Haya yanazuia dua yako kujibiwa Haya yanazuia dua yako kujibiwa 

Dua ni ibada na ni sababu, lakini athari zake hazipimwi kwa kupatikana kwa kile kinachoombwa mara moja; kwani jibu linaweza kuwa kwa kupewa kitu kwa kucheleweshwa au kuondolewa balaa. 

Aidha, jibu linaweza kuzuiwa kwa haraka (kukosa subira), kughafilika kwa moyo, na maasi. 

Uislamu unabainisha kwamba kujibiwa kwa dua hakufungamani na maneno pekee, bali kunahusiana na unyenyekevu wa kweli, haja ya kinachoombwa, uhudhurishaji wa moyo, kufuata Sunna (muongozo wa Mtume), na kuomba kupitia majina ya Allah Mtukufu. 

Hakika dua ni silaha ya muumini, na ni miongoni mwa tiba zenye manufaa makubwa. Ni adui wa balaa; huizuia, huiondoa, au huipunguza ikiwa tayari imeshuka. 

Na watu kuhusu sababu hizi wamegawanyika katika makundi matatu: Mosi, kuna wanaozipuuza (sababu) kabisa na kuziacha. Pili, kuna wanaozitegemea kupita kiasi na kuzifanya tegemeo la mioyo yao. Hawa wote wawili wamekosea.

Tatu, ni njia ya kati  kuwa mtu amtegemee Allah Mtukufu, amuombe na amwelekee Yeye, huku akizichukua sababu na kuzitekeleza. Sababu peke yake hazitimizi matokeo, bali hutimia kwa taufiq (uwafikishwaji) na kuwezeshwa na Allah.

Amesema Ibn Taymiyyah (Allah amrehemu): “Dua ni miongoni mwa sababu alizozikadiria Allah Mtukufu. Kuelekea kwenye sababu peke yake (bila kumtegemea Allah) ni kufanya ushirikina katika Tawhidi (upwekeshaji); na kupuuzia sababu kabisa ni upungufu wa akili; na kuziacha kabisa ni kasoro katika Sharia. 

Bali mja (mtu) anatakiwa kumtegemea Allah Mtukufu katika dua yake na matamanio yake, na Allah Mtukufu humpa sababu anazotaka.” Na amesisitiza umuhimu wa sababu hizi Ibn al-Qayyim (Allah amrehemu) akisema kwamba Qur’ani yote inaonesha wazi kuwa mambo ya dunia na Akhera yanategemea sababu na matendo. 

Anasema: “Mwenye kuelewa suala hili vizuri, atanufaika sana; hatategemea kudura ya Allah pekee kwa ujinga au uzembe, bali atapambana na kudura  kwa kudura, na kuzuia kudura kwa kudura.” 

Linalopaswa kwa mtu ni kuomba kwa dua zilizo pokewa (zilizothibiti), kwani dua ni miongoni mwa ibada bora zaidi. Na Allah ametukataza kufanya uvukaji mipaka ndani yake, hivyo ni wajibu kufuata yale yaliyowekwa na kusuniwa, kama ilivyo katika ibada nyingine

Hali za dua 

Mtume wa Allah (Rehema na amani ziwe juu yake) amesema : “Hakuna Muislamu anayemuomba Allah dua isiyo na dhambi wala kukata undugu, isipokuwa humpa moja kati ya haya matatu: Ama humharakishia jibu lake, au humwekea akiba Akhera, au humuepushia shari mfano wake.” Masawahaba wakasema: Basi tutaomba sana..”

Kadhalika Mtume wa Allah  amesema: “Hakuna kinachoongeza umri isipokuwa wema, wala hakuna kinachorudisha qadar (makadirio ya Allah kwa mja-Kudura) isipokuwa dua; na mtu hunyimwa riziki kwa sababu ya dhambi anayofanya.” 
Kwa sababu hii, Ibn Qayyim alieleza hali za dua pamoja na balaa, akasema:

Dua ina hali tatu: Mosi, iwe na nguvu kuliko balaa, basi huiondoa. Pili, iwe dhaifu kuliko balaa, basi balaa humshinda mja, lakini dua inaweza kulipunguza kidogo balaa. Tatu: zilingane (kati ya dua na balaa), zikazuiana kila moja na nyingine. 

Hadithi hizi na maneno ya wanazuoni yanaonesha umuhimu wa dua, na kwamba muumini hupata kheri katika hali zote: Ama  Allah humtimizia alichokiomba, au humwekea akiba Akhera, au humuepushia shari kwa kiwango kilekile alichoomba. 

Hivyo basi, dua ni yenye manufaa katika kila hali, na ni ibada kubwa; kwani Mtume wa Allah amesema: “Dua ni ibada.” Kisha akasoma:

“Na Mola wenu amesema: Niombeni, nitakujibuni…” [40: 60] Na hakuna anayeshindwa kuomba au akaacha dua isipokuwa ni mwenye hasara. 

Hakuna mkono ulionyoshwa kwa Allah Mkarimu ukarudishwa mtupu; bali mja lazima apewe mojawapo ya mambo matatu. Lakini kuna tofauti kati ya haja iliyoombwa; kwani kujibiwa dua ni suala pana zaidi. 

Inawezekana Allah Mtukufu akajibu dua ya mja kwa kumpa thawabu akhera au kumuepushia shari, hata kama hakumpa kile alichokiomba hapa duniani kwa hekima anayojua Allah Mwenyewe.

Vizuizi vya kujibiwa dua 

Miongoni mwa vizuizi vikubwa vya kujibiwa dua ni haraka na kukosa subira. Mtu huomba dua, kisha anapoona jibu limechelewa, huchoka na kusema: “Nimeomba sana lakini sijajibiwa,” kisha huacha dua. 

Amesema Ibn Taymiyyah: “Mja hujibiwa maadamu hajafanya haraka… na ajue kuwa ushindi upo pamoja na subira, na faraja ipo pamoja na dhiki.” Na Ibn al-Qayyim alifananisha hali hii na mtu aliyepanda mbegu kisha akaacha kuitunza kwa sababu tu ameona imechelewa kukua. 

Si haraka tu, bali pia kuna vizuizi vingine, kama vile: dua yenyewe kuwa na mambo yasiyopendwa na Allah Mtukufu (kama kuomba dhambi). Moyo wa muombaji kuwa dhaifu au umeghafilika.  
Kufanya maasi na kula haramu. Katika hadithi, Mtume amesema:

“Ombeni Allah hali ya kuwa na yakini ya kujibiwa, na mjue kwamba Allah hakubali dua kutoka kwa moyo ulioghafilika.”

0712 690811

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *