
Dodoma. Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Juma Mkomi ameagiza Wakurugenzi na Wakuu wa Idara za Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu wote kushiriki kikao kitakachofanyika jijini Dodoma, kwani kimebeba ajenda muhimu zaidi.
Mkoani ametoa kauli hiyo leo Jumatano Mei 26, 2026 akisema kikao cha wakuu hao kitafanyika Juni Mosi hadi 3, 2026 ambapo kwenye mkutano huo pia watahudhuria viongozi wa idara zinazojitegemea, Wakala za Serikali, Mashirika ya Umma, Sekretarieti za Mikoa pamoja na Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Katibu Mkuu amesema kikao hicho kitaongozwa na kaulimbiu ya ‘Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu katika Utumishi wa Umma Ulio Sikivu, Jumuishi, Wenye Matokeo na Uwajibikaji Kuelekea Dira 2050’.
Kwa mujibu wa Mkomi, kikao kazi hicho hufanyika kila mwaka kwa lengo la kutoa fursa kwa viongozi wa rasilimaliwatu kubadilishana uzoefu na kujadili namna bora ya kuboresha utekelezaji wa majukumu ya Serikali katika usimamizi wa rasilimaliwatu.
“Kikao pamoja na mambo mengine kitajadili matumizi ya mifumo ya kidijiti ikiwemo e-Uhamisho, e-Watumishi, e-Utendaji, e-Mrejesho pamoja na HR Assessment kwa kuzingatia shabaha na vipaumbele vya Taifa kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, lakini ni mambo ambayo yanapigiwa kelele, hivyo nawataka waje tujadiliane,” amesema Mkomi.
Amesema washiriki watapata nafasi ya kujadili mafanikio na changamoto zilizopo katika usimamizi wa rasilimali watu pamoja na kupendekeza njia bora za kuzitatua ili kuongeza ufanisi katika utumishi wa umma.
“Viongozi mbalimbali wenye dhamana ya kusimamia rasilimaliwatu katika utumishi wa umma watapewa maelekezo mahususi kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu usimamizi wa rasilimaliwatu. Hivyo, ninasisitiza viongozi tajwa kushiriki kikao kazi hicho wao wenyewe bila ya kuwakilishwa,” alisema Mkomi.
Amesema mgeni rasmi katika kikao hicho anatarajiwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete ambapo kuanzia sasa wahusika kwenye kikao hicho wanatakiwa kuanza kujisajili kupitia mfumo wa TSMS kwa kutumia tovuti ya Wizara kabla ya Mei 29, 2026 saa 6:00 usiku ili kurahisisha maandalizi ya kikao hicho.
Mkomi amesema ili kutambua umuhimu wa kikao, washiriki wote wanatakiwa kufika katika Ukumbi wa Mabeyo Hall Mei 31, 2026 kuanzia saa 4:00 asubuhi kwa ajili ya kuchukua vitambulisho vyao kabla ya kuanza kwa kikao kazi hicho.
