Mradi waboresha huduma ya maji HanangMradi waboresha huduma ya maji Hanang

MANYARA: Wananchi wa Wilaya ya Hanang mkoani Manyara wameendelea kunufaika na huduma za maji safi, vyoo bora pamoja na elimu ya usafi wa mazingira na usafi binafsi baada ya Shirika la WaterAid Tanzania kukabidhi rasmi mradi wa WASH katika Shule ya Msingi ya Gidamula iliyopo Hanang mkoani Manyara kwa serikali.

‎Makabidhiano hayo yamefanyika Mei 28, 2026 katika shule hiyo, ambapo mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Mbulu, Michael Semindu aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Queen Sendiga.



‎Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Programu wa WaterAid Tanzania, Beda Levira, ambaye alimwakilisha Mkurugenzi wa shirika hilo Anna Mzinga, amesema mradi huo utasaidia wanafunzi pamoja na jamii ya eneo hilo waliokuwa wakikabiliwa na changamoto ya ukosefu wa maji safi na salama.

‎Amesema shirika hilo litaendelea kushirikiana na serikali katika kuanzisha na kuendeleza miradi ya maji kwa ajili ya kuwahudumia wananchi na kuboresha afya pamoja na mazingira ya kujifunzia kwa wanafunzi.



‎Kwa upande wake, mgeni rasmi Michael Semindu amepongeza shirika la WaterAid Tanzania kwa kuendelea kuwa msaada mkubwa kwa serikali katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za kijamii, hususan sekta ya maji, afya na usafi wa mazingira.

‎”Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo wanaojitokeza kusaidia jamii. Nawahimiza wananchi kuitunza miundombinu hii ili iweze kudumu na kuwanufaisha kizazi cha sasa na kijacho,” amesisitiza Semindu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *