Arusha. Zaidi ya wananchi 1,300 katika Kijiji cha Jangwani, Kata ya Mto wa Mbu, Wilaya ya Monduli mkoani Arusha, wamelazimika kuhama makazi yao baada ya nyumba zao kuzingirwa na maji ya mafuriko.
Mafuriko hayo yamesababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, katika Wilaya ya Monduli baadhi ya miteremko imekuwa ikielekeza maji yake katika Ziwa Manyara ambalo limejaa kupita kiasi na kusababisha kufurika na kuingia katika makazi ya wananchi.
Athari hizo zimeathiri zaidi ya kaya 400 huku zaidi ya ekari 350 za mashamba ya ndizi na mpunga zikiharibiwa.
Akizungumza kuhusu hali hiyo, Diwani wa Kata ya Mto wa Mbu, Huseni Musa amesema maji hayo yametoka katika mito mbalimbali ikiwemo Makuyuni, Buger na Babati ambayo yote huelekeza maji yake katika Ziwa Manyara.
Amesema tangu mwaka 2022/23 wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakikumbwa na changamoto ya mafuriko kutokana na mito hiyo kumwaga maji mengi katika ziwa hilo ambalo kwa sasa limejaa na kuathiriwa na tope kutokana na kukosa matengenezo ya muda mrefu.
Musa amesema kutokana na mafuriko hayo wananchi wengi wameyakimbia makazi yao kuokoa maisha yao.
“Baadhi ya wananchi wamehifadhiwa na ndugu zao, lakini wenye uwezo wameanza kupanga nyumba maeneo ya Mto wa Mbu mjini,” amesema diwani huyo.
Ameongeza kuwa tayari amewasilisha kilio hicho kwa halmashauri ili kuona namna ya kuwasaidia wananchi kupata maeneo mbadala ya kuishi na kulima pamoja na msaada wa chakula katika kipindi hiki cha mpito.
Mkazi wa eneo hilo, Elirehema Mbayani, amesema mvua za Februari zilichangia ongezeko la maji na hali ilianza kuwa mbaya zaidi mwezi Aprili ambapo maji yalianza kuingia katika Kitongoji cha Jangwani kabla ya kusambaa hadi maeneo ya Magomeni.
Amesema hofu kubwa ya wananchi ni uwezekano wa kuendelea kwa mvua zaidi kufuatia utabiri wa hali ya hewa unaoonyesha uwezekano wa mvua kubwa katika siku zijazo.
“Tuliona hatari mapema tukahama. Tunashukuru Mungu hakuna vifo wala majeraha, lakini tunahofia mvua za El Niño zinaweza kuongeza madhara. Tunaomba Serikali itusaidie kupata maeneo mbadala salama ya kuishi,” amesema.
Mkazi mwingine, Rehema Richard, amesema wananchi wanakabiliwa pia na hatari ya njaa baada ya mashamba yao kuharibiwa na mafuriko.
“Tunaomba msaada wa chakula cha haraka. Tupo kwa ndugu na majirani lakini hawataweza kuhimili kwa muda mrefu kulisha,” amesema.
Aidha, amesema kuna hofu kuhusu usalama wa miundombinu ya umeme, hasa nguzo zilizozungukwa na maji, hali inayoweza kusababisha hitilafu au madhara kwa wananchi hususan watoto wanaocheza karibu na maeneo hayo.
Mbunge wa Jimbo la Monduli, Isack Joseph Copriano, alipotembelea eneo hilo alitoa msaada wa Sh3 milioni kwa ajili ya chakula cha waathirika.
Pia, ameahidi kuwasilisha kero hiyo Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Kitengo cha Maafa kwa ajili ya hatua za haraka za msaada.
“Nawapa pole sana kwa changamoto hii. Nitalifikisha suala hili Ofisi ya Waziri Mkuu ili wananchi hawa wapate msaada wa haraka,” amesema mbunge huyo.
Ameongeza kuwa atawasiliana na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) pamoja na taasisi nyingine kuhakikisha hatari zinazoweza kusababishwa na miundombinu ya umeme zinashughulikiwa kwa haraka.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Gloria Kimathi amesema suala hilo linaendelea kufanyiwa tathmini na taarifa rasmi itatolewa baada ya taratibu za kitaalamu kukamilika.
