Kombe la Dunia lapangua mechi tatu Ligi Kuu BaraKombe la Dunia lapangua mechi tatu Ligi Kuu Bara

BODI ya Ligi Kuu Tanzania (TPLB), imetangaza kufanya mabadiliko ya muda kwa mechi tatu za Ligi Kuu Bara msimu huu ili kutoingiliana na zile za Fainali za Kombe la Dunia 2026.

Uamuzi huo umefanyika kutokana na kwamba, Ligi Kuu Bara itaendelea kuchezwa hadi Juni 30, 2026, huku Fainali za Kombe la Dunia 2026 michezo yake ikitarajiwa kuanza Juni 11, 2026 hadi Julai 19, 2026.

Taarifa ya TPLB iliyotolewa leo Mei 29, 2026, imesema: “Bodi ya Ligi Kuu Tanzania imefanya mabadiliko ya muda kwa michezo mitatu (3) ya Ligi Kuu ya NBC ili kutoingiliana na fainali za Kombe la Dunia zitakazofanyika katika nchi za Marekani, Mexico na Canada kuanzia Juni 11, 2026.

“Michezo iliyofanyiwa mabadiliko ni ile iliyokuwa inaingiliana na michezo ya Kombe la Dunia iliyokuwa ichezwe saa 1 na saa 3 usiku.

“Bodi ya Ligi imezingatia tofauti ya saa kati ya nchi hizo na Tanzania, jambo ambalo litasaidia kuepusha muingiliano kati ya mechi za Ligi na michezo ya Kombe la Dunia.

“Maboresho haya ya muda wa mchezo yamelenga kuhakikisha kuwa hakuna athari kwa klabu, wadhamini, wadau wa matangazo pamoja na mashabiki lakini pia kuwapa nafasi wadau kufuatilia mashindano yote mawili bila changamoto ya ratiba kugongana katika kipindi cha mashindano hayo ya kimataifa.”

Katika kulitolea ufafanuzi hilo la ligi kuchelewa kumalizika, taarifa hiyo imesema: “Ratiba ya mashindano ya kimataifa kwa mwaka 2025 ilijumuisha Michuano ya Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN) pamoja na Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ikafanya Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-2026 kusogezwa mbele kwa lengo la kutoa nafasi kwa timu ya Taifa kushiriki kikamilifu katika majukumu ya kimataifa sambamba na kuzipa klabu muda wa kutosha wa maandalizi baada ya mashindano hayo.

“Awali, michuano ya CHAN ilikuwa imepangwa kufanyika Februari 2025, hata hivyo iliahirishwa na kufanyika kuanzia Agosti 2 hadi 30, 2025. Kutokana na mabadiliko hayo ya ratiba, wachezaji wengi waliokuwa katika majukumu ya timu ya Taifa walirejea kwenye klabu zao mwishoni mwa mwezi Agosti, hali iliyosababisha Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutoa muda maalumu wa mapumziko na maandalizi kabla ya kuanza rasmi kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya NBC msimu wa 2025-2026.”

Mbali na hilo, maandalizi ya AFCON pamoja na kalenda ya mashindano ya CAF yametajwa kuwa sehemu ya sababu zilizochangia upangaji mpya wa ratiba ya Ligi, kwa lengo la kuhakikisha kuwa klabu pamoja na timu ya Taifa zinapata mazingira bora ya ushindani bila kuathiri ubora na mwenendo wa mashindano ya ndani.

“Msimu wa 2025-2026 ulianza rasmi kwa mchezo wa Ngao ya Jamii uliofanyika Septemba 16, 2025 kabla ya Ligi Kuu ya NBC kuanza Septemba 17, 2025. Tangu kuanza kwa msimu huu, ligi imeendelea kwa ushindani mkubwa huku klabu zikionesha kiwango kizuri na mashabiki kuendelea kupata burudani ya hali ya juu katika viwanja mbalimbali nchini,” imefafanua taarifa hiyo.

Kwa mujibu wa ratiba ilivyo na mabadiliko hayo ya muda, kuna mechi tatu zinazokumbana na hali hiyo ambazo ni Coastal Union vs Namungo iliyopangea kuchezwa Juni 12, 2026 saa 3:00 usiku kwa muda wa awali, Simba vs Pamba Jiji (Juni 14 saa 1:00 usiku) na JKT vs Tanzania Prisons (Juni 18 saa 1:00 usiku).

Kwa upande wa Fainali za Kombe la Dunia, mechi tatu zinazoingiliana na zile za Ligi Kuu Bara ni ya Juni 12 kati ya Canada dhidi ya Bosnia and Herzegovina itakayoanza saa 4:00 usiku, Ujerumani vs Curacao (Juni 14 saa 2:00 usiku) na Czechia vs Afrika Kusini (Juni 18 saa 1:00 usiku).

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *