TANZANIA imesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utaongeza kasi ya kufikiwa kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs) kwa kuyajumuisha kikamilifu katika mipango ya maendeleo ya muda mfupi, wa kati na wa muda mrefu.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo alipohutubia Mdahalo Mkuu wa Jukwaa la Kisiasa la Ngazi ya Juu la Umoja wa Mataifa kuhusu Maendeleo Endelevu (High-Level Political Forum – HLPF) unaoendelea New York, Marekani.
Akiwasilisha tamko la Tanzania katika mdahalo huo, Prof. Mkumbo amesema licha ya changamoto zinazoikabili dunia, ikiwemo mabadiliko ya tabianchi, misukosuko ya uchumi na migogoro ya kikanda, Tanzania imeendelea kupiga hatua katika utekelezaji wa SDGs.
Ametaja mafanikio hayo kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi na huduma za usafi wa mazingira, kuboreshwa kwa huduma za afya, kupanuka kwa fursa za elimu bora, kuimarika kwa upatikanaji wa umeme, kuharakishwa kwa mageuzi ya kidijitali, kuongezeka kwa uwekezaji katika miundombinu ya kimkakati pamoja na kuimarishwa kwa uhamasishaji wa rasilimali za ndani na uwezo wa taasisi za umma.
Prof. Mkumbo ameeleza kuwa Tanzania inaichukulia Ajenda 2030 kama sehemu ya safari yake ya maendeleo ya muda mrefu, ambapo utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 utaenda sambamba na Mpango wa Nne wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano (FYDP IV), hatua itakayoweka msingi wa kuendeleza utekelezaji wa SDGs hata baada ya mwaka 2030.
Amebainisha kuwa vipaumbele vya Serikali katika kipindi kijacho vitajikita katika kuendeleza kilimo cha kisasa, maendeleo ya viwanda, uchumi wa buluu, kuimarisha ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, kuharakisha mageuzi ya kidijitali, kuendeleza rasilimali watu na kuongeza uhamasishaji wa rasilimali za ndani ili kuchochea ukuaji jumuishi na endelevu.
Aidha, Prof. Mkumbo amesisitiza kuwa mafanikio ya Ajenda 2030 yanahitaji ushirikiano madhubuti wa kimataifa, akieleza kuwa nchi nyingi zinazoendelea bado zinakabiliwa na changamoto ya nakisi ya fedha inayopunguza kasi ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Kutokana na hali hiyo, ametoa wito kwa jumuiya ya kimataifa kutekeleza kikamilifu Azimio la Kisiasa la Umoja wa Mataifa la mwaka 2023 na kuunga mkono mpango wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa SDG Stimulus.SOMA: Dira ya Maendeleo 2050 kuwekeza rasilimaliwatu
Amesema hatua hizo zinapaswa kujumuisha kupunguza riba za mikopo, kushughulikia changamoto za madeni, kuongeza upatikanaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya miradi ya maendeleo na kuharakisha mageuzi ya mfumo wa fedha wa kimataifa ili uwe jumuishi na unaozingatia mahitaji ya nchi zinazoendelea.
Tanzania inatarajia kuwasilisha rasmi Taarifa yake ya Tatu ya Mapitio ya Hiari ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu (Third Voluntary National Review – VNR), ikiwa ni sehemu ya tathmini ya maendeleo yaliyofikiwa katika utekelezaji wa Ajenda 2030.
