
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, leo Mei 21,2026 imemteua mchezaji wa zamani wa Manchester United, Rio Ferdinand, kuwa Balozi wa Hiari wa Utalii wa Tanzania katika hatua inayolenga kuitangaza nchi kimataifa kupitia watu wenye ushawishi mkubwa duniani.
Katika hafla ya uteuzi huo, Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashatu Kijaji, amesema serikali inaendelea kutumia njia mbalimbali kuitangaza Tanzania na vivutio vyake vya kipekee duniani kote.
Dk Kijaji amesema sekta ya utalii imeendelea kukua kwa kasi kubwa katika miaka ya hivi karibuni, ambapo mapato yatokanayo na utalii yameongezeka kutoka Dola 1.32 bilioni (Sh3.4 trilioni) hadi kufikia zaidi ya Dola 4.4 bilioni (Sh11.5 trilioni).
Amesema mafanikio hayo yanaendelea kuchangia maendeleo ya taifa pamoja na utoaji wa huduma kwa wananchi.
“Fedha hizi zinaingia serikalini na kusaidia kuwahudumia Watanzania. Tunajivunia kuona sekta ya utalii ikiendelea kukua na kuitangaza Tanzania duniani,” amesema Dk Kijaji.
Katika ziara yake nchini, Rio Ferdinand amepata fursa ya kutembelea Hifadhi ya Taifa ya Serengeti ambapo alionesha kuvutiwa na uzuri wa mazingira pamoja na wanyamapori waliopo nchini.
Akizungumzia ziara na uteuzi huo, Rio amesema Tanzania umempa uzoefu wa kipekee ambao hajawahi kuupata katika maeneo mengi aliyowahi kutembelea duniani.
“Nimebahatika kutembelea sehemu nyingi duniani kutokana na maisha yangu ya soka na kazi ninazofanya, lakini mapokezi niliyoyapata Tanzania yamekuwa ya kipekee sana. Tangu nilipotua nchini, nimepokelewa kwa upendo mkubwa,” amesema Rio Ferdinand.
Aidha, amewataka watu duniani kutosikiliza maneno au mitazamo hasi kuhusu Afrika bila kufika na kujionea wenyewe hali halisi.
“Mambo mengi huzungumzwa kuhusu Afrika, lakini ningewashauri watu wafike kwanza kabla ya kuamini wanayoambiwa. Ukarimu wa watu wa Tanzania, tamaduni zao na mazingira yake ni vitu vya kipekee sana,” amesema.
Rio amesema uzoefu alioupata Tanzania umeimarisha zaidi imani yake kuwa Afrika ni sehemu nzuri duniani na akaahidi kutumia ushawishi wake kuitangaza Tanzania kwa kiwango kikubwa zaidi.
Kupitia akaunti zake mbalimbali za mitandao ya kijamii zenye zaidi ya wafuasi milioni 25, serikali inaamini Rio Ferdinand atasaidia kuwafikia watu wengi duniani na kuwavutia kuja kutembelea Tanzania.
Kwa upande wake, Rio ameahidi kufanya kazi hiyo kwa moyo wote na kuhakikisha anaiacha Tanzania ikiwa imepiga hatua kubwa zaidi katika utalii wa kimataifa.
“Kila jambo ninalofanya maishani mwangu huwa nalenga kuboresha na kusaidia watu wengine. Ninapokuwa sehemu fulani natamani niache ikiwa bora zaidi kuliko nilivyoikuta. Hata katika jukumu hili haitakuwa tofauti,” amesema Rio Ferdinand.
Uteuzi wa Rio Ferdinand unaonekana kuwa sehemu muhimu ya mkakati wa Tanzania wa kutumia watu maarufu duniani kuitangaza nchi, kuongeza idadi ya watalii na kukuza uchumi kupitia sekta ya utalii.
