
Mahakama Kuu ya Kenya imesitisha kwa muda kuanzishwa kwa kituo cha Karantini kwa wagonjwa wa Ebola raia wa Marekani, kilichotarajiwa kujengwa nchini humo. Kufuatia uamuzi huo, wakuu wa Marekani wamedai kuwa watashughulikia hofu ya Wakenya kuhusiana na kituo hicho.
Taarifa ya Jumamosi kutoka Ofisi ya Jeremy P. Lewin, Naibu Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Misaada wa Kigeni, ilisema: “Tumejulishwa kuhusu hatua ya mahakama nchini Kenya dhidi ya kituo cha kutenga wagonjwa wa Ebola. Tunawasiliana na mamlaka za Kenya na tuna matumaini kuwa tunaweza kutatua pingamizi.”
Taarifa hiyo ni majibu ya kwanza ya hadharani kutoka Washington tangu Mahakama Kuu ya Kenya isimamishe uanzishaji au kuanza kufanya kazi kwa kituo hicho kilichopendekezwa, hadi pale shauri la kikatiba litakaposikilizwa na kuamuliwa.
Jaji Patricia Nyaundi alitoa maagizo hayo Ijumaa baada ya kundi la kutetea haki kupinga mradi huo, likisema kuwa unazua masuala ya kikatiba na ya maslahi ya umma yanayohitaji mapitio ya kimahakama.
Kituo hicho kilichopendekezwa kimeibua mjadala mkali nchini Kenya, kufuatia taarifa kwamba kitatumika kuwashguhulikia raia wa Marekani wanaoweza kuwa wameathiriwa na Ebola wakati wa mlipuko unaoendelea katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kuwa Marekani haitawaruhusu nchini humo waathirika au washukiwa wa ugonjwa wa Ebola na kwamba watatibiwa katika nchi nyingine imewakasirisha sana Wakenya wanaoona nchi yao inatumiwa kama jaa la taka na Marekani.
Wizara ya Afya ya Kenya imeutetea mpango wa kujenga kituo hicho na kusema ni sehemu ya ushirikiano wa kimataifa kuhusu kukabiliana na makongjwa kwa kuzingatia kanuni zote la afya.
Muungano wa Madaktari Kenya (KMPDU) umeitaka serikali iwe na uwazi kamili kuhusu makubaliano yoyote yanayohusiana na kituo hicho kilichopendekezwa, ukisema masuala ya afya ya umma na usalama yanapaswa kujadiliwa wazi kabla ya mpango wowote kama huo kusonga mbele.