
Dar es Salaam. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Kusini, kimedai kuwa watu wenye mapanga wamevamia maandalizi ya mkutano wa hadhara wa chama hicho uliokuwa ufanyike leo Mei 23, 2026 katika viwanja vya Soko Kuu Songea mkoani Ruvuma, na kuwashambulia wanachama pamoja na viongozi waliokuwa eneo hilo.
Mkutano huo uliokuwa umepangwa kufanyika Songea Mjini, ulitarajiwa kuongozwa na Kaimu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Kusini, Belchomans Ponera.
Mwananchi ilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Ruvuma, Marco Chilya ambaye amesema bado hajapata taarifa rasmi kuhusu tukio hilo hadi wakati habari hii inaandikwa.
“Sijazipata taarifa hizo, nipo nje kidogo ya mji kwa muda huu, naomba nifuatilie kwa watendaji wangu ili nijue nini kimetokea kuhusiana na taarifa hizo ulizonazo,” amesema.
Kwa mujibu wa Chadema, tukio hilo limetokea wakati viongozi na wanachama walipokuwa wakikamilisha maandalizi ya mkutano huo uliokuwa umeahirishwa Mei 14 mwaka huu kwa kile kilichoelezwa kuwa ni kupisha shughuli za Mwenge wa Uhuru.
Akizungumza kuhusu tukio hilo, Ponera ameliambia Mwananchi kuwa awali walikubaliana na Jeshi la Polisi kuusogeza mbele mkutano huo baada ya ushauri uliotolewa na jeshi hilo.
Hata hivyo, amesema hali ilibadilika ghafla walipokuwa wakifanya maandalizi ya mwisho ya mkutano huo.
Ponera amedai baada ya taarifa hiyo, kundi la watu aliowatuhumu kuwa ni askari pamoja na vijana wengine waliingia eneo hilo na kuanza kuwatawanya wanachama kwa nguvu.
Kwa mujibu wa Ponera, vurugu hizo zimesababisha taharuki katika viwanja hivyo huku baadhi ya wanachama wakidaiwa kujeruhiwa kwa mapanga wakati wa purukushani hizo.
Amedai watu hao wamenyofoa na kushusha bendera za Chadema zilizokuwa zimewekwa eneo la mkutano kabla ya kuondoka baada ya maandalizi yote kuvurugwa.
Akizungumzia athari za matukio ya namna hiyo kwa nchi, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema kuongezeka kwa matukio ya ukatili katika shughuli za kisiasa kunaweza kuifanya jamii kuanza kuyaona mambo hayo kuwa ya kawaida, hivyo kuenea kwa uovu.
“Matukio haya yatatengeneza usugu. Kujirudiarudia kwa matukio haya yatalifikisha Taifa katika hatua ambayo hata yanapotokea yataonekana kama ya kawaida, kila mtu atajiamulia cha kufanya na Serikali itakosa maana, vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vitakosa sababu ya uwepo wake.”
“Hata ugonjwa kuna wakati hupata usugu dhidi ya dawa, vivyo hivyo matukio ya uonevu yakidumu jamii huwa sugu, huyaona ya kawaida, na ndipo uovu huongezeka,” anasema.
