
Dar es Salaam. Simba Queens imejihakikishia ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania (TWPL) baada leo Jumapili, Mei 31, 2026 kuibuka na ushindi mnono wa mabao 5-2 dhidi ya Mashujaa Queens kwenye Uwanja wa KMC Complex, Dar es Salaam.
Matokeo ya mchezo wa leo, yameifanya Simba Queens kufikisha pointi 56 ambazo haziwezi kufikiwa na timu nyingine yoyote katika ligi hiyo msimu huu.
Mabao ya ushindi ya Simba Queens katika mechi ya leo yamefungwa na Zainah Nandedeh, Aisha Mnunka, Jentrix Shikangwa aliyepachika mawili na moja likiwa la kujifunga la Mashujaa Queens.
Mabao ya Mashujaa Queens leo yamewekwa kimiani na Sabina Mbuga na Zainab Mohamed.
Hii ni mara ya tano kwa Simba Queens kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake Tanzania na ndio timu inayoongoza kwa kuchukua ubingwa huo mara nyingi nchini.
Mara nne zilizopita, Simba Queens ilitwaa ubingwa katika misimu ya 2019/2020, 2020/2021, 2021/2022 na 2023/2024.
Timu inayoshika nafasi ya pili kwa kutwaa taji hilo mara nyingi ni JKT Queens iliyochukua mara nne na Mlandizi Queens imetwaa mara moja.
Katika Uwanja wa Meja Jenerali Isamuhyo, wenyeji JKT Queens wamelazimishwa sare ya bao 1-1 na Yanga Princess.
Bao la JKT Queens limepachikwa na Donisia Minja na kwa upande wa Yanga Princess aliyewafungia ni Jeannine Mukandayisenga.