Dar es Salaam. Mbunge wa Kigoma Mjini ambaye ni mwanamuziki wa Bongo Fleva, Clayton Chipando maarufu kama Baba Levo, amesema bado anaiona tasnia ya muziki kuwa sehemu kubwa ya maisha yake licha ya kuingia kwenye siasa kwa kuwawakilisha wananchi bungeni. 

Msanii huyo ambaye aliwahi kutamba na nyimbo kama ‘Amen’, ‘Amapiano’ na nyinginezo, alisema nafasi yake ya ubunge imekuwa daraja muhimu la kuwasemea wasanii moja kwa moja serikalini.

Akizungumza katika mahojiano maalumu na Mwananchi, Baba Levo alisema moja ya vitu anavyojivunia ni uwezo wake wa kuielewa sanaa kwa undani kutokana na maisha aliyopitia kwenye muziki kabla ya kuwa mbunge. Kwa mujibu wake, changamoto nyingi zinazowakabili wasanii zinaweza kutatuliwa kwa haraka iwapo zitafikishwa kwenye mamlaka husika kwa njia sahihi.

“Moja kati ya kazi yangu ni kutetea wasanii wote. Kwa sababu najua sanaa ilivyo, kama kuna kitu kinaenda vibaya nina nafasi ya kukisema bungeni na kinawasilisha moja kwa moja kwa wahusika,” alisema Baba Levo.

Mbunge huyo alisema bado ana mapenzi makubwa na muziki na hawezi kuuacha kabisa kwa sababu ni kipaji kilichomtoa mbali. Hata hivyo, amekiri kuwa majukumu ya ubunge yamepunguza muda wake wa kufanya kazi za muziki kama zamani alipokuwa akitoa nyimbo mara kwa mara na kufanya show sehemu mbalimbali nchini.

Baba Levo ambaye aliwahi kuwa karibu sana na lebo ya WCB Wasafi, alisema mashabiki wake wanapaswa kutarajia kazi mpya kubwa aliyomshirikisha Diamond Platnumz. Alisema kolabo hiyo itakuwa moja ya kazi kubwa kutokana na ukubwa wa jina la Diamond kwenye muziki wa Afrika.

“Kutomshirikisha Diamond haiwezekani. Kuna watu wanatumia mamilioni kumtafuta, mimi nina nafasi ya kufanya naye bure, kwa hiyo nina wimbo naye na utakuwa mkubwa sana,” alisema.

Katika mahojiano hayo, Baba Levo pia alizungumzia namna maisha yake yalivyobadilika baada ya kuwa mbunge wa Kigoma Mjini. Anasema zamani alikuwa akifanya mambo mengi kama msanii wa kawaida bila kuangaliwa sana. Lakini sasa kila hatua anayopiga inatazamwa kwa jicho tofauti kutokana na nafasi yake ya uongozi.

“Sasa mimi ni mbunge, si kioo cha jamii kwa hiari bali kwa wajibu. Kila kitu unachofanya kinaangaliwa kwa jicho tofauti,” alisema.

Baba Levo alifunguka kuhusu wasanii wanaotamani kuingia kwenye siasa, akisema wengi wao wana uwezo mkubwa wa kuwa viongozi kwa sababu tayari wana ushawishi mkubwa kwa jamii. Hata hivyo, anasema safari ya kupata nafasi ndani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) si rahisi kama watu wengi wanavyodhani.

“Mchakato ni mgumu sana. CCM ina wanachama wengi sana na kupata nafasi si rahisi kama watu wanavyodhani,” alisema.

Kwa upande mwingine, anasema anaamini wasanii wengi wana uwezo wa kuwa viongozi wazuri iwapo wataamua kuwa na nidhamu, uvumilivu na kujituma kwa dhati.

“Asilimia kubwa ya wasanii wana uwezo wa kuwa viongozi wazuri, wanachotakiwa ni nidhamu na kupambana bila kukata tamaa,” anasema.

Akizungumzia mahusiano yake na mastaa wengine wa muziki, Baba Levo alisema zaidi ya asilimia 90 ya wasanii wanamuunga mkono kwenye shughuli zake za kijamii na maendeleo. 
Alitaja majina ya Nandy, Billnass, Diamond Platnumz na Zuchu kuwa wamekuwa karibu naye kwenye miradi mbalimbali ikiwamo michango ya madawati na kusaidia jamii.

Baba Levo pia alikumbuka maisha yake ya zamani kwenye muziki na kusema hajawahi kujutia chochote alichowahi kufanya akiwa msanii. Alisema kila hatua aliyopita ilikuwa sehemu ya safari ya maisha iliyomjenga mpaka kufikia hapo alipo leo.

“Hizo zilikuwa stegi za maisha za kutafuta maisha na kujijenga,” alisema.

Kuhusu wachambuzi wa muziki na wadau wa burudani mitandaoni, alisema wana nafasi kubwa ya kuijenga sanaa iwapo watafanya kazi kwa haki na weledi. Ameonya kuwa baadhi yao wanapopendelea au kushawishiwa kwa fedha wanaweza kuharibu tasnia na kuua vipaji vya wasanii chipukizi.

Mbali na muziki na siasa, Baba Levo alisema kwa sasa ameanza rasmi safari yake ya elimu katika kituo cha Brothers Education ambapo anajiandaa kufanya mtihani wa QT kabla ya kuendelea na masomo ya sekondari hadi chuo kikuu. Amesisitiza  elimu ni jambo muhimu kwa kiongozi yeyote kwa sababu humsaidia kuwa na upeo mpana wa kufikiri na kufanya maamuzi sahihi.

Akizungumzia mjadala wa “uchawa” Baba Levo alisema kwake anaiona kama aina ya influence au upambe ambao si tatizo iwapo mtu hafanyi kwa kuvuka mipaka ya utu wake.

“Tatizo linakuja pale mtu anapovuka mipaka ya utu wake,” alisema.

Akimalizia msanii huyo anasema ofisi yake ya Kigoma Mjini iko wazi kwa wananchi wote na ataendelea kutumia nafasi yake kuwaunganisha wananchi na viongozi wa kitaifa ili kuhakikisha changamoto zao zinapatiwa ufumbuzi kwa haraka.

Anasema dhamira yake ni kuona wasanii, vijana na wananchi wa kawaida wanapata nafasi ya kusikilizwa na kufikiwa na maendeleo kupitia uongozi wake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *