
Dar es Salaam. Kesi ya kuchapisha taarifa za uongo mtandaoni inayomkabili meya wa zamani wa Kinondoni na Ubungo, Boniface Jacob na mwanaharakati Godlisten Malisa, inasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu, ili iweze kuendelea na usikilizwaji katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
Hata hivyo, mshtakiwa Malisa ni mgonjwa na yupo nchini Marekani kwa matibabu.
Hayo yameelezwa leo Mei 28, 2026 na mdhamini wa Malisa, ambaye hakujitambulisha jina mahakamani hapo, wakati kesi hiyo ilipoitwa kwa ajili ya kutajwa.
Amesema Malisa amefanyiwa upasuaji na anaendelea na matibabu na anatarajia kuruhusiwa kutoka hospitali Juni 26, 2026.
Awali, wakili wa Serikali Pancras Protas ameieleza mahakama hiyo mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ushindi Swallo, anayesikiliza kesi hiyo.
Protas amedai kuwa kesi imeitwa kwa ajili ya kutajwa, ikisiburi uamuzi wa Mahakama Kuu, baada ya Jamhuri kukata rufaa kupinga uamuzi uliotole na Mahakama ya Kisutu wa kukataa mashahidi wa Jamhuri kulindwa wakati wa kutoa ushahidi.
“Mheshimiwa hakimu, kesi hii imeitwa kwa kutajwa na bado tunasubiri uamuzi wa Mahakama Kuu, hivyo kwa sababu hiyo tunaomba mahakama itupangie tarehe nyingine,” amedai Wakili Protas.
Baada ya kutoa taarifa hiyo, wakili wa utetezi, Dickson Matata akishirikiana na Gloria Ulomi, walikubaliana na ombi la upande wa Jamhuri la kuomba ahirisho.
Hakimu Swallo ameahirisha kesi hiyo hadi Julai 20, 2026 na kuelekeza siku hiyo mshtakiwa huyo awepo mahakamani.
“Kesi naiahirisha hadi Julai 20, 2026 kwa kutajwa na siku hiyo mshtakiwa anatakiwa awepo Mahakamani hapa,” amesema Hakimu Swallo.
Itakumbukwa, Serikali ilikata rufaa Mahakama Kuu kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kisutu wa kukataa ombi lao la kulindwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka katika kesi hiyo.
Uamuzi huo ulitolewa Mei 5, 2025 na Hakimu Swallo, aliyesikiliza ombi hilo, ambapo katika uamuzi wake alitupilia mbali ombi la Serikali kwa kueleza kuwa halina mashiko.
Kutokana na hali hiyo, Serikali ilikata rufaa Mahakama Kuu, kupinga uamuzi uliotolewa na Mahakama hiyo.
Jacob, maarufu Boni Yai, mkazi wa Mbezi Msakuzi, Dar es Salaam, mfanyabiashara na mwanasiasi, aliyewahi kuwa meya wa Manispaa ya Ubungo na Malisa, mkazi wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, wote kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka matatu ya kutoa taarifa za uwongo mitandaoni.
Wanadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao yao ya kijamii ya X (zamani Twitter) na Instagram, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia.
Hata hivyo, wakati kesi hiyo ikisubiri uamuzi wa Mahakama Kuu, tayari mashahidi watano wa upande wa Serikali wameshatoa ushahidi wao dhidi ya washtakiwa hao.
Katika kesi ya msingi, washtakiwa wanakabiliwa na kesi ya jinai namba 11805/2024, yenye mashtaka matatu.
Wanadaiwa kutenda makosa hayo kati ya Machi 19 na Aprili 22, 2024 jijini Dar es Salaam.
Katika mashtaka hayo, wanadaiwa kuchapisha taarifa za uwongo katika mitandao yao ya kijamii ya X (zamani Twitter) na Instagram, kinyume na kifungu cha 16 cha Sheria ya Makosa ya Mtandao namba 14 ya mwaka 2015, wakilihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia.
Katika tuhuma hizo, wanadaiwa kulihusisha Jeshi la Polisi na mauaji ya raia akiwemo mkazi wa Dar es Salaam, Robert Mushi maarufu kama Babu G na aliyekuwa dereva wa magari ya watalii, Wilaya ya Karatu mkoani Arusha, Omari Msemo.
Pamoja na mambo mengine Jacob aliandika kuwa, licha ya ndugu kutoa taarifa Polisi Kanda Maalumu Dar es Salaam lakini kila siku Polisi walikuwa wakisema kuwa halijapata taarifa wala fununu zozote na kuwataka ndugu waendelee kuwa wavumilivu wakiendelea kumtafuta.
Hata hivyo ndugu walidokezwa na msiri mmoja akiwataka waende Hospitali ya Polisi Kilwa Road mkachungulie vyumba vya kuhifadhi maiti ambako walikwenda wakamkuta ndugu yao akiwa ameua na wahusika wa hospitali walidai kuwa mailiti ilipelekwa tangu Aprili 10, 2024 na askari wa Jeshi la Polisi.
Katika andiko lake alihoji: “Maiti ina siku 12 HospItali ya Polisi Kilwa Road haijui bila Jeshi la Polisi kujua ipo hapo? Polisi walioipeleka maiti ni wa nchi gani?
Kwa mara ya kwanza, washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo Mei 6, 2024 na kusomewa jumla ya mashtaka matatu, mawili kati ya hayo yanamkabili Jacob pekee yake, huku Malisa akikabiliwa na shtaka moja.
