Pacome hesabu zimegoma Yanga, sababu zaanikwaPacome hesabu zimegoma Yanga, sababu zaanikwa

Dar es Salaam. Majina matatu yanayozungumzwa sana kwenye Ligi Kuu ya NBC hivi sasa ni viungo washambuliaji Allan Okello wa Yanga, Clatous Chama wa Simba na Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam FC.

Makali ya watatu hao katika kufumania nyavu na kupika mabao katika siku za hivi karibuni zmefanya wawe gumzo kwa wafuatiliaji wa Ligi Kuu ambayo imebakiza raundi tano ili ifikie tamati.

Hata hivyo wakati watatu hao wakitamba, kuna majina ambayo yamekuwa hayaimbwi sana msimu huu kulinganisha na hali ilivyokuwa katika nyakati kama hii msimu uliopita.

Kupungua kwa makali ya kufumania nyavu msimu huu kwa wachezaji 11 kumefanya majina yao yasiwe midomoni mwa watu hivi sasa kulinganisha na msimu uliopita ambapo muda kama huu walikuwa miongoni mwa nyota gumzo kwenye ligi.

Kiungo wa Yanga, Pacome Zouzoua ambaye msimu uliopita alikuwa miongoni mwa waliokuwa katika kinyang’anyiro cha ufungaji bora akipachika mabao 13, anaongoza orodha ya nyota hao 10 ambao wameonekana kuyumba msimu huu.

Raia huyo wa Ivory Coast hadi sasa amepachika mabao sita tu, saba pungufu ya yale aliyoweka kimiani katika msimu wa 2024/2025.

Jonathan Sowah ambaye yupo nje ya kikosi cha Simba kwa sababu zinazotajwa kuwa za utovu wa nidhamu, msimu huu amefumania nyavu mara tatu tu tofauti na msimu uliopita ambapo alifunga mabao 13.

Mshambuliaji Mkenya wa Singida Black Stars, Elvis Rupia anafuatia katika chati ya nyota hao ambao msimu huu unaonekana kuwaendea kombo ambapo amefumania nyavu mara tatu awamu hii, wakati msimu uliopita alifunga mabao 10.

Ni wazi kwamba Rupia hatoweza kufikia idadi ya msimu uliopita kwa vile hivi sasa yuko nje ya kikosi cha Singida Black Stars kwa sababu za nje ya uwanja.

Nyota wa Azam FC, Nassoro Saadun na Zidane Sereri nao wanaonekana kuwa na upepo mbaya msimu huu kulinganisha na msimu uliopita.

Msimu huu Sereri amefunga mabao mawili wakati msimu uliopita alipachika mabao sita, huku Saadun sasa hivi ana bao moja na katika msimu wa 2024/2025 alifumania nyavu mara tisa.

Mshambuliaji wa Singida Black Stars, Offen Chikola hadi sasa hajafumania nyavu kwenye Ligi Kuu wakati msimu uliopita aliwatungua makipa mara nane.

Katika kikosi hicho cha Singida Black Stars, yupo Marouf Tchakei ambaye msimu uliopita alifunga mabao nane na sasa ana bao moja.

Mfungaji bora wa Kagera Sugar kwenye Ligi Kuu msimu uliopita, Peter Lwasa, mambo sio mazuri kwake ndani ya Pamba Jiji FC iliyomsajili katika dirisha kubwa la usajili mwaka jana kwani amefunga mabao matatu tu msimu huu.

Upepo pia unaonekana kutokuwa mzuri msimu huu kwa washambuliaji wawili wa Mashujaa FC, Japhary Kibaya na Selemani Bwenzi.

Kibaya ambaye alikuwa na mabao sita msimu jana, sasa ana mabao mawili tu na Bwenzi aliyefumania nyavu mara tano, msimu huu ameambulia patupu hadi sasa.

Nuksi ya msimu huu inaonekana kumuandama pia kiungo mshambuliaji wa Fountain Gate, Elie Mokono ambaye hajafunga bao lolote wakati msimu uliopita alipachika mabao sita.

Akizungumzia ukame wake msimu huu, Bwenzi amesema kuwa majeraha yamechangia kumfanya ashindwe kutimiza matarajio.

“Nimekuwa na changamoto ya majeraha jambo ambalo linanifanya nipate wakati mgumu kurudi katika ubora wangu.

“Bado naendelea kupambana na naamini msimu ujao utakuwa bora zaidi kwangu kwa uwezo wa mwenyezi Mungu,” amesema Bwenzi.

Kocha wa IAA FC iliyopo First League, Zulfikar Mahadi amesema kuwa ni jambo la kawaida kwa wachezaji kupoteza ubora wao huku akianika sababu.

“Kuna wachezaji wanaangushwa na mbinu za makocha wapya na wengi wanaathirika na usajili wa wachezaji wapya au kujiunga na timu ambazo haziendani na uchezaji wao.

“Pia kuna changamoto ya kushindwa kumudu mazingira mapya au majeraha lakini ni jambo la kawaida na sio geni kwenye soka,” amesema Mahadi.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *