiyo ambayo tayari muda wa matumizi yake umekwisha.
“Wamezibaziba mpaka haiwezekani kuzibaziba tena. Barabara hii haikutengewa fedha, mimi nikiunga mkono bajeti hii nitawasaliti wananchi wa kusini, nitakuwa nasaliti ilani ya uchaguzi ya chama changu (CCM).”
“Kwa hiyo natangaza wazi kabisa, siungi mkono bajeti hii mpaka fedha zitengwe kwenye hii barabara,” amesema.
Mbunge wa Korogwe Vijijini (CCM), Timotheo Mzava yeye ametaka kuongezwa kasi ya utekelezaji wa ujenzi wa mradi wa Barabara ya Korogwe-Dindira-Bumbuli hadi Soni yenye urefu wa kilomita 74 iliyoahidiwa kwenye ilani mara nne.
Pia, amesema baadhi ya maeneo katika barabara hiyo hayapitiki nyakati za mvua, akisisitiza wakati inasubiriwa lami, zitolewe fedha kwa ajili ya ukarabati ili iendelee kupitika.
Aidha, amezungumzia barabara ya kutoka Tanga kwenda Segera na Serega kwenda Chalinze, akisema mbali na wembamba wake, pia muda wa matumizi yake umekwisha lakini haijaonekana kwenye mpango wa bajeti hiyo.
“Kwenye hili, watu wa Tanga, Morogoro, Chemba na Singida, tuungane kwa ajili ya barabara hii ya kilomita 324, tusikubali kupitisha bajeti hii kama hatujapata mkakati madhubuti wa Serikali kutengeneza barabara hii kwa kiwango cha lami,” amesema.
