MSHAMBULIAJI wa Dodoma Jiji, Edgar William ameandika rekodi mpya katika kikosi cha ‘Walima Zabibu’, baada ya kufikisha mabao saba ya Ligi Kuu Bara na kuivuka ya msimu uliopita wa 2024-2025, wakati akiwa Fountain Gate.
Nyota huyo amefunga bao moja jana katika sare ya 1-1 dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma na kufikisha mabao saba, akiivuka ya msimu wa 2024-2025, alipofunga sita.
Katika mechi hiyo kali na ya kusisimua ya raundi ya 24, wenyeji Dodoma Jiji ilipata bao hilo la Edgar William dakika ya 11, akiwazidi ujanja mabeki wa Mashujaa, kisha maafande hao kuchomoa dakika ya 85, kupitia kwa Balama Mapinduzi ‘Kipenseli’.
Kabla ya kutua Dodoma Jiji, msimu wa 2024-2025, Edgar aliifungia Fountain mabao sita ya Ligi Kuu na kuasisti pia mawili, huku akikumbukwa msimu wa 2023-2024, alipokuwa mfungaji bora wa Championship akiwa na KenGold baada ya kufunga mabao 21 na kutwaa Tuzo ya Mchezaji Bora, akiwashinda Casto Mhagama aliyecheza naye KenGold na Mganda Boban Zirintusa, aliyekuwa Biashara United ya Mara.
Nyota huyo anashikilia rekodi nzuri Championship kwani amepandisha pia timu mbili Ligi Kuu Bara, akianza na Mbeya Kwanza msimu wa 2021-2022, kisha KenGold msimu wa 2023-2024.
Edgar amesema ni jambo nzuri kwake kuona amekuwa na mwenendo mzuri wa kiwango chake, ingawa anapaswa kuendelea kupambana zaidi ili kutimiza malengo ya kikosi hicho na yake binafsi.
“Mchezaji mzuri ni yule anayefanyia tathimini ya kiwango chake mwenyewe msimu baada ya msimu, nimefurahia kuvunja rekodi yangu na kuweka mpya, kwangu ni mafanikio lakini nataka kuendelea kupambana zaidi ya hapa nilipo sasa,” amesema Edgar.
