Polisi yatanda ofisi za Chadema, kigogo wake akihojiwa, msaidizi wa Lissu…Polisi yatanda ofisi za Chadema, kigogo wake akihojiwa, msaidizi wa Lissu…

Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Bara, Amani Golugwa amesema msaidizi wa Tundu Lissu, David Jumbe, ‘ametekwa’ na watu wasiojulikana usiku wa kuamkia leo Alhamisi, Mei 21, 2026 nyumbani kwake Mabwepande, Bunju jijini Dar es Salaam huku yeye mwenyewe akihojiwa na Jeshi la Polisi.

Akizungumza na Mwananchi leo Mei 21, 2026 kabla ya Jeshi la Polisi kuzingira ofisi za Chadema Mikocheni jijini Dar es Salaam kufanya mahojiano na Golugwa, amesema taarifa zinazosambaa mitandaoni ni za kweli.

“Hizi ni taarifa za kweli na tutaongea na waandishi wa habari muda si mrefu,” amesema Golugwa.

Mwananchi limefika Chadema asubuhi ya leo ambapo kumeitishwa mkutano na waandishi wa habari uliopangwa kufanyika saa 3:00 asubuhi kuzungumzia tukio la ‘kutekwa’ kwa David, lakini mkutano huo umechelewa kuanza.

Mkutano huo umeshindikana kuanza kwa wakati kutokana na kile kilichoelezwa na Mkuu wa Idara ya Habari wa Kurugenzi ya Habari na Uenezi ya Chadema, Gervas Lyenda  kuwa Golugwa anahojiwa.

Lyenda amesema wamechelewa kuanza mkutano na waandishi wa habari kutokana na kiongozi wao huyo kuzuiliwa na Jeshi la Polisi, ambalo linaendelea kufanya mahojiano naye ndani ya ofisi za Chadema Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Mwananchi imeshuhudia magari manne ya askari wa Jeshi la Polisi yakiwa pembezoni mwa ofisi za Chadema huku baadhi wakifanya doria wakiwa na silaha za moto.

Kwa mujibu wa taarifa zilizosambaa mtandaoni kuanzia usiku wa kuamkia leo Mei 21, 2026, David anadaiwa kuchukuliwa nyumbani kwake Mabwepande, Bunju jijini Dar es Salaam.

Taarifa hiyo inayodaiwa kuwa ni maelezo ya mke wa Jumbe inasema:

“Jumbe alikuwa anarudi nyumbani na alipofika getini alifuatwa na watu hao, wakamkamata na kumwingiza kwenye gari aina ya Land Cruiser kisha kuondoka kwa mwendo mkali.

Msaidizi wa Tundu Lissu, David Jumbe

“Jumbe alipiga kelele na kujaribu kujitetea lakini watu hao wakamzidi nguvu. Majirani walipofika walijaribu kuikimbiza gari hiyo bila mafanikio,” imeeleza taarifa hiyo.

Katika purukushani hizo, Jumbe anadaiwa kudondosha kiatu alichokuwa amevaa kabla ya kuchukuliwa na watu hao ambao hawakujitambulisha kwa familia.

Mwananchi inaendelea kumsaka Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro, kwa ufafanuzi kuhusu tukio la kuhojiwa kwa Golugwa na madai ya kutoweka kwa David Jumbe.

Endelea kufuatilia Mwananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *