Jumuiya ya maridhiano Tanzania yajibu muswada wa maseneta wa MarekaniJumuiya ya maridhiano Tanzania yajibu muswada wa maseneta wa Marekani

Dar es Salaam. Jumuiya ya Maridhiano na Amani Tanzania (JMAT), imeitaka Serikali ya Marekani kuwakemea maseneta Jeanne Shaheen na Ted Cruz na madai yao kwenye muswada wa sharia kuhusu Tanzania yabaki maoni binafsi yasiyoakisi msimamo rasmi wa nchi hiyo.

Imesema, kauli ya maseneta hao ni uzushi, uchochezi wa wazi ambao hauwezi kukubalika kwa namna yeyote uwe wa kisiasa au wa kidini.

Msimamo ni kufuatia muswada mpya uliowasilishwa na maseneta hao  wiki iliyopita mjini Washington wa kutathmini upya uhusiano wa Marekani na Tanzania, wakitaja madai ya kuzorota kwa demokrasia pamoja na mambo mengine ikiwemo uwepo wa ubaguzi wa kidini nchini.

Akizungumzia kinachofanywa na maseneta hao  leo Mei 26,2026 kupitia mkutano  na Waandishi wa Habari jijini Dodoma, Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo, Sheikh Alhad Mussa Salim, amesema wanapingana na kauli ya maseneta hao.

“Uwepo wetu hapa ni kielelezo tosha yanayosemwa na maseneta hao ni uzishi na ni kitu kisiochokubalika na uchochezi wa wazi wazi,” amesema na kuongeza;

“Tunaitaka Serikali ya Marekani mara moja, iwakemee maseneta hao na ikanushe kauli hiyo ibaki kuwa yao binafsi ambayo kwetu sisi Watanzania imetuumiza,” amesema.

Amesema undugu uliopo Tanzania ni wa damu, ubindamu na hakuna mwenye uwezo wa kuwatengenaisha Watanzania.

 “Tunaomba waendelee kuheshimu nchi yetu ambayo inatawaliwa kwa misingi ya sheria, kanuni na katiba, waheshimu mamlaka yetu, uchochezi wa namna yeyote uwe wa kidini na kisiasa hatutaukubali kwa namna yeyote ile,” amesema.

Amesema, mambo yaliyotokea Oktoba 2025 Serikali imeyashughulikia kulingana na sheria zilizopo na inaendelea kushughulikia.

Sheikh Salim ameomba Tanzania iachwe kwani kinachofanyika huenda ni kutokana na wivu, kwani taifa lilivuka salama yalitokea Oktoba 29, 2025.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa JMAT, Askofu Israel Maasa, amesema Jumuiya hiyo imepokea kwa uzito taarifa hiyo ya ubalozi wa Marekani nchini Tanzania

Amesema Tanzania hakuna mtu aliyenyimwa uhuru au kufanyiwa ghasia kwa sababu za dini.

 “Kwa hakika kabisa, mtu, nchi au taasisi yeyote inayotoa shutuma za namna hii itakuwa haifahamu Tanzania, haina taarifa sahihi au kupotswa na watu wenye husda na taifa letu au wenye nia zao tofauti na nchi yetu,” amesema.

Askofu Maasa ameikumbusha Marekani na jumuiya za kimataifa, Tanzania imejengwa kupitia misingi ya umoja wa kitaifa mshikamano wa kijamii, kuheshimiana kwa dini, kuishi pamoja tangu kupatikana kwa uhuru 1961.

Askofu huyo amesema tuhuma za uwepo wa ubaguzi wa kidini nchini Tanzania zimewasikitisha, kuwakasirika na kuwafedhehesha.

“Raia wa Marekani wanaoishi Tanzania ni mashahidi wa kushamiri kwa uhuru wa kuabudu hapa nchini, hatutaki kuamini kwamba Marekani, taifa ambalo sote tuliumizwa na kulia pamoja wakati wa mashambulizi ya ugaidi Dar es Salaam 1998 linaweza kufanya kazi ya kupandikiza chuki za kidini hapa nchini,” amesema.

Kutokana na hayo, Jumuiya hiyo imeitaka bunge la Marekani kukataa hoja hiyo ya kibaguzi ya baadhi ya maseneta wake ambayo amedai haina ukweli bali inalemnga kupandikiza chuki nchini.

“Tunaomba Serikali ya Rais Samia kufanya mapitio ya mahusiano ya kidiplomasia baina ya Tanzania na Marekani ili kuweka msimamo wa kutoivumilia uchonganishi wa kidini ambao unaweza kuliingiza taifa katika matatizo makubwa,” amesema.

Askofu Maasa amesema, Rais Samia ameoinyesha nia ya dhati ya kuchukua hatua dhidi ya matukio yaliyotokea Oktoba 2025 ikiwa ni pamoja na kuunda tume ya uchunguzi na jinai ili uwajibikaji wa haki uchukue nafasi na katiba ipatikane kama alivyoahidi.

Askofu huyo amesema kama kweli Marekani ina nia njema inapaswa kuunga mkono hatua zinazochukuliwa na serikali badala ya kuwa chanzo cha migogoro na migawanyiko.

“Tunatoa wito kwa wadau wote wa ndani na nje ya nchi kuendelea kuunga mkono mazungumzo ya kujenga na kuheshimu misingi ya kidiplomasia na kuendeleza ushirikinano unaojenga mahusiano ya mataifa yetu,”amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *