
Waasi wa RSF wamewaua angalau raia 27, wakiwemo wazee, katika shambulio dhidi ya vijiji vilivyoko magharibi mwa Bara katika jimbo la North Kordofan nchini Sudan.
Hayo ni kwa mujibu wa shirika la misaada ya kibinadamu la Mtandao wa Madaktari wa Sudan, lenye makao yake mjini Cairo.
Taarifa ya shirika hili imesema mashambulizi hayo yalifanyika Alhamisi katika eneo la al-Murrah, na kuyataja kuwa ni “uhalifu mpya unaowalenga raia wasio na silaha katika maeneo yasiyo na uwepo wa kijeshi” wakati wa sikukuu ya Eid al-Adha.
Shirika hilo limesema mashambulizi hayo yamezidisha zaidi hali ambayo tayari ni “janga la kibinadamu” linalowakabili wananchi kutokana na vita vinavyoendelea.
Vita vya sasa vya Sudan vilianza mwezi Aprili 2023 baada ya mvutano wa muda mrefu kati ya jeshi na kundi la Rapid Support Forces (RSF). Serikali ya Sudan imesema kwamba Falme za Kiarabu (UAE) inaunga mkono waasi hao wa RSF wanaotekeleza mauaji ya kimbari nchini humo.
RSF na washirika wake wanadhibiti eneo la magharibi la Darfur pamoja na maeneo ya Kordofan yaliyo karibu na mpaka wa Sudan Kusini. Maeneo yote mawili yana utajiri wa visima vya mafuta na migodi ya dhahabu. RSF pia imekuwa ikipambana mara kwa mara na jeshi kwa ajili ya kudhibiti Bara.
Mashambulizi hayo yanakuja wakati zaidi ya asilimia 40 ya wakazi wa Sudan wanakabiliwa na njaa kali, kwa mujibu wa ripoti iliyotolewa Alhamisi na taasisi ya IPC inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa.
Ripoti hiyo ilisema karibu watu milioni 19.5 kote Sudan wanakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, huku mzozo huo ukiendelea kuchochea kile ambacho mashirika ya misaada yanakitaja kuwa moja ya majanga mabaya zaidi ya kibinadamu duniani.
Mzozo huo umeua angalau watu 59,000, umewafanya takriban milioni 13 kuyahama makazi yao, na kusukuma maeneo mengi ya nchi katika hali ya njaa. Zaidi ya watu milioni 30 wanahitaji msaada wa kibinadamu.