Hospitali ya Benjamin Mkapa yasaka Sh7 bilioni kusaidia upandikizaji figo, urotoHospitali ya Benjamin Mkapa yasaka Sh7 bilioni kusaidia upandikizaji figo, uroto

Dar es Salaam. Hospitali ya Benjamin Mkapa (BMH) imezindua kampeni ya kuchangisha Sh7 bilioni ili kufadhili upandikizaji wa figo na uroto kwa wagonjwa 100 wasio na uwezo katika kipindi cha miaka miwili ijayo.

Mpango huo unalenga kuwasaidia wagonjwa 50 wanaohitaji upandikizaji wa uroto, hasa watoto wanaougua ugonjwa wa selimundu na wengine 50 ambao fizo zao zimeshindwa kufanya kazi kwa muda mrefu.

Akizungumza na wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuelekea maadhimisho ya miaka 10 ya hospitali hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa BMH, Dk Abel Makubi amesema Serikali tayari imetoa fedha za awali, lakini ongezeko la mahitaji ya huduma za kibingwa kama hizo linahitaji ushirikishwaji mpana wa wadau.

“Tunalenga kukusanya Sh7 bilioni ndani ya miaka miwili ili kuwasaidia wagonjwa waliopo kwenye orodha ya kusubiri,” amesema Dk Makubi.

“Tayari tuna wagonjwa 50 walio tayari kwa upandikizaji wa uroto na wengine 50 wanaosubiri upandikizaji wa figo. Serikali imetusaidia, lakini mahitaji yameongezeka kwa kiasi kikubwa,” ameongeza.

Amesema upatikanaji wa huduma za upandikizaji viungo nchini umepunguza gharama za matibabu na kuokoa fedha za kigeni zilizokuwa zikitumika kwa rufaa za matibabu nje ya nchi.

Wahariri wakifuatilia mkutano wa Hospitali ya Benjamin Mkapa uliolenga kutangaza mafanikio ndani ya miaka 10 tangu kuanzishwa kwake pamoja malengo ya baada ye kuongeza huduma za kibingwa na utalii wa tiba. Picha na Mapigapicha Wetu

Amedokeza kuwa upandikizaji wa figo katika BMH hugharimu kati ya Sh40 milioni hadi Sh45 milioni, ikilinganishwa na takribani Sh60 milioni nje ya nchi.

Kwa upandikizaji wa uroto, alisema wagonjwa hutumia kati ya Sh50 milioni na Sh55 milioni hapa nchini, wakati matibabu sawa nje ya nchi hugharimu zaidi ya Sh275 milioni.

“Taratibu hizi zinahitaji uwekezaji mkubwa, lakini kuzitoa hapa nchini kumeiwezesha nchi kuokoa fedha nyingi,” amesema Dk Makubi.

“Hata hivyo, gharama hizi zilizopunguzwa bado ni kubwa kwa familia nyingi, ndiyo maana tunaomba wadau na watu wenye mapenzi mema waunge mkono mpango huu,” ameongeza.

Hospitali hiyo imeongeza idadi ya watumishi kutoka 20 hadi 1,073, wakiwemo madaktari bingwa 100 na madaktari bingwa bobezi 30 na matokeo yake ya tiba yamefikia viwango vya kimataifa.

“Matokeo yetu yanalingana na yale yanayopatikana India, Ulaya na Marekani,” alisema.

Serikali imewekeza zaidi ya Sh283 bilioni katika miundombinu na vifaa tiba vya kisasa, huku ikitarajiwa kuadhimisha miaka 10 ya uanzishwaji wake Julai 15 mwaka huu.

Mtaalamu wa upandikizaji figo, Profesa Masumbuko Mwashambwa, amesema BMH ilianza kutoa huduma za upandikizaji mwaka 2018 kupitia ushirikiano na Tokushukai Medical Corporation ya Japan, kutokana na urafiki wa muda mrefu kati ya hayati Rais wa zamani Benjamin Mkapa na Dk Torao Tokuda wa Japan.

Alisema hadi sasa BMH imefanya upandikizaji wa figo kwa wagonjwa 56, ingawa ugonjwa wa figo bado ni changamoto kubwa ya afya ya umma inayoendelea kukua.

“Utafiti unaonyesha kuwa takribani asilimia 10 ya watu duniani wanaugua magonjwa yanayohusiana na figo na kila baada ya sekunde 20 mtu mmoja hufariki kutokana na matatizo ya figo,” amesema.

Shinikizo la damu na kisukari, alisema ni miongoni mwa visababishi vikuu vya ugonjwa wa figo, ambapo takribani theluthi moja ya wagonjwa wa kisukari hupata matatizo ya figo.

Profesa Mwashambwa alibainisha kuwa ingawa gharama za upandikizaji wa ndani ni nafuu kuliko matibabu ya nje ya nchi, bado familia nyingi zinashindwa kumudu Sh45 milioni pamoja na gharama za dawa za gharama kubwa baada ya upasuaji.

Mtaalamu wa upandikizaji uroto, Dk Stella Malangaya alisema BMH inaendelea kujitokeza kama kituo cha ubora wa huduma za upandikizaji huo katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Amesema hospitali hiyo imeanza kuvutia wagonjwa kutoka nchi jirani, jambo linaloongeza ujuzi na pia kukuza utalii wa tiba.

Hata hivyo, kama ilivyo kwa figo, amesema uwezo wa kumudu gharama bado ni changamoto kubwa kwa Watanzania wa kawaida.

“Kwa sasa, watoto 50 wapo kwenye orodha ya kusubiri, wengi wao wakisumbuliwa na ugonjwa wa selimundu,” amesema Dk Malangaya.

Aliongeza kuwa kampeni ya uchangiaji pia itasaidia kupanua miundombinu ya tiba kutoka watu watatu wanaotibiwa kwa wakati mmoja hadi sita na kuwezesha ununuzi wa vifaa maalumu.

Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Deodatus Balile amesema Tanzania inapiga hatua kubwa katika tiba za kibingwa, akipongeza mafanikio ya upasuaji wa hivi karibuni na kueleza kuwa matokeo yamezidi simulizi hasi zinazosambazwa mitandaoni.

Alitoa wito kwa Watanzania kuunga mkono kampeni hiyo ya Sh7 bilioni kupitia nguvu ya vyombo vya habari ili kuhakikisha mustakabali bora wa baadaye.

Naibu Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo), Rodney Mbuya amesema chapa ya BMH imejijengea imani kwa umma na amewataka wanahabari kuwaelimisha wananchi na kutangaza huduma za Serikali.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *