Unguja. Kwa mara ya kwanza meli ya kimataifa ya mafuta kutoka Saudia Arabia imeshusha petroli, dizeli na mafuta ya ndege katika Bandari Jumuishi ya Mangapwani.

Akizungumza baada ya kupokea meli hiyo leo Mei 31, 2026, Katibu Mkuu Wizara ya Maji, Nishati na Madini, Joseph Kilangi amesema meli hiyo kushusha mafuta moja kwa moja Zanzibar inaonesha kuendelea kuimarika kwa miundombinu ya uhifadhi wa rasiliamali hiyo.

Pia, amesema hatua hiyo inatokana na dhamira ya dhati ya Serikali ya awamu ya nane kuamua kuifanya Bandari ya Mangapwani kuwa jumuishi ikiwemo ushushaji wa nishati ya mafuta.

“Zanzibar ilikuwa na changamoto ya upungufu wa mafuta kwa kipindi kirefu kipindi cha nyuma japo sio kwa kiasi kikubwa kutokana na vita vinavyoendelea mashariki ya kati kwa nchi ya Israel, Iran na Marekani na tulikuwa na mletaji mmoja wa mafuta kutoka Tanga,” amesema.

Amesema tayari mkataba na mtu huyo wameshamaliza na waliingia mkataba mwingine na Kampuni ya One Petrolium (OP) ambapo kwa mara ya kwanza imeleta meli yake na mara ya kwanza Zanzibar, inashusha mafuta mengi kuliko kipindi kingine chochote huko nyuma.

Amesema mafuta hayo lita milioni 36 yanategemewa kutumika kwa muda wa mwezi mzima.

“Tukimaliza kushusha, meli hii inarudi tena Saudi Arabia kwenda kuchukua mafuta na kuja moja kwa moja hapa, hatua ambayo itapunguza gharama za uendeshaji na tunaamini hali ya vita ikitulia bei ya mafuta itashuka Zanzibar,” amesema.

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti Nishati na Maji (Zura), Rashid Abdullah Fadhil amesema meli hiyo yenye jina la MT CLEAROCEAN MIRACLE imekuja na lita 36,271,100.

Amesema mafuta hayo ni petroli lita 14,702,045, dizeli lita 11,476,3926 na mafuta ya ndege lita 10,092,663.

Amesema mara nyingi Zanzibar ilikuwa ikipokea meli ndogondogo kwa ajili ya ushushaji wa mafuta kiwango ambacho kilikuwa hakitoshelezi.

“Tutakuwa hatuna upungufu tena wa mafuta kwa kipindi cha mwezi mzima na pia itaondoa usumbufu wa meli ndogo ndogo kwenda Dar es salam ambapo mara nyingi kuna msongamano wa meli na kusababisha upungufu wa mafuta Zanzibar kupatikana kirahisi,” amesema.

Rashid amesema pia itaondosha usumbufu wa meli ndogo kwenda Mombasa ambako pia hujitokeza msongamano wa meli huko na kusababisha Zanzibar kukosekana kwa mafuta.

Amebainisha kwamba huo ni mwanzo na wanatarajia itakuwa ni muendelezo mwezi ujao kuanzia 25 hadi 30 meli nyingine itaingia Zanzibar kwa ajili ya kushusha rasilimali hiyo.

“Tumeona tuje na ubunifu huu kwa sababu duniani tunaona hali ilivyo ili tuwe na uhakika wa mafuta hapa nchini na tunaamini hali ikitulia Afrika ya kati basi bei ya mafuta itashuka,” amesema.

Amewatoa hofu wananchi kuwa wasitarajie kwamba Zanzibar itakuwa na upungufu wa mafuta.

Dk Mohammead Jameel ni Mkuu wa Biashara Kampuni ya One Petrolium, amesema kampuni hiyo itahakikisha kila mwezi mafuta yanakuwa yanaingia Zanzibar kutoka Saudia Arabia ambayo itaweka uhakika wa upatikanaji wa nishati hiyo itakayopunguza gharama za kusafirisha nishati hiyo mara kwa mara.

“Kila mwezi meli zetu zitakuwa zinaleta nishati hii ili kuhakikisha hakuna upungufu na wananchi wanapata nishati hiyo kwa uhakika,” amesema

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *