Viongozi Jumuiya ya Wafanyabiashara Makambako wabebeshwa mzigo wa kodiViongozi Jumuiya ya Wafanyabiashara Makambako wabebeshwa mzigo wa kodi

Njombe. Viongozi wa Jumuiya ya Wafanyabiashara waliochaguliwa kuongoza kwa kipindi cha miaka minne ijayo katika Halmashauri ya Mji wa Makambako, mkoani Njombe, wametakiwa kutatua changamoto zinazowakabili wafanyabiashara, ikiwemo suala la kodi kubwa inayodaiwa kutokidhi kiwango cha uzalishaji wao.

Katika uchaguzi huo, Siphaely Msigala amechaguliwa kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara Makambako kwa kupata kura 161 kati ya kura 161 zilizopigwa.

Makamu Mwenyekiti ni Abusalum Magoma aliyepata kura 160, Katibu ni Edson Gadau aliyepata kura 161 na Mtunza Hazina ni Upendo Lutambi aliyepata kura 161.

Hayo yameelezwa leo Mei 28, 2026 na wafanyabiashara katika uchaguzi wa viongozi wa jumuiya hiyo uliofanyika katika ukumbi wa Midtown, Halmashauri ya Mji wa Makambako mkoani Njombe.

Wamesema jumuiya hiyo inatakiwa kuwatembelea wafanyabiashara wadogo ili kujua changamoto zao, hatua ambayo itasaidia kuwahamasisha kujiunga na jumuiya hiyo tofauti na ilivyo sasa.

Aidha, wameeleza kuwa bado kuna changamoto ya uelewa kuhusu umuhimu wa jumuiya hiyo, hivyo viongozi wanapaswa kutenda haki kwa wanachama na wasio wanachama ili wawe mabalozi kwa wale ambao bado hawajui umuhimu wa kujiunga na jumuiya ya wafanyabiashara.

Baadhi ya wafanyabiashara, akiwemo Martin Njavike, wamewataka viongozi waliochaguliwa kuhakikisha wanatatua changamoto za kodi ambazo zimekuwa kero kwa wafanyabiashara wengi.

“Viongozi pia watenge muda wa kutembelea masoko mbalimbali na kusaidia kuunda uongozi wa jumuiya katika maeneo hayo ili kurahisisha utendaji kazi,” amesema Njavike.

Akizungumza baada ya kuchaguliwa kuongoza Jumuia hiyo,  Msigala amesema watafanyia kazi maoni yote yaliyotolewa na wafanyabiashara huku akisisitiza umuhimu wa mshikamano katika kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili.

“Kwanza tutahakikisha tunajenga umoja wetu na mshikamano wenye nguvu kwa kuwafikia wafanyabiashara wote kupitia viongozi kwenye maeneo maalumu ya kibiashara,” amesema Msigala.

Awali, Kaimu Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Njombe, Beatrice Kahoho, amewataka wafanyabiashara hao kuendelea kushirikiana na mamlaka hiyo ili kuleta maendeleo mkoani humo.

Amesema kuna mabadiliko ya ulipaji wa kodi ya asilimia mbili kwa mazao ya misitu ambapo kuanzia Juni 1, 2026 wafanyabiashara watatakiwa kufika ofisini kulipa kodi hiyo badala ya kulipa katika mageti ya ushuru.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *