Waziri Mkuu atoa maagizo maadhimisho ya Ziwa VictoriaWaziri Mkuu atoa maagizo maadhimisho ya Ziwa Victoria

Mwanza. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba ametoa maelekezo kwa nchi zinazozungukwa na Ziwa Victoria ikiwemo kuhakikisha vituo vya uokozi vilivyopo Tanzania, Kenya na Uganda vinaanza kufanya kazi kwa haraka, ubora na ufanisi.

Akizungumza leo Alhamisi Mei 21, 2026 kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya Ziwa Victoria iliyoandaliwa na nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kwa uratibu wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria (LVBC), Dk Mwigulu amesema ajali za majini hazitoi taarifa.

Huku akitoa pole kwa waathirika wa ajali ya meli ya Mv Bukoba iliyotokea Mei 21, 1996 mkoani Mwanza, Dk Mwigulu amesema vituo hivyo kikiwemo kikuu cha kikanda cha kuratibu uokoaji katika Ziwa Victoria kilichopo Mwanza, Tanzania, vianze kufanya kazi haraka baada ya ujenzi wake kukamilika.

“Siku kama ya leo mwaka 1996 ilitokea ajali kubwa ya meli ya Mv Bukoba ndani ya Ziwa Victoria, hivyo pia siku ya leo imebeba kumbukumbu nzito na historia kubwa nzito kwa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema.

Vituo vingine vidogo vya uokoaji vipo Kisumu, Kenya na Entebbe, Uganda ambavyo vitasaidia katika uokozi pale kutakapotokea ajali ndani ya ziwa hilo.

“Masuala ya majini hayatoi taarifa yakitokea ndiyo yametokea…kwa hiyo ni vyema pakawa na ufanisi wa juu katika kutekeleza uratibu wake ili kuokoa maisha ya watumiaji wa vyombo vinavyopita majini, usafirishaji pamoja na shughuli nyingine za kiuchumi,” amesema.

Dk Mwigulu amezitaka nchi hizo kuhakikisha zinatoa kipaumbele kwenye suala ya utunzaji mazingira pamoja na kuratibu na kusimamia upandaji miti.

Waziri Mkuu wa Tanzania, Dk Mwigulu Nchemba (kulia) akimkabidhi cheti cha pongezi, Katibu Mkuu Wizara ya Maji na Mazingira nchini Uganda, Dk Alfred Okot Okidi (kushoto).

“Sote tunawajibika kuweka kipaumbele kutunza mazingira, kuratibu na kusimamia shughuli endelevu la kupanda miti rafiki kwa maji katika mwambao wa Ziwa Victoria kwa nchi zote wanachama wa Afrika Mashariki na wanaozungukwa na bonde la ziwa hilo,” amesema.

Ametaka mikakati endelevu iwepo ya kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira ya Ziwa Victoria kwa wananchi hususani watoto na vijana.

“Kwa kupitia shule za msingi na sekondari anzisheni klabu zinazojihusisha na masuala ya uhifadhi wa mazingira ya Ziwa Victoria ili kuweza kuwa utamaduni endelevu wa kupanda miti na kutunza mazingira,” ameongeza Dk Mwigulu.

Katibu Mtendaji wa LVBC, Dk Masinde Bwire amesema siku ya Ziwa Victoria inaonesha kutambuliwa kwa umuhimu wa ziwa hilo.

“Hatua hii muhimu inaonesha kutambuliwa kwa umuhimu wa kimkakati wa ziwa Victoria kwa watu na uchumi wa Jumuiya ya Afrika Mashariki,” amesema.

Ameeleza kuwa, maadhimisho hayo yanaendana na siku ya kumbukumbu ya ajali mbaya ya meli ya Mv Bukoba.

Baadhi ya viongozi na wananchi waliohudhuria kilele cha siku ya maadhimisho ya Ziwa Victoria.

“Tulipoteza maisha zaidi ya watu 800, maadhimisho ya leo siyo tu tukio la kawaida na sherehe pekee. Ni wito wa kutafakari, kuchukua hatua na kujenga tabia ya kulinda moja wapo ya thamani kubwa za asili barani Afrika,” amesema Dk Bwire

Amesema maadhimisho hayo pia ni wito wa kutafakari na kulinda ziwa hilo kwani si chanzo tu cha maji bali ni uhai kwa watu wa Afrika Mashariki na kutegemewa na watu zaidi ya milioni 55 moja kwa moja na watu milioni 400 kwa njia isiyo moja kwa moja ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, barani Afrika na duniani.

Amesema sehemu mbalimbali ya Ziwa Victoria zinakaribiwa na upungufu wa ubora wa maji kutokana na shughuli za kibinadamu.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, James Millya amesema nchi hizo kwa pamoja wamefanikisha maandalizi ya programu shirikishi ya usimamizi wa rasilimali za maji katika Bonde la Ziwa Victoria.

Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, (LVBC), Dk Masinde Bwire akizungumza kwenye maadhimisho ya siku ya Ziwa Victoria yaliyofanyika kikanda mkoani Mwanza.

“Kupitia Programu hii, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imepata fedha za msaada kutoka Serikali ya Shirikisho la Ujerumani na Umoja wa Ulaya jumla ya Euro milioni 16.38 kwa ajili ya upanuzi wa mtandao wa majitaka wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa),

“Hususani kuunganisha kaya 1,800 na taasisi mbalimbali kwenye mfumo wa kisasa wa majitaka; ujenzi wa kilomita 14.4 za mabomba ya majitaka pamoja na ukarabati na ufungaji wa pampu mpya kwenye vituo vitatu vya kusukuma majitaka vilivyopo jijini Mwanza,”amesema.

Katibu Mkuu Wizara ya Maji nchini Uganda, Dk Alfred Okot Okidi amesema wamejizatiti kuendeleza usimamizi wa jumla wa ulinzi wa Ziwa Victoria kupitia programu za uhifadhi wa mazingira zinazotekelezwa nchini Uganda.

Naye, Waziri wa Maji nchini Tanzania, Jumaa Aweso amezishukuru nchi wanachama kwa kuridhia maadhimisho hayo ya kwanza kufanyikia Tanzania.

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (kushoto)  akipokea cheti cha pongezi kutoka kwa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba (kulia) wakati wa kilele cha maadhimisho ya Siku ya Ziwa Victoria iliyofanyika kwa siku nne jijini Mwanza.

Amesema Tanzania itakuwa mstari wa mbele kuhakikisha Ziwa Victoria linalindwa na kutunzwa kwa ajili ya vizazi vijavyo na linaendeleza maendeleo ya kiuchumi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *