Chanzo cha picha, Getty Images
Jeshi la Marekani limesema limefanya mashambulizi mapya kusini mwa Iran, likilenga maeneo ya makombora ya Iran pamoja na boti zilizokuwa zikijaribu kuweka mabomu ya majini.
Kamandi Kuu ya Jeshi la Marekani (CENTCOM) imesema katika taarifa kwamba mashambulizi hayo yalifanywa kwa lengo la kujilinda na yalikusudiwa “kulinda wanajeshi wetu dhidi ya vitisho vinavyotokana na vikosi vya Iran.”
Msemaji wa CENTCOM, Kapteni Tim Hawkins, alisema jeshi la Marekani linaendelea kulinda vikosi vyake huku likionyesha kujizuia wakati wa kipindi cha usitishaji mapigano kinachoendelea.
Mashambulizi hayo yamefanyika wakati msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran, Esmail Baghaei, akisema kuwa kuna maendeleo fulani yaliyopatikana katika mazungumzo na Marekani, lakini akasisitiza kuwa makubaliano ya kumaliza mzozo huo “hayako karibu kufikiwa.”
Kwa mujibu wa Kapteni Hawkins, mashambulizi hayo yalilenga eneo karibu na Bandar Abbas, mji wa bandari ulioko kusini mwa Iran na makao ya kambi ya jeshi la wanamaji la Iran katika Mlango Bahari wa Hormuz.
Vyombo vya habari vya serikali ya Iran vilikuwa vimeripoti awali kuwa maafisa wa eneo hilo walikuwa wakichunguza chanzo cha milipuko iliyosikika katika Bandar Abbas.
Hadi sasa, Iran haijatoa tamko rasmi kuhusu mashambulizi hayo ya karibuni ya Marekani. Pia haijafahamika ni athari gani mashambulizi hayo yanaweza kuwa nayo kwa juhudi za kufikia makubaliano ya amani kati ya Washington na Tehran.
Mwishoni mwa wiki, Rais wa Marekani, Donald Trump, alikuwa ameashiria kuwa pande hizo zilikuwa karibu kufikia makubaliano, lakini baadaye alisema amewaagiza wapatanishi wa Marekani kutoharakisha mchakato huo.
Marekani na Iran zimekuwa zikiheshimu usitishaji mapigano tangu Aprili 8. Hata hivyo, Iran imeendelea kudhibiti usafiri wa majini katika Ghuba kupitia Mlango Bahari wa Hormuz, huku Jeshi la Wanamaji la Marekani likijaribu kuzuia shughuli za bandari za Iran.
Mzozo huo ulianza Februari 28 baada ya Marekani na Israel kufanya mashambulizi makubwa dhidi ya Iran.
Tehran ilijibu kwa kushambulia Israel na baadhi ya mataifa washirika wa Marekani katika Ghuba, pamoja na kuzuia kwa kiasi kikubwa usafiri wa majini katika Mlango Bahari wa Hormuz, hatua iliyochangia kupanda kwa bei ya mafuta duniani.
Pia unaweza kusoma:
