Brazzaville. Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Chama cha Hifadhi ya Jamii Afrika (ASSA) zimekubaliana kushirikiana kuimarisha matumizi ya mtaji wa ndani wa Afrika katika kufadhili maendeleo ya muda mrefu, ikiwamo miradi ya miundombinu na mifumo ya ulinzi wa jamii.

Makubaliano hayo yalitiwa saini Mei 28, 2026 pembeni mwa mikutano ya mwaka ya kundi la Benki ya Maendeleo ya Afrika inayoendelea mjini Brazzaville, Jamhuri Kidemokrasia ya Congo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa baada ya utiaji saini huo, ushirikiano huo unakusudia kuongeza mchango wa mifuko ya pensheni na taasisi za hifadhi ya jamii katika kuchochea uwekezaji wa maendeleo barani Afrika kupitia mtaji wa muda mrefu unaokusanywa na taasisi hizo.

Makubaliano hayo, yalisainiwa na Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sekta ya Fedha wa AfDB, Ahmed Attout, huku ASSA ikiwakilishwa na Katibu Mkuu wake, Meshach Bandawe.

Kupitia ushirikiano huo, taasisi hizo zinatarajia kushirikiana katika maeneo mbalimbali ikiwamo kubadilishana maarifa, kutoa msaada wa kitaalamu kwa wanachama, kuimarisha utawala wa uwekezaji na kutafuta fursa za uwekezaji zinazoweza kuchangia maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hatua hiyo inakuja wakati nchi nyingi za Afrika zikitafuta mbinu za kuongeza matumizi ya rasilimali za ndani kufadhili miradi ya maendeleo, sambamba na kupunguza utegemezi wa mikopo na misaada ya nje.

Makubaliano hayo pia yanaendana na Dira Mpya ya Muundo wa Kifedha wa Afrika kwa Maendeleo (NAFAD) na Makubaliano ya Abidjan, yanayosisitiza umuhimu wa kuhamasisha akiba na mitaji ya ndani kusaidia maendeleo endelevu ya Afrika.

Hivi karibuni kamati ya utendaji ya mawaziri wa sekta ya miundombinu na Nishati ya Umoja wa Afrika (AU) ulipitisha azimio la kuendelea kuipa nguvu Jumuiya ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii Afrika kuimarisha shughuli zake.

Aidha Jumuiya hiyo inatarajiwa kuzindua jukwaa la kwanza la mifuko yote ya Hifadhi ya Jamii ya Nchi za Afrika litakalofanyika 23 Julai hadi 24, 2026 Jijini Abidjan nchini Cote d Ivoire.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *