Dar es Salaam. Wakati dunia ikikabiliwa na upungufu wa misaada ya kimataifa katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI, Tanzania imezindua kampeni ya GGML Kilimanjaro Challenge Against HIV/AIDS 2026 yenye lengo la kukusanya dola milioni moja (takribani Sh2.6 bilioni) kuimarisha huduma za kinga.

Uzinduzi wa kampeni hiyo umefanyika leo Mei 30 jijini Dar es Salaam kupitia matembezi ya pamoja na harambee ya uchangishaji fedha katika ufukwe wa Coco Beach, ukihusisha wadau mbalimbali wa sekta binafsi, taasisi za kifedha na mashirika ya maendeleo.

Akizungumza katika hafla hiyo, Makamu wa Rais wa AngloGold Ashanti anayesimamia Ustahimilivu na Mahusiano Afrika, Simon Shayo, amesema lengo la kampeni hiyo ni kuhakikisha upatikanaji wa rasilimali endelevu kwa mapambano dhidi ya UKIMWI nchini.

Amesema kupitia Geita Gold Mining Ltd (GGML) na GGML Kili Challenge Trust, kampeni hiyo imeendelea kuwa daraja muhimu la kuchangisha fedha kwa zaidi ya miaka 24, ikihusisha wadau wa sekta binafsi na jamii kwa ujumla.

“Kila mmoja ana nafasi ya kuchangia katika mapambano haya kwa sababu bado kuna uhitaji mkubwa wa dawa, huduma na msaada kwa watu wanaoishi na VVU,” amesema Shayo.

Mwaka huu, kampeni hiyo imeingia ubia na Jukwaa la Watendaji Wakuu Tanzania (CEOrt) ili kuongeza nguvu ya uchangishaji na ushirikiano wa sekta binafsi katika kufikia lengo la Sh2.6 bilioni.

Baadhi ya wadau wanaoshiriki katika kampeni hiyo ni Stanbic Bank Tanzania, NMB Bank, NBC, Puma Energy, Heritage Insurance, Coastal Aviation, Asante Tours na Mwananchi Communications Limited.

Mratibu Mkazi wa Umoja wa Mataifa nchini Tanzania, Susan Ngongi Namondo, ameipongeza GGML kwa kuendelea kuwa mstari wa mbele katika kuchangisha rasilimali za ndani, akisema kupungua kwa misaada ya kimataifa kunahitaji suluhisho la ndani zaidi kupitia ushirikiano wa sekta mbalimbali.

Amesema mafanikio yaliyopatikana katika mapambano dhidi ya UKIMWI yamechangiwa na uwekezaji katika elimu, tiba na uhamasishaji, lakini bado kuna haja ya kuongeza nguvu ili kufikia lengo la kutokomeza maambukizi mapya ifikapo 2030.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa GGML, Ashraf Suryaningrat, amesema kampeni hiyo imejengwa katika mshikamano wa wadau wote, akisisitiza kuwa upandaji wa Mlima Kilimanjaro utakaofanyika Julai mwaka huu utakuwa sehemu muhimu ya kufanikisha lengo la uchangishaji.

Kwa upande wa sekta binafsi, Meneja Mwandamizi wa Mahusiano wa Stanbic Bank Tanzania, Dickson Senzi, amesema ushiriki wa taasisi hizo unaonyesha dhamira ya kuwekeza katika afya na maendeleo ya jamii kupitia ushirikiano wa pamoja.

Katika uzinduzi huo, ahadi zilizotolewa zilifikia zaidi ya Sh150 milioni, huku waandaaji wakisema kampeni za uchangishaji zitaendelea katika majukwaa mbalimbali hadi kufikia lengo la Sh2.6 bilioni.

Kwa zaidi ya miaka 24, GGML Kili Challenge Trust imekuwa ikiratibiwa kwa kushirikiana na TACAIDS, ikiwa ni jukwaa muhimu la kuelekeza rasilimali za sekta binafsi katika mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI nchini.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *