
Dar es Salaam. Tume ya Rais ya Uchunguzi wa Kijinai katika Matukio ya Ghasia za Wakati na Baada ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025, inayoongozwa na Jaji Mahakama ya Rufani, Shaban Lila, imeburutwa mahakamani ikipingwa uhalali wake.
Tume hiyo maarufu Tume ya Jaji Lila imeundwa na Rais Samia Suluhu Hassan kufuatia ripoti ya Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Uvunjifu wa Amani wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, iliyoongozwa na Jaji Mkuu mstaafu, Mohamed Chande Othman.
Wajumbe wengine wa tume hiyo ambao uteuzi wake ulitangazwa Mei 18, 2026 ni majaji wastaafu wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Gad John Mjemmas, Awadh Mohamed Bawazir na Aishieli Nelson Sumari.
Hata hivyo, siku chache tu baada ya kutangazwa kwa tume hiyo na wajumbe wake, mwanaharakati Buberwa Buberwa na mwenzake Joseph Mabugo, wakiwakilishwa na mawakili Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu, wamekwenda mahakamani kuhoji uhalali wake.
Buberwa na Mabugo wamefungua shauri hilo Mahakama Kuu Masjala Ndogo Kigoma, dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Shaban Ally Lila (mwenyekiti wa tume) na wajumbe wake watatu, Gad John Mjemmas, Awadhi Mohamed Bawazir na Aishiel Nelson Sumari.
Katika shauri hilo waombaji hao wanaomba ruhusa ya kufungua shauri la mapitio na kuiomba mahakama hiyo itengue uamuzi huo wa Rais Samia kuunda tume hiyo na uteuzi wa wajumbe wake, pamoja na amri ya kumzuia kuchukua tena hatua kama hizo.
Shauri hilo limefunguliwa chini ya hati ya dharura sana iliyothibitishwa na mawakili Mpoki na Mwasipu wakidai kama shauri hilo halitasikilizwa haraka wajibu maombi hasa mwenyekiti na wajumbe wa tume hilo wataendelea na mchakato wa uchunguzi huo, wakati hawana mamlaka hayo kikatiba na kisheria.
Katika shauri hilo waombaji hao wameikumbusha mahakama kufuatia matukio yaliyotokea wakati na baada ya uchaguzi huo, Jeshi la Polisi liliwakamata watu kadhaa maeneo mbalimbali nchini na kuwafungua kesi mbalimbali.
Wakati kesi zinaendelea Rais aliagiza baadhi ya watuhumiwa waachiwe kutokana na uzito wa ushahidi uliokuwepo.
Kisha aliunda tume ya kuchunguza matukio hayo aliyoyaita ya uvunjifu wa Amani (Tume ya Jaji Chande ambayo iliwasilisha ripoti yake Aprili 23, 2026.
Pamoja na mambo mengine katika hotuba ya kukabidhi ripoti hiyo mwenyekiti alibainisha watu 518 waliuawa na wengine kujeruhiwa huku ikitahadharisha idadi hiyo inaweza kuwa zaidi.
Rais Samia akizungumza baada ya kupokea ripoti hiyo, Aprili 23, 2026 pamoja na mambo mengine alitangaza kuunda tume nyingine ya kuchunguza vitendo vya kijinai wakati wa katika matukio hayo.
Hata hivyo, waombaji wanadai kitendo cha Rais kuunda tume kuchunguza kitu ambacho aliamuru watuhumiwa waachiwe bila mahakama kutoa uamuzi wowote kuhusu uhusika wao, inakosa mantiki kisheria na ni kitendo cha kibaguzi kinachopingana na ibara ya 13 (1) ya Katiba ya nchi.
Katika hati ya maelezo na kiapo chao cha pamoja waombaji hao wanadai kwa mujibu wa Sheria ya Tume ya Uchunguzi sura ya 32(R:E 2023) Rais hana Mamlaka ya kuunda Tume nyingine baada ya Tume ya Jaji Chande kutoa ripoti yake.
Wanabainisha kwa mujibu wa sheria hiyo kifungu cha 21(1) (a) na (b) Rais kama ataona kuna haja ya kuchunguza zaidi baada ya kusoma ripoti ya Jaji Chande anatakiwa kumuagiza Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuliagiza Jeshi la Polisi kupeleleza zaidi.
Pia wanadai mujibu wa kifungu hicho kama ripoti inajitosheleza waliotajwa wachukuliwe hatua za Kisheria.
Vilevile wanadai Rais hana Mamlaka ya kuunda Tume ya Kuchunguza Matukio ya Kijinai kwa sababu DPP ndiye mtu pekee mwenye jukumu hilo kikatiba na kisheria.
Wamesisitiza Sheria ya Huduma Mashtaka Sura ya 430 ( Marejeo ya mwaka 2023) inampa DPP mamlaka ya kipekee kufanya jukumu hilo bila kujali Sheria nyingine zozote za nchi hii.
Pia wanaeleza DPP amepewa majukumu ya kikatiba na kisheria kuratibu na kusimamia upelelezi na uchunguzi wa makosa ya jinai kasoro makosa yanayohusu mahakama ya kijeshi.
Shauri hilo limepangwa kusikilizwa kesho Jumatatu, Juni Mosi na Jaji Agustine Rwizile, katika hatua hiyo ya awali ya ruhusa ya kufungua shauri hilo.
Katika hatua hiyo waombaji ili mahakama iweze kuwaruhusu kufungua shauri rasmi la kuipinga tume hiyo, wanapaswa kuithibitishia kuwa wamekidhi matakwa ya kisheria ya kupewa ruhusa hiyo.
Matakwa hayo ni kuonesha kuna hoja inayobishaniwa inayopaswa kutolewa uamuzi, kwamba wana maslahi katika jambo wanalolilalamikia na kwamba wamewasilisha maombi hayo ndani ya wakati.