
MWENYEKITI wa mashindano ya Yamle Yamle Cup, Sadiq Ali (Flash) amesema mshindi wa kwanza wa mashindano hayo yatakayoanza Juni 2026, ataondoka na zawadi ya Sh20 milioni, kombe na medali za dhahabu.
Mwenyekiti huyo, amesema mwitikio wa wananchi na vijana kushiriki mashindano hayo umekuwa mkubwa kutokana na ongezeko la maombi ya fomu za usajili kutoka maeneo mbalimbali ya Zanzibar.
Amesema mshindi wa pili ataondoka na Sh10 milioni na medali za fedha, watatu Sh5 milioni na wanne Sh3 milioni, huku timu zitakazocheza siku ya ufunguzi itakayoshinda itapata Sh5 milioni na itakayoshindwa, Sh3 milioni.
Mbali na hilo, Sadiq amesema timu zote zitakazotinga hatua ya robo fainali zitapatiwa Sh1 milioni za kujiandaa.
Zawadi nyingine zitakazotolewa ni kipa bora, mfungaji bora na mchezaji mdogo na kila mmoja atapata pikipiki huku mchezaji bora wa nusu fainali atapata Sh1 milioni.
Pia mwamuzi bora, kocha bora, kikundi cha ushagiliaji bora, wote watapata Sh1 milioni na timu yenye nidhamu itapata Sh2 milioni.
“Baadhi ya fomu za maombi tayari zimekwisha kutokana na idadi kubwa ya waombaji,” amesema.
