Sababu Tanzania kuzipiku China na Kenya nchini UgandaSababu Tanzania kuzipiku China na Kenya nchini Uganda

Tanzania imeipiku China na kuwa chanzo kikubwa zaidi cha bidhaa zinazoingizwa Uganda, jambo linaloonyesha mabadiliko makubwa katika mtiririko wa biashara za kikanda yaliyochochewa zaidi na ongezeko kubwa la uagizaji wa dhahabu na madini ya thamani.

Kitabu cha Takwimu cha Mamlaka ya Mapato Uganda (URA) cha mwaka 2024/25 kilichochapishwa Machi mwaka huu kinaonyesha kuwa Uganda iliagiza bidhaa zenye thamani ya Shilingi za Uganda 56.8 trilioni katika mwaka wa fedha ulioishia Juni 2025.

Kati ya kiasi hicho, Tanzania pekee ilichangia bidhaa zenye thamani ya Sh12.46 trilioni sawa na asilimia 21.94 ya bidhaa zote zilizoagizwa, hivyo kuwa chanzo kikubwa zaidi cha bidhaa zinazoingia Uganda mbele ya China, India, Falme za Kiarabu (UAE) na Kenya. Mabadiliko hayo ni makubwa ikizingatiwa kuwa miaka minne iliyopita Tanzania ilikuwa nyuma ya China, India, UAE na Kenya.

Kupaa kwa kasi kwa Tanzania

Takwimu zinaonyesha kuwa bidhaa zilizoagizwa Uganda kutoka Tanzania ziliongezeka kutoka Sh1.12 trilioni Juni 2022 hadi Sh12.46 trilioni Juni 2025, sawa na ukuaji wa takribani asilimia 1,017 ndani ya miaka minne, kiwango ambacho ni kikubwa zaidi miongoni mwa washirika wakuu wa biashara wa Uganda.

Kwa kulinganisha, bidhaa kutoka China zimeongezeka kutoka Sh6.45 trilioni hadi Sh10.92 trilioni katika kipindi hicho, sawa na ukuaji wa asilimia 69, huku bidhaa kutoka Kenya zikiongezeka kutoka Sh2.49 trilioni hadi Sh4.39 trilioni, sawa na ukuaji wa asilimia 76.

Takwimu za URA pia zinaonyesha kuwa bidhaa kutoka India zimeongezeka kutoka Sh4.12 trilioni hadi Sh5.48 trilioni ndani ya miaka minne, sawa na ongezeko la asilimia 33, huku bidhaa kutoka UAE zikiongezeka kutoka Sh3.82 trilioni hadi Sh4.58 trilioni, sawa na asilimia 20.

Takwimu hizo zinaonyesha kuwa Tanzania haijaipiku China pekee, bali pia imeongeza pengo dhidi ya washirika wa jadi wa biashara wa Uganda.

Mgawanyo wa bidhaa zinazoingizwa Uganda

Kati ya bidhaa zote zenye thamani ya Sh56.83 trilioni zilizoingizwa Uganda katika mwaka wa fedha 2024/25, nchi tano za juu zilichangia takribani theluthi mbili sawa na asilimia 66.5.

Tanzania pekee ilichangia karibu asilimia 21.9, ikifuatiwa na China yenye asilimia 19.2, huku India ikichangia asilimia 9.6. UAE ilichangia asilimia 8.1 na Kenya ikifunga orodha ya vyanzo vikubwa vya bidhaa kwa asilimia 7.7.

Kwa thamani halisi, Tanzania iliongoza kwa bidhaa zenye thamani ya Sh12.46 trilioni, ikifuatiwa na China yenye Sh10.92 trilioni, India Sh5.48 trilioni, UAE Sh4.58 trilioni na Kenya Sh4.39 trilioni. Afrika Kusini ilifuata kwa karibu ikiwa na bidhaa zenye thamani ya Sh3.28 trilioni.

Takwimu hizo zinaonyesha mabadiliko makubwa katika muundo wa bidhaa zinazoingizwa Uganda, huku nchi za Afrika, hasa Tanzania, zikizidi kutawala biashara ya kikanda.

Sababu ya dhahabu

Mkurugenzi wa Utafiti wa Benki Kuu ya Uganda, Adam Mugume, alisema sehemu kubwa ya bidhaa zinazoingia kutoka Tanzania ni dhahabu na madini ya thamani.

Kwa mujibu wa Mugume, bidhaa nyingi zinazoagizwa kutoka Tanzania ni dhahabu, jambo linaloeleza thamani ya takribani Sh12.46 trilioni iliyorekodiwa katika takwimu za biashara.

Mbali na dhahabu, alisema bidhaa nyingine zinazoingizwa kutoka Tanzania, zikiwamo mchele na bidhaa nyingine, zina thamani ya kati ya dola milioni 100 hadi 150 pekee.

Kitabu cha takwimu cha URA kinaunga mkono maelezo hayo, huku kikionyesha kuwa bidhaa za madini ya thamani na vito vya mapambo ziliongezeka kutoka Sh4.22 bilioni tu katika mwaka wa fedha 2021/22 hadi Sh16.65 trilioni mwaka 2025.

