Dar es Salaam. Mkuu wa Jeshi la Polisi Tanzania (IGP), Camilius Wambura ameeleza namna askari wa jeshi hilo walivyokuwa wakiishi kwenye makazi duni kwa muda mrefu kabla ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan kuanza ujenzi wa makazi bora ya kisasa kwa ajili yao.
IGP Wambura amesema hayo leo Alhamisi Mei 28, 2026 mbele ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla ya kuhitimisha Mafunzo ya Maofisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Polisi iliyofanyika Kurasini jijini Dar es Salaam.
Katika hafla hiyo, video ilionyeshwa ikilinganisha makazi ya zamani ya askari polisi na majengo mapya yanayoendelea kujengwa. Akizungumza baada ya video hiyo kuonyeshwa, IGP Wambura amesema hali ya makazi hayo ilikuwa mbaya kiasi cha kufanana na kambi za wavuvi.
“Unayoona Mheshimiwa Rais sio kambi ya wavuvi, hayo ndiyo makazi ya askari polisi uliyoyakuta,” amesema Wambura.
Amesema makazi hayo ndiyo yaliyokuwa yakitumiwa na askari polisi kwa muda mrefu wakati wakitekeleza jukumu lao la kulinda raia na mali zao katika mazingira magumu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Amiri Jeshi Mkuu, Samia Suluhu Hassan akiwasili katika uwanja wa Chuo cha Taaluma ya Polisi kilichopo Kurasini Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya kuhitimisha Mafunzo ya Maafisa na Wakaguzi Wasaidizi wa Jeshi la Polisi, Mei 28, 2026.
Kwa mujibu wa IGP Wambura, Rais Samia hakuridhishwa na hali ya makazi hayo na akaamua kutoa fedha kwa ajili ya ujenzi wa nyumba bora za askari polisi nchini.
Amesema makazi mengi ya zamani tayari yamevunjwa ili kupisha ujenzi wa maghorofa mapya ya kisasa, huku vibanda viwili vikibaki kama sehemu ya historia ya jeshi hilo.
“Tutaacha vibanda viwili kwa ajili ya kumbukumbu kwamba jeshi hili liliwahi kupitia kadhia hii, lakini alikuja Rais Samia akatutoa ndani ya mazingira hayo na kutuweka kwenye majengo haya. Sisi ni akina nani tusisimulie hadithi hii nzuri,” amesema.
Mbali na suala la makazi, IGP Wambura ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuliwezesha Jeshi la Polisi katika maeneo mbalimbali ikiwemo miundombinu, vitendea kazi na bajeti.
Amesema Serikali ya Rais Samia imeonyesha dhamira ya dhati ya kuboresha utendaji wa jeshi hilo kwa kutatua changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikilikabili.
“Kwa upande wa majengo tumetekeleza jumla ya miradi ya ujenzi na ukarabati wa majengo 320, tumekamilisha majengo 174 na tunaendelea na miradi mingine 146 ambayo ipo katika hatua mbalimbali,” amesema.
IGP Wambura pia ameishukuru Serikali kwa kulipatia Jeshi la Polisi magari 1,394 ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitatu, hatua aliyosema imeondoa kabisa matumizi ya magari mabovu yaliyokuwa yakisababisha usumbufu mkubwa kwa askari.
“Mheshimiwa Rais, nimewahi kumuona ofisa wa polisi akielekea ofisini huku gari analotumia likisukumwa kutoka nyumbani hadi ofisini kwa sababu halijawaka. Likifika ofisini linasukumwa tena hadi nyumbani. Sasa magari yote mabovu yameondolewa baada ya Rais Samia kutupatia magari haya,” amesema.
Katika muhula wa pili wa uongozi wa Rais Samia, IGP Wambura amesema Jeshi la Polisi linaendelea kujipanga kuboresha zaidi utendaji wake kwa kuimarisha falsafa ya polisi jamii pamoja na matumizi ya teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama).
Amesema lengo la hatua hiyo ni kuwafikia wananchi kuanzia ngazi ya familia hadi kata ili kujenga ushirikiano wa karibu katika mapambano dhidi ya uhalifu.
“Hii ni mwarobaini wa kuwafikia wahalifu mapema na kuzuia uhalifu kabla haujatokea. Tunalenga kujenga jamii inayotambua wajibu wake na haki zake katika suala zima la haki jinai na usalama wao,” amesema.
Aidha, IGP Wambura amewakumbusha maofisa waliohitimu mafunzo hayo umuhimu wa kuwa wazalendo katika kazi zao, akisisitiza kuwa kiapo walichokula ni ahadi itakayowaongoza katika kipindi chote cha utumishi wao.
