
Dar es Salaam. Kutoboa kitovu au ulimi kwa ajili ya urembo ili kuvaa cheni au vito vingine kunazidi kupata umaarufu miongoni mwa vijana, hata hivyo nyuma ya mtindo huo kuna maswali ya kiafya kuhusu maambukizi na usalama.
Urembo huo kwenye kitovu hufanyika kwa kutoboa tundu dogo kwenye ngozi juu au karibu na kitovu kutegemea na matakwa ya mtobolewaji, vivyo hivyo kwenye ulimi ambapo hutobolewa tundu dogo kwenye eneo la ulimi analochagua mhusika.
Baada ya kutoboa, kito, kama vile pete ya tumbo au kingine kinaweza kuvaliwa na mhusika.
Huduma hiyo imekuwa ikitolewa kwenye saluni au spa katika miji mikubwa na majiji, na baadhi ya watoa huduma wameeleza namna zoezi inavyofanyika hadi kukamilika.
Kwa nyakati tofauti wameiambia Mwananchi kwamba, hadi utoboaji kukamilika inaweza kuchukua dakika 20 mpaka 30 huku kupona kukichukua wiki tatu hadi nne kutegemeana na mhusika.
“Wapo ambao huchukua hadi wiki mbili kupona na wengine wanapona ndani ya siku tatu mpaka nne,” amesema mmoja wa watoa huduma hiyo jijini Dar es Salaam, akifafanua kuwa gharama yake huanzia Sh 25,000 kutegemea na saluni.
Mtoa huduma mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Vaileth Ayoub amesema baada ya huduma huwa wanamshauri mteja asiweke maji kwenye kidonda hadi kipone.
“Huwa kuna kipini wanavalishwa, haitakiwi kidonda kinapokuwa kibichi kiingie maji, ndiyo sababu huwa tunashauri kwa wale wanaopenda kuogelea waache kwanza hadi wapone kabisa. Inaweza kuchukua hadi miezi mitatu bila kuogelea,” amesema.
Simulizi ya waliotoboa
Ester John alitoboa kitovu miaka miwili iliyopita, amesema alifanya hivyo baada ya kuona kwenye mitandao ya kijamii mmoja wa wanamuziki nchini amefanya hivyo.
“Nilitamani urembo huo na kulazimika kuitafuta hiyo huduma,” amesema akibainisha kwamba ilimchukua miezi minne hadi kupona.
“Hata hivyo, bado nilikuwa natumia dawa ya kupaka katika eneo la kitovu ili kuwa sawa, nilifanya hivyo kwa mwaka mzima,” amesema.
Teresia Rwegoshora yeye anadai kujutia uamuzi wake wa kutoboa kitovu alioufanya miezi sita iliyopita.
“Nimekuwa na jukumu la kusafisha mara kwa mara sehemu niliyotoboa, naona kama ni mateso, nimekuja kujuta baada ya kutoboa,” amesema.
Rukia Jumbe amesema ilimchukua mwaka mzima hadi kupona kabisa baada ya kutoboa kitovu na ulimi mwaka 2024.
“Ni urembo ambao nilivutiwa nao baada ya kuona watu wametoboa na kupendeza japo baada ya ufanya hivyo kuna nyakati unazipitia zinakutesa kiafya, siku zingerudi nyuma nisingetoboa,” amesema.
Kwa Janeth Julius yeye ni tofauti, anasema anaufurahia urembo huo ambao anaamini unamfanya kuwa maridadi zaidi.
Madaktari watoa tahadhari
Wakizungumzia madhila ya urembo huo, baadhi ya madaktari wamesema pamoja na kwamba hawajawahi kupata kesi za changamoto ya waliotoboa, lakini kuna uwezekao wa kupata bakteria kwa baadhi yao.
Daktari bingwa wa kurekebisha maumbile Hospitai ya Taifa Muhimbili-Mloganzila, Dk Lauren Rwanyuma amesema mtu anapotoboa kitovu au ulimi, kwa kuwa kitu anachokiweka baada ya kutoboa ni kigeni katika mwili, kuna uwezekano wa kusababisha wadudu kuingia.
“Wapo wengine wanaweza kupata uvimbe au hata mzio, kwa kuwa si miili yote inakubaliana na hali ya kutoboa toboa,” amesema.
Amesema kiafya bado hajapata kesi ya namna hiyo, lakini kitaalamu hali hiyo inaweza kusababisha bakteria kwa mtu aliyetoboa.
Daktari wa meno mkoani Morogoro, Dk Hudson Mfinanga amesema mtu anayetoboa ulimi anapaswa kuchukua tahadhari ya kuepuka kumeza kipini alichokivaa kwenye ulimi.
“Ikitokea umemeza hicho kichuma (kipini) hilo ni tatizo, japo kiafya kwenye ulimi sidhani kama kuna madhara, maana wakati mwingine kuna urembo katika meno na watu wanawekea vyuma au nyaya za urembo wa meno,” amesema.
Amesema huwa kuna namna za kitaalamu urembo huo unafanyika na kwenye nchi zilizoendelea kuna hospitali maalumu kwa ajili ya kazi hiyo na si kujiwekea tu.