Hii ina maana kuwa bidhaa za kundi hilo ziliongezeka karibu mara 4,000 ndani ya miaka minne. Bidhaa hiyo pekee ilichangia karibu asilimia 29 ya bidhaa zote zilizoingizwa Uganda katika mwaka wa fedha 2024/25.

Kwa kulinganisha, nafaka kama mahindi, mchele na ngano, ambazo pia ni kundi kubwa la bidhaa za biashara ya kikanda, zilikuwa na thamani ya Sh4.72 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/25.

Hivyo, kundi la madini ya thamani limekuwa bidhaa kubwa zaidi inayoingizwa Uganda kwa tofauti kubwa sana.

Kitendawili cha biashara ya dhahabu

Takwimu za URA pia zinaonyesha mwenendo mwingine wa kuvutia. Wakati Uganda iliagiza madini ya thamani na vito vya mapambo vyenye thamani ya Sh16.65 trilioni katika mwaka wa fedha 2024/25, nchi hiyo pia ilisafirisha nje bidhaa hizo zenye thamani ya Sh15.82 trilioni katika kipindi hicho hicho.

Hali hiyo inaonyesha kuongezeka kwa nafasi ya Uganda kama kitovu cha biashara na usafishaji wa dhahabu katika ukanda huu, ambapo dhahabu huingizwa kutoka nchi jirani kama Tanzania na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kabla ya kusafishwa, kuchakatwa na kuuzwa tena nje.

Thamani ya bidhaa za madini ya thamani na vito vya mapambo zilizosafirishwa nje pia imeongezeka kwa kasi kutoka Sh18.66 bilioni Juni 2022 hadi Sh15.82 trilioni Juni 2025.

Kahawa, chai na viungo vya chakula vimeendelea kuwa kundi la pili kwa ukubwa la bidhaa zinazouzwa nje ya Uganda, zikiwa na thamani ya Sh7.63 trilioni.

Kenya yapoteza nafasi

Kenya, ambayo kihistoria ilikuwa moja ya washirika wakubwa wa biashara wa Uganda, imeendelea kupoteza nafasi dhidi ya Tanzania.

Katika mwaka wa fedha 2021/22, Uganda iliagiza bidhaa zenye thamani ya Sh2.49 trilioni kutoka Kenya, zaidi ya mara mbili ya bidhaa za Tanzania zilizokuwa Sh1.12 trilioni.

Hata hivyo, kufikia Juni 2024, Tanzania tayari ilikuwa imeipita Kenya kwa bidhaa zenye thamani ya Sh8.03 trilioni dhidi ya Sh2.88 trilioni za Kenya.

Pengo hilo liliongezeka zaidi katika mwaka wa fedha 2024/25 ambapo Tanzania ilisafirisha bidhaa zenye thamani ya Sh12.46 trilioni kwenda Uganda ikilinganishwa na Sh4.39 trilioni za Kenya.

Hii ina maana kuwa kufikia Juni 2025, Tanzania ilisafirisha bidhaa karibu mara tatu zaidi kwenda Uganda kuliko Kenya.

Hata DRC, ambayo kwa kawaida huonekana zaidi kama soko la bidhaa za Uganda, ilirekodi ongezeko kubwa la bidhaa zinazoingia Uganda, zikiongezeka kutoka Sh44.6 bilioni Juni 2022 hadi Sh2.18 trilioni Juni 2025.

Afrika kuwa chanzo kikuu cha bidhaa

Takwimu pana za kikanda zinaonyesha kuwa Afrika kwa kasi inakuwa chanzo muhimu zaidi cha bidhaa zinazoingizwa Uganda.

Kitabu cha takwimu cha URA kinaonyesha kuwa bidhaa kutoka Afrika ziliongezeka kutoka Sh5.11 trilioni hadi Sh30.68 trilioni ndani ya miaka minne hadi Juni 2025.

Hii ina maana kuwa bidhaa kutoka Afrika zimeongezeka mara sita ndani ya miaka minne pekee.

Ukuaji huo unaendana na kuongezeka kwa biashara ya madini, ushirikiano wa kikanda chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA), pamoja na kuongezeka kwa njia za biashara kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Hata hivyo, China bado ni muuzaji muhimu kwa Uganda, hasa katika bidhaa za viwandani, mashine, vifaa vya elektroniki, vifaa vya viwanda, nguo na vifaa vya ujenzi.

Lakini kupaa kwa Tanzania kunaonyesha namna biashara ya bidhaa, hasa dhahabu, inavyobadilisha takwimu za uagizaji bidhaa na mwenendo wa biashara za kikanda.

Ukuaji mkubwa wa biashara

Takwimu za URA zinaonyesha kuwa bidhaa zilizoingizwa Uganda ziliongezeka hadi Sh56.83 trilioni sambamba na ukuaji wa mauzo ya nje, ambayo ndani ya miaka minne iliyochunguzwa yameongezeka kutoka Sh13.16 trilioni hadi Sh40.33 trilioni.

Kwa ujumla, biashara ya Uganda karibu imeongezeka mara mbili kutoka Sh45.27 trilioni hadi Sh97.16 trilioni.

URA imeeleza kuwa ukuaji huo umetokana na kuongezeka kwa kiwango cha biashara, kuimarika kwa ushirikiano wa kikanda na kuongezeka kwa ushiriki katika biashara ya kimataifa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *