
Jeshi la Jamhuri ya Kiislamu ya Iran limetoa onyo kali kuhusu mashambulizi ya kulipiza kisasi yatakayokuwa “mazito na makali zaidi” iwapo tawala za Marekani na Israel zitafanya uchokozi mpya.
Jeshi limesisitiza kuwa limehuisha orodha yake ya shabaha na liko tayari kikamilifu kwa vita.
Katika mahojiano na Televisheni ya Al Jazeera, Brigedia Jenerali Abolfazl Shekarchi, msemaji mwandamizi wa Majeshi ya Iran, amesema kuwa jibu lolote dhidi ya uchokozi mpya litakuwa tofauti kabisa na yale yaliyoshuhudiwa huko nyuma.
Amesema kuwa maadui bila shaka watakumbana na mambo ya kushtukiza na mbinu mpya za kivita. Amesema iwapo eneo hili litaingia katika mzunguko mwingine wa vita, mashambulizi ya Iran yatavuka mipaka ya kikanda.
Kadhalika, Jenerali Shekarchi aligusia suala la mauzo ya mafuta, akionya kuwa iwapo vita vitaanza upya na Iran ikazuiliwa kuuza mafuta yake, basi itazuia mafuta yote yasitoke katika eneo la Ghuba ya Uajemi.
Uchokozi wa kihalifu wa Marekani na Israel dhidi ya Iran ulianza mnamo Februari 28 kupitia mashambulizi ya anga yaliyopelekea kuuawa shahidi kwa viongozi waandamizi na makamanda wa Iran, akiwemo Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah al-Udhma Seyyed Ali Khamenei (Mwenyezi Mungu amrehemu).
Majeshi ya Iran yalijibu mapigo kwa kurusha makombora na ndege zisizo na rubani kwa siku arubaini mfululizo yakilenga ngome za utawala wa Israel katika ardhi zinazokaliwa kwa mabavu na utawala huo, pamoja na kambi na zana za kijeshi za Marekani kote Asia Magharibi.
Aidha, Iran ilifunga Lango Bahari la Hormuz kwa maadui na washirika wao kufuatia kuanza kwa vita hivyo vya kichokozi.
Baada ya Marekani kutangaza usitishaji vita, mtawala wa nchi hiyo, Donald Trump, aliamuru vikwazo haramu dhidi ya meli na bandari za Iran. Hatua hiyo ni ukiukaji wa makubaliano ya kusitisha mapigano yaliyosimamiwa na Pakistan na kuanza kutekelezwa Aprili 8.
