DAR ES SALAAM: SERIKALI imesema itaendelea kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa huduma za usafiri wa mtandao huku ikisisitiza kuwa sekta hiyo imekuwa mhimili muhimu wa ukuaji wa uchumi, ajira kwa vijana na maendeleo ya huduma za kidijiti nchini.
Kauli hiyo imetolewa leo Dar es Salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Usafiri kwa njia ya Barabara Wizara ya Uchukuzi, Andrew Magombana, wakati akizungumza katika kongamano la wadau wa usafiri mtandao lililoandaliwa na Kampuni ya Mwananchi (MCL) kwa kushirikiana na Bolt Tanzania.
Magombana alisema sekta ya uchukuzi ina mchango mkubwa katika shughuli za kijamii na kiuchumi kwa kuwawezesha wananchi kufika maeneo mbalimbali kwa urahisi na kwa wakati.
“Sekta ya uchukuzi ni sawa na mishipa ya damu katika mwili wa binadamu kwa sababu inasaidia wananchi kufika kazini, kufanya biashara, kupata elimu na huduma nyingine muhimu. Hivyo ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa,” alisema Magombana.
Alisema ukuaji wa huduma za usafiri wa kidigiti umechochewa na uwekezaji mkubwa unaofanywa na serikali katika miundombinu ya kisasa ikiwemo barabara, Reli ya Kisasa ya SGR pamoja na mabasi ya mwendokasi.

Kwa mujibu wa Magombana, maendeleo hayo yamefungua fursa mpya kwa kampuni za usafiri wa mtandao kupanua huduma zao huku wananchi wakinufaika na urahisi wa usafiri pamoja na kupungua kwa muda wa kupotea kwenye foleni.
Aidha, alisema sekta hiyo imeendelea kuwa chanzo kikubwa cha ajira kwa vijana kupitia shughuli za udereva, uwekezaji wa magari pamoja na huduma nyingine zinazohusiana na teknolojia ya usafiri.
Alisema serikali pia inaendelea kuhimiza matumizi ya nishati safi ikiwemo gesi asilia (CNG) na magari ya umeme ili kupunguza gharama za usafiri na kulinda mazingira.
Kwa upande wake, Meneja Mwandamizi Bolt Afrika Mashariki, Demetrius Kanyankole, alisema majukwaa ya usafiri wa kidigiti yanaendelea kubadilisha mfumo wa usafiri mijini huku yakichochea ajira na ukuaji wa uchumi.
Alisema Bolt kwa sasa inafanya kazi katika zaidi ya miji minane nchini na kushirikiana na zaidi ya madereva zaidi ya 4000 ambao wanaotoa huduma kwa mamilioni ya abiria.
“Huduma hizi pia zinasaidia kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi, leseni na mifumo ya malipo ya kidijitali huku zikiboresha uwazi na usalama kwa kuwa kila safari inarekodiwa,” alisema Kanyankole.
Naye Mtendaji Mkuu wa Sahara Ventures, Jumanne Mtambalike, alisema Tanzania inapaswa kuendelea kukumbatia ubunifu na teknolojia ili kuongeza ajira kwa vijana na kukuza uchumi wa kidijitali.
Alisema mageuzi ya kidijitali yanafungua fursa kubwa siyo tu katika usafiri wa abiria, bali pia usafirishaji wa mizigo, biashara mtandao na huduma za kifedha.
