KIGOMA: SERIKALI mkoani Kigoma imeahidi kutatua changamoto zisizo za kikodi zinazowakabili wafanyabiashara na wasafirishaji wa malighafi ya kutengeneza saruji (Clinker) kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kupitia Bandari ya Kigoma kuelekea Rwanda.
Ahadi hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Kigoma, Hassan Rugwa, baada ya kupokea ujumbe wa wafanyabiashara kutoka Rwanda ulioongozwa na Habib Kambanga, ambao uliwasilisha maombi ya kufanyika maboresho katika eneo la maegesho ya magari, kupunguzwa kwa vizuizi vya barabarani pamoja na kuondolewa kwa vikwazo visivyo vya kikodi.

Rugwa amesema baada ya kupokea maombi hayo, amezielekeza mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kushughulikia changamoto hizo, ikiwemo kuboresha eneo la maegesho kwa kuweka miundombinu muhimu sambamba na kutatua changamoto za vizuizi vilivyopo barabarani.

Awali, Balozi Kambanga alisema kuwa maboresho hayo yakitekelezwa kwa wakati yataimarisha mazingira ya biashara na usafirishaji katika ushoroba wa Kigoma na Rusumo mkoani Kagera, akieleza kuwa vikwazo vilivyopo kwa sasa vinapunguza kasi ya uzalishaji kutokana na malighafi hiyo kuchelewa kufika viwandani.

Kwa upande wake, Meneja wa Bandari za Ziwa Tanganyika kutoka Tanzania Ports Authority, Edward Mabula, amesema wamepokea mapendekezo ya wadau hao na wanaendelea kuyafanyia kazi, ikiwemo kuangalia uwezekano wa kutenga na kujenga eneo la muda kwa ajili ya maegesho ya magari katika Bandari ya Nchi Kavu ya Katosho iliyopo Manispaa ya Kigoma Ujiji.
