KAGERA: Wananchi wanaojishughulisha na kilimo cha mazao katika Tarafa ya Rulenge, wilayani Ngara mkoani Kagera, kwa pamoja wameanzisha Chama cha Msingi Rulenge (AMCOs) ambacho kitawasaidia kukusanya mazao yao na kufuatilia bei nzuri za masoko kwa ajili ya kuuza kwa pamoja mazao ya kahawa, maharage, mahindi, parachichi na alizeti.
Mwenyekiti wa bodi ya uanzishwaji wa chama hicho cha msingi, Mhandisi Deusderthi Kakoko, alisema kuwa kwa miaka mingi wananchi wa vijiji 23 vinavyounda Tarafa ya Rulenge wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya kukosa masoko ya uhakika ya mazao yao, hususan mahindi na maharage, huku zao la kahawa likihudumiwa na chama kimoja cha msingi kilichoko makao makuu ya Wilaya ya Ngara kinachojulikana kama Ngara Farmers.
Alisema maamuzi hayo ya pamoja yamepitia michakato mbalimbali ya kutafuta mabadiliko ya kilimo, ikiwemo kuanzisha programu maalumu ya kujenga uelewa kwa wakulima kuhusu kilimo bora mseto kinachohusisha mazao hayo matano yanayostawi kwa wingi katika vijiji hivyo. Aidha, programu hiyo inahusisha elimu ya kupima rutuba ya udongo ili kutambua changamoto zilizopo, elimu ya mbegu bora, pamoja na kuimarisha umoja wa wakulima ili kuuza mazao kwa pamoja na kupata msaada wa kilimo kutoka serikalini.

Alisema utafiti uliofanyika na wataalamu mbalimbali wa kilimo na ardhi kwa mwaka 2024/2025 ulibaini kuwa baadhi ya wakulima wanamiliki mashamba lakini hawajui idadi sahihi ya miche inayopaswa kupandwa, huku wengine wakizalisha kwa wingi lakini wanatapeliwa na wafanyabiashara wachache wenye tamaa wanaonunua mazao yao kwa bei ya chini.
“Tumeendelea kufarijika na hatua ya serikali ya kupandisha bei ya kahawa, lakini wilaya yetu ilikuwa na chama kimoja cha msingi ambacho huduma zake hazikuwafikia wananchi ipasavyo. Hali hiyo imewafanya wananchi kuamua kuanzisha chama chao cha msingi ili kupata suluhisho la pamoja na kuinua uchumi wao,” alisema Kakoko.

Alisema changamoto nyingine zinazowakabili wakulima wa Tarafa hiyo ni pamoja na kutokuwepo kwa duka la pembejeo, matumizi yasiyo sahihi ya mbolea, pamoja na elimu ndogo kuhusu kilimo bora cha mazao yanayoshindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi. Alisema AMCOs imeanzishwa ili kutatua changamoto hizo.
Alieleza kuwa hadi sasa ofisi za chama hicho zimefunguliwa na wananchi wameanza kujisajili kujiunga na ushirika huo. Aidha, bodi iliyochaguliwa imeajiri maafisa ugani wa muda ambao tayari wameanza kuwafikia wakulima mmoja mmoja kutoa elimu ya kilimo, utambuzi wa magonjwa ya mazao, na uelewa wa dhana ya ushirika.
Uzinduzi wa chama hicho cha msingi umepokelewa kwa furaha na wakulima mbalimbali wa Tarafa ya Rulenge ambao wamesema ununuzi wa mazao kwa muda mrefu umekuwa ukihusisha madalali wengi, hali inayosababisha baadhi ya wakulima kutapeliwa au kulipwa bei ndogo bila ushahidi wa maandishi.

Mmoja wa wakulima, Agustin Karoli Bisesele, mkazi wa Rulenge anayejishughulisha na kilimo cha kahawa na mahindi, alisema changamoto ya kukosa elimu ya ushirika imekuwa kubwa kwa miaka mingi, lakini sasa wanaona matumaini kupitia AMCOs itakayowawezesha kuungana na kutafuta masoko kwa pamoja.
Kwa upande wake, Onesmo Machumi Kakoko, mkulima wa kahawa, mahindi na maharage, alisema amekuwa akiuza mazao yake kupitia chama cha msingi cha Ngara Farmers, lakini umbali na upatikanaji mdogo wa maafisa ugani umeathiri upatikanaji wa elimu ya kilimo bora. Alisema kuwa kuwepo kwa kituo hicho karibu na wakulima kutasaidia kuongeza ubora na uzalishaji wa mazao.
Mkuu wa Idara ya Kilimo, Umwagiliaji na Ushirika wilayani Ngara alisema kuanzishwa kwa chama hicho cha msingi kutarahisisha upatikanaji wa huduma kwa wakulima na kuongeza uzalishaji wa kahawa hadi kufikia tani 30,000, ambazo wilaya inalenga kuzalisha kama zao la kimkakati, sambamba na kuongeza uzalishaji wa mazao mengine kupitia mfumo wa umoja wa wakulima.
Alisema moja ya faida kubwa ya ushirika ni serikali kusogeza huduma za pembejeo, mbegu bora, huduma za ugani na ushauri wa kilimo karibu na wakulima, hatua itakayochochea mabadiliko makubwa ya kilimo katika ukanda huo na vijiji jirani.
Alitoa wito kwa wakulima kufuata misingi ya ushirika na kujiunga kwa wingi ili waweze kunufaika kwa pamoja katika safari ya kuboresha maisha yao na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa kupitia mazao yao.
