Dar es Salaam. Wakati teknolojia ya akili unde (AI), ikizidi kushika kasi duniani, kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Leo XIV, ameonya teknolojia hiyo akisema inapaswa kudhibitiwa na kuvuliwa uwezo wa kuleta madhara kabla haijageuka tishio kwa utu wa binadamu.
Katika waraka wake wa kwanza wa mafundisho uitwao Magnifica Humanitas (Ubinadamu Mkuu), Papa amesema dunia ipo katika njia panda ya maadili huku maendeleo ya AI yakihatarisha kuibua kile alichokiita “utumwa mpya wa kidijitali.”
Papa Ameyasema hayo Mei 25, 2026 katika ukumbi wa Synod Hall uliopo Vatican City, wakati wa uzinduzi rasmi wa waraka wake huo wa kwanza wa mafundisho.
“Najua neno hilo ni zito, lakini nimelichagua kwa makusudi kwa sababu wakati huu unahitaji lugha inayoweza kuvuta usikivu wa dunia,” alisema Papa Leo.
Waraka huo, ambao kwa kawaida huandikwa kwa maaskofu wa Kanisa Katoliki lakini sasa hutumika kama ujumbe wa dunia nzima, umejikita zaidi katika athari za AI kwa jamii, siasa, vita na haki za binadamu.
Kwa mujibu wa Papa huyo, kuna hatari dunia ikarudia makosa ya zamani kwa kuruhusu teknolojia kutumika kuwanyonya watu, hasa katika namna AI inavyozalishwa na kutumika.
Alisema matumizi ya AI katika vita yanaongeza hatari ya migogoro kwa sababu yanaweza kupunguza ushiriki wa maamuzi ya kibinadamu na kufanya vita ionekane jambo la kawaida.
“Hakuna algoriti inayoweza kufanya vita kuwa vya maadili,” aliandika Papa huyo, akionya pia dhidi ya mashindano ya silaha zinazotumia AI.
Katika waraka huo, Papa alikosoa pia matumizi ya AI kwenye siasa, hasa kupitia picha na video zinazoweza kubadilishwa kwa lengo la kupotosha umma au kueneza propaganda.
Wakati wa uzinduzi wa waraka huo, mtaalamu wa AI na mwanzilishi mwenza wa kampuni ya Anthropic, Christopher Olah, amesema hata maabara za AI zinafanya kazi katika mazingira yenye shinikizo la kibiashara ambalo wakati mwingine linaweza kwenda kinyume na kufanya jambo sahihi kwa jamii.
Papa Leo pia alitoa wito maalumu kwa watengenezaji wa AI akisema kila uamuzi wa kiteknolojia unaonyesha namna wanavyoutazama ubinadamu.
Waraka huo unaonekana kuwa ujumbe mzito kwa viongozi wa dunia, kampuni za teknolojia na watafiti wa AI, wakati ambapo matumizi ya akili unde yanaendelea kuongezeka kwa kasi duniani.
