Chuo cha Uhamiaji kutumia tafiti kutatua changamoto za uhamiajiChuo cha Uhamiaji kutumia tafiti kutatua changamoto za uhamiaji

Moshi. Katika juhudi za kuboresha na kuimarisha masuala ya usalama na uhamiaji nchini, Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (Trita) kilichopo mkoani Kilimanjaro, kimejipanga kutumia tafiti mbalimbali za kisayansi kutoa suluhisho la changamoto zinazoikabili sekta ya Uhamiaji Afrika Mashariki na Afrika kwa ujumla.

Tafiti hizo ambazo zitachapishwa katika jarida maalumu la kitaaluma la chuo hicho (The Journal of Migration and Securiry Studies) zitasaidia kuboresha utawala, sheria na sera zinazohusu uhamaji na usalama, pamoja na kuisaidia Serikali kufanya uamuzi sahihi wenye tija kwa kuzingatia ushahidi wa kisayansi.

Akizungumza leo Mei 22, 2026, Mkuu wa Utafiti na Ushauri chuoni hapo, Dk Adventina Laurent amesema kutokana na chuo hicho kujikita katika masuala ya uhamaji na usalama, tafiti zitakazochapishwa na jarida hilo zitasaidia kutoa majibu ya changamoto zinazoikumba sekta ya Uhamiaji nchini.

Dk Adventina amesema mapendekezo yatakayotokana na tafiti hizo yataisaidia nchi kupata manufaa makubwa katika kuimarisha usalama na maendeleo ya nchi kwa ujumla.

Mkuu wa Kitengo cha Utafiti na Ushauri wa Chuo cha Kikanda cha Uhamiaji (TRITA) mkoani Kilimanjaro, Dk Adventina Laurent, akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake. Picha na Janeth Joseph.

Aidha, amewataka watafiti wa ndani na nje ya chuo hicho kuwasilisha makala zao kwa ajili ya kuchapishwa, akisisitiza kuwa taarifa zitakazopokewa lazima ziwe za kweli na zenye kuzingatia misingi ya kitaaluma.

“Tunakaribisha watafiti kuleta tafiti zao ili zichapishwe kwenye jarida hili. Tafiti hizo zitasaidia kujenga Taifa lenye usalama na uamuzi sahihi yanayotokana na ushahidi wa kisayansi,” amesema.

Amsema: “Dunia nzima suala la usalama ni muhimu sana. Jarida hili litasaidia Taifa, Afrika na dunia kwa ujumla kwa sababu litakuwa linachapisha tafiti zenye majibu na mapendekezo ya changamoto mbalimbali.”

Naye, Mkuu wa Chuo hicho, Kamishna Msaidizi wa Uhamiaji, Hoja Mahiba amesema tafiti zitakazofanywa na wanataaluma wa ndani na nje ya chuo hicho kuhusu masuala ya uhamaji na usalama zitachapishwa katika jarida hilo la chuo.

Aidha, amesema mpango wa chuo hicho ni kuwa kituo cha umahiri katika masuala ya usalama na uhamaji barani Afrika, hivyo jarida hilo litakuwa na hadhi ya kimataifa kwa kushirikisha watafiti kutoka maeneo mbalimbali barani Afrika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *