Matatani akituhumiwa kumuua mtendaji wa kijijiMatatani akituhumiwa kumuua mtendaji wa kijiji

Njombe. Jeshi la Polisi Mkoa wa Njombe linamshikilia mkazi wa kijiji cha Kiwe, Kata ya Mawengi wilayani Ludewa, Kalisto Haule (34), kwa tuhuma za kumuua kwa kumkata na panga Ofisa Mtendaji wa kijiji hicho, Peter Ng’ingo (52), kufuatia mgogoro unaodaiwa kuhusiana na faini za shughuli za ukataji miti, uuzaji wa kuni na uchomaji mkaa.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Mahamoud Banga amesema tukio hilo lilitokea Mei 22, 2026 saa 10:30 alfajiri katika kitongoji cha Wecha, kijiji cha Kiwe wilayani Ludewa.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Mei 23, 2026, Kamanda Banga amesema chanzo cha tukio hilo kinadaiwa kuwa ni hasira za mtuhumiwa kutokana na kutozwa faini mara kwa mara na mtendaji huyo kwa shughuli zake za ukataji miti kwa ajili ya kuni na uchomaji mkaa.

“Sababu ya tukio hili ni kujichukulia sheria mkononi, lakini kilichochochea ni faini za mara kwa mara ambazo mtuhumiwa alikuwa akitozwa na mtendaji kutokana na shughuli zake za ukataji miti kwa ajili ya kuni na uchomaji mkaa,” amesema Banga.

Wananchi wa kijiji cha Kiwe wakimsikiliza Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, alipofika kutoa pole na kuzungumza nao kufuatia tukio la mauaji ya mtendaji wa kijiji hicho.

Amesema marehemu alikuwa akimuita mtuhumiwa ofisini na kumtoza faini kwa kushirikiana na mwenyekiti wa kijiji kila alipobaini anaendelea na shughuli hizo zinazokiuka taratibu za mazingira.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, kabla ya kutekeleza mauaji hayo, mtuhumiwa alifika nyumbani kwa mwenyekiti wa kitongoji lakini hakumkuta, badala yake alimkuta mkewe na kumshambulia kwa kumpiga kwa ubapa wa panga mgongoni.

Baada ya hapo, inadaiwa mtuhumiwa alielekea nyumbani kwa mtendaji wa kijiji hicho ambako alivunja mlango wa nyumba kabla ya kufanya shambulio lililosababisha kifo chake.

Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Ludewa, Olivanus Thomas, amesema mtuhumiwa tayari amekamatwa na anaendelea kushikiliwa na Jeshi la Polisi kwa hatua zaidi za kisheria.

Thomas alitoa kauli hiyo jana Mei 22, 2026 alipofika kijijini Kiwe kutoa pole kwa familia ya marehemu pamoja na wananchi wa eneo hilo.

Amesema tukio hilo limeiacha familia ya marehemu katika majonzi makubwa, hasa watoto waliokuwa wakimtegemea baba yao kwa malezi na mahitaji ya kila siku.

“Kwa sasa jukumu la malezi ya watoto limebaki kwa mama pekee, jambo ambalo linaumiza jamii nzima,” amesema Thomas.

Aidha, amewataka wazazi na walezi kuzingatia malezi bora kwa watoto pamoja na kuwajenga katika misingi ya maadili na hofu ya Mungu ili kusaidia kupunguza matukio ya ukatili katika jamii.

Mkuu huyo wa wilaya pia amewahimiza wananchi kuendelea kudumisha mshikamano wa kijamii na kuimarisha ibada ili kuepusha matukio ya namna hiyo ambayo amesema yanachafua taswira ya Wilaya ya Ludewa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *