Simanjiro yajipanga kukabili mabadiliko ya tabianchiSimanjiro yajipanga kukabili mabadiliko ya tabianchi

Simanjiro. Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara imeweka mikakati ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mradi maalumu wa kusaidia jamii kukabili ukame na mafuriko ya mara kwa mara.

Akizungumzia hilo leo Mei 23,2026 Mratibu wa mradi huo, Joseph Shamba amesema jamii itajengewa uwezo wa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi kupitia mpango wa Scale unaotekelezwa kwa ushirikiano wa Serikali na Benki ya Dunia.

Amesema mradi huo unatekelezwa katika mikoa 21 ya Tanzania Bara na mikoa mitano Zanzibar, huku Manyara ikiwa na halmashauri tatu zilizoingia awamu ya kwanza.

Kwa Simanjiro, mradi utatekelezwa katika kata sita za Oljoro Namba Tano, Shambarai, Msitu wa Tembo, Loiborsoit, Ruvu Remit na Kitwai zinazokabiliwa na ukame na mafuriko.

Madiwani na watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara wakifuatilia taarifa ya utekelezaji wa mradi wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Picha na Joseph Lyimo.

Shamba amesema mradi huo wa miaka mitano unalenga kuimarisha uwezo wa serikali kuu, serikali za mitaa na jamii katika kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Simanjiro, Kaleya Mollel amesema mradi huo utasaidia wafugaji na wakulima kukabiliana na changamoto za ukame na mafuriko.

Diwani wa Oljoro Namba Tano, Robert Melembuki ameishukuru Serikali kwa kuleta mradi huo akisema utasaidia kufanya tathmini sahihi ya madhara ya mabadiliko ya tabianchi na njia za kukabiliana nayo.

Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Mwanjaa Jacob amesema jamii inapaswa kutoa ushirikiano ili kuhakikisha mradi huo unaleta matokeo chanya.

Mkazi wa Shambarai, Edward Lukumay amesema eneo hilo limekuwa likikumbwa na mafuriko kila mwaka hali inayoharibu makazi na mashamba, hivyo mradi huo utakuwa msaada mkubwa kwa wananchi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *