
Msemaji wa Jeshi la Iran ametoa onyo kali kwa Marekani kuwa hakuna kitendo chochote cha uchokozi kitakachoweza kulazimisha kufunguliwa kwa Lango la Bahari la Hormuz, kufuatia uamuzi wa Tehran wa kulifunga lango hilo la kimkakati baada ya Marekani kukiuka makubaliano.
Brigedia Jenerali Mohammad Akrami-Nia amesema kwamba: “Rais mkandamizaji na fisadi wa Marekani lazima ajifunze kuheshimu sheria za kimataifa, haki za mataifa, na heshima ya watu. Kama tulivyosema hapo awali, Lango la Hormuz halitafunguliwa kamwe kupitia vita, uhasama, au vitendo vya uchokozi vya Marekani.”
Jenerali Akrami-Nia vilevile amebainisha kuwa, ingawa Wamarekani walikubaliana na mipango ya Iran kuhusu Lango la Hormuz kama sehemu ya mkataba, baadaye walijaribu kuanzisha njia mpya “kupitia udanganyifu.”
Amesisitiza kuwa, “Majeshi ya Iran yalisimama kidete dhidi ya ukiukaji huo wa ahadi wa Wamarekani na kutangaza kuwa hatua yoyote katika Lango la Hormuz nje ya mipango iliyoelekezwa katika mkataba wa maelewano itajibiwa kwa uamuzi madhubuti kutoka kwa Jamhuri ya Kiislamu.”
Amesisitiza kuwa: “Njia pekee ya kulifungua Lango la Hormuz ni Marekani kuheshimu haki za taifa la Iran na kutii masharti ya mkataba wa maelewano uliomaliza vita.”
Wakati huo huo, mbunge mwandamizi wa Iran amesema kuwa Majlisi ya Ushauri ya Kiislamu (Bunge la Iran)imeanzisha rasmi mswada wa kutilia mkazo udhibiti wa Lango la Hormuz huku kukiwa ya ongezeko la uchokozi na ubabe wa Marekani katika njia hiyo ya kimkakati.
Mkuu wa Kamati ya Usalama wa Taifa na Sera ya Mambo ya Nje ya Bunge, Ebrahim Azizi, ametangaza hatua hiyo kwenye chapisho lake katika mtandao wa X siku ya Jumanne, akisema kuwa kuanzishwa kwa mswada huo kulienda sambamba na kudunguliwa kwa ndege zisizo na rubani (drones) za Marekani katika eneo hilo.
Iran imeweka vizuizi vya usafiri kupitia Lango la Hormuz tangu siku za mwanzo za vita vya kichokozi vya Marekani na utawala wa Kizayuni vilivyoanza Februari 28, na kusimama chini ya usitishaji vita mapema Aprili baada ya operesheni za kishujaa za Jamhuri ya Kiislamu za kulipiza kisasi zilizofanikiwa.
Mnamo Juni 17, Tehran na Washington zilitiliana saini Mkataba wa Maelewano (MoU) uliowezeshwa na Pakistan, ambao Kifungu cha 5 kinaweka jukumu la kufungua na kusimamia lango hilo mikononi mwa Iran.
Hata hivyo, Rais wa Marekani Donald Trump ametishia kutwaa udhibiti wa njia hiyo ya kimkakati, akidai Washington “italipwa pesa nyingi” kwa ajili ya usimamizi huo.
Hali hii inajiri wakati Tehran imetangaza kuwa Lango la Hormuz limefungwa “hadi taarifa nyingine” na angalau hadi “mwisho wa uingiliaji kati wa Marekani katika eneo hili.”
Iran imesisitiza mara kwa mara kuwa njia hiyo ya majini haitarejea kamwe katika hali yake ya kabla ya vita na kwamba itasimamiwa na nchi hiyo kwa mujibu wa sheria za kimataifa.