
Rais Masoud Pezeshkian ametangaza kwamba Iran haitasalimu amri kwa mashinikizo ya Marekani na matwaka ya kuchupa mipaka ya utawala huo, akisema wapatanishi wa Iran watahakikisha haki za taifa zinarejeshwa kikamilifu kupitia mchakato wa kidiplomasia.
Akizungumza katika mkutano na wanajumbe wa Chama cha Biashara siku ya Jumatatu, Pezeshkian alibainisha kuwa baada ya kushindwa katika upande wa kijeshi, adui sasa ameelekeza juhudi zake kwenye vita vya kiuchumi.
“Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haitasalimu amri kwa mashinikizo na matakwa ya kuchupa mipaka kwa hali yoyote ile,” amesema Rais Pezeshkian.
Rais ameongeza kwamba licha ya adui kuhamia kwenye vita vya kiuchumi baada ya kushindwa kijeshi, “serikali na sekta binafsi, kupitia mshikamano, ushirikiano na muawana, watafanikiwa pia katika awamu hii.”
Rais Masoud Pezeshkian pia amesifu mchango wa sekta binafsi na watendaji wa kiuchumi katika kusimamia hali nyeti ya nchi, akiwataja kama vinara wa mapambano ya kiuchumi katika vita kamili vya mseto vya adui.
