
ARUSHA: TANZANIA imejiandaa kutekeleza kwa zaidi ya miradi 60 yenye thamani ya Dola za Kimarekani bilioni 2.85 sawa na zaidi ya Sh trilioni 7 hadi 8 kupitia sekta mbalimbali za utalii, uvuvi, uchumi wa buluu, miundombinu na sekta nyinginezo.
Hayo yamesemwa leo Jijini Arusha na Mkurugenzi Mkuu Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi(TISEZA) ,Gilead Teri wakati akizungumza na wanahabari juu ya mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji unaotarajia kufanyika Juni 1-2 Jijini Arusha ambapo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo ataufungua Juni mosi mwaka huu.
Amesema miradi hiyo 60 thamani ya fedha hizo imefanyiwa utafiti wa kina na huku akisema mkutano huo si wa mazungumzo bali ni mkutano wa biashara kwani Tanzania imejiandaa kwa miradi hiyo zaidi ya 60 ili kuibua fursa mbalimbali za uwekzaji kutokana na mazingira wenzeshi ya uwekaji yaliyowekwa na serikali ya awamu ya sita.
Amesema mkutano huo wa kwanza unafanyika kwa ushirikiano na Taasisi ya Utafiti wa Masuala ya Kiuchumi na Kijamii(ESRF) na UNDP na kuongeza kuwa taasisi mbalimbali za fedha zaidi ya 20 hadi 25 zimealikwa kuja kujionea miradi hiyo na kuchambua ili kufanya uwekezaji kutoka mataifa mbalimbali nje ya nchi ili kuchambua miradi hiyo na kuwekeza.
Naye, John Rutere kutoka ambaye ni Mwakilishi Mkazi Mwandamizi wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Mpango wa Maendeleo (UNDP),ameipongeza Tanzania kuchukua hatua ya kutafuta miradi mbalimbali ya uwekaji badala ya kungojea nchi za nje kutoa fedha za maendeleo hivyo kupitia miradi hiyo ni hatua muhimu kwa uwekezaji ili kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini Tanzania na kujenga uhusiano imara kati ya wawekezaji, watunga sera, taasisi za kifedha, waendelezaji wa miradi pamoja na wadau wa maendeleo.
“UNDP inaipongeza Tanzania kwa hatua hii hata wawekezaji wakitoa fedha tutahakikisha watanzania wa kawaida wanapata manufaa na huu ni mkutano utakaotoa taswira nzuri kwa manufaa ya badae katika kuhakikisha nchi hii inajitegemea zaidi kupitia miradi mbalimbali ya uwekezaji ”
Huku Profesa Fortunata Makene ambaye ni Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Uchumi na Kijamii(ESRF) alisema umoja huo unamanufaa zaidi katika kuwezesha suluhisho halisi za uwekezaji, ushirikiano wa kweli na fursa za maendeleo.
